Uchunguzi wa Afya kwenye Kazi: JKCI yawafikia Watumishi wa Serikali

Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo kwa sasa inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Salehe Mwinchete akitoa elimu ya magonjwa ya moyo kwa watumishi wa umma wanaoshiriki Kikao kazi cha 6 cha Serikali Mtandao kinachofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC) . Wataalamu wa JKCI wanatoa huduma ya Uchunguzi na matibabu ya moyo kwenye kikao kazi hicho.

Mtaalamu wa vipimo vya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Beatrice Mwakabende akimpima Mtumishi wa Umma kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi wakati wa  Kikao kazi cha 6 cha Serikali Mtandao kinachofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC).


Afisa Uuguzi wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo kwasasa inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nadia Zuberi akimpima kipimo cha kuangalia uwiano baina ya urefu na uzito (BMI) Mtumishi wa Umma aliyehudhuria Kikao Kazi cha 6 cha Serikali Mtandao kinachofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mikutano  wa Arusha (AICC).

*******************************************************************************************************************************************************************************************

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeendelea kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watumishi wa umma kwakuweka kambi maalumu ya siku tatu katika Kikao Kazi cha 6 cha Serikali Mtandao (e-GA) kinachofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC).

Akizungumza wakati wa kambi hiyo Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo kwasasa inasimamiwa na JKCI Dkt. Salehe Mwinchete alisema watumishi wa umma mara nyingi hukosa muda wa kupima afya zao kutokana na majukumu ya kikazi, hivyo JKCI hutumia mikutano kama jukwaa la kuwafikia na kuwapatia huduma za kinga mapema.

“Tuko hapa AICC katika mkutano wa watendaji wa serikali kupitia eGA ambapo washiriki wengi ni watumishi wenye majukumu mengi na wanakosa muda wa kwenda hospitali kupima na JKCI imekuwa na utamaduni wa kushiriki katika hafla kama hizi ili kuwasogezea huduma za uchunguzi wa afya”, alisema Dkt. Mwinchete.

Dkt. Mwinchete ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo alisema  juhudi hizo za Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) zinaendana na mikakati ya kimataifa ya afya inayohimiza uchunguzi wa mapema wa magonjwa yasiyoambukiza.

“Dunia kwa sasa kupitia mikakati ya afya ya kimataifa inayosisitiza uchunguzi na ugunduzi wa mapema wa magonjwa yasiyoambukiza, fursa kama hii ni adimu kwa washiriki wa mkutano kufanya vipimo vya awali vinavyoweza kubaini vihatarishi vya magonjwa hayo”, alisema Dkt. Mwinchete.

Kwa upande wake Afisa Utumishi wa Bodi ya Maziwa Tanzania Viktoria Masanja aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuwaletea huduma hizo karibu na eneo la mkutano huku akisema watumishi wengi hutumia muda mwingi ofisini na hupata changamoto ya kwenda kupima afya hadi wanapolazimika kwenda kupima baada ya kupata  maradhi.

“Kwa sisi tunaokaa muda mrefu ofisini mara nyingi hatuendi kupima afya mpaka tatizo likusukume, kupitia kikao kazi hiki cha eGA tumepata fursa ya kufika kwenye banda la JKCI na kupima afya zetu na nimepata ushauri mzuri hasa kuhusu uzito wangu na namna ya kuudhibiti”, alisema Viktoria.

Naye Afisa TEHAMA wa Bodi ya Maziwa Tanzania Legani Maikomole alisema hana mazoea ya kwenda hospitalini mara kwa mara kupima afya  licha ya kuwa na changamoto za kiafya lakini ujio wa huduma hizo umempa nafasi ya kupima afya yake.

“Mimi sina mazoea ya kwenda hospitalini mara kwa mara lakini leo nimepata nafasi ya kupima afya yangu na kupata ushauri mzuri wa kitaalamu, sasa ni jukumu langu kufanyia kazi maelekezo niliyopewa ili kuepuka matatizo makubwa ya kiafya”, alisema Legani.

Ushiriki wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika mikutano ya kitaifa unaendelea kuwa chachu ya kuongeza uelewa wa umuhimu wa kupima afya na kuwafikia makundi ambayo kwa kawaida hupata changamoto ya kupata muda wa kufika hospitalini hatua inayochangia kupunguza mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza nchini.

Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi

Msumbiji kushirikiana na JKCI katika tiba ya moyo