Viatu vyenye kisigino kirefu hatari kwa afya ya magoti.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Beatrice Nangawe akitoa elimu ya afya bora kwa wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD) wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi wa afya iliyofanyika hivi karibuni katika ofisi za MSD Kanda ya Mabibo jijini Dar es Salaam.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed Aloyce akimpa ushauri mmoja wa wafanyakazi wa Bohariy a Dawa (MSD) wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi wa afya iliyofanyika hivi karibuni katika ofisi za MSD Kanda ya Mabibo jijini Dar es Salaam.

Daktari bingwa wa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Theophilly Mushi akitoa elimu kuhusu magonjwa ya moyo kwa wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD) wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi wa afya iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa JKCI hivi karibuni katika ofisi za MSD Kanda ya Mabibo jijini Dar es Salaam.

Mtaalamu wa mazoezi tiba wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Jackline Mariki akitoa elimu kuhusu umuhimu wa afya ya viungo kwa wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD) wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi wa afya iliyofanyika hivi karibuni katika ofisi za MSD Kanda ya Mabibo jijini Dar es Salaam.


Baadhi ya wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD) wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa na wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi wa afya kwa wafanyakazi wa MSD iliyofanyika hivi karibuni katika ofisi za MSD Kanda ya Mabibo jijini Dar es Salaam.

Picha na: JKCI

****************************************************************************************************************************

Wanawake wametakiwa kuzingatia uvaaji wa viatu vyenye kisigino kifupi kuimarisha afya ya miguu na kuepuka kuvaa viatu vyenye kisigino kirefu ama kisigino flati ambavyo ni hatari kwa afya ya magoti.

Hayo yamesemwa na Mtaalamu wa mazoezi tiba kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Jaqline Mariki wakati akizungumza na wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD) katika kambi ya matibabu ya siku mbili ya uchunguzi wa afya iliyofanyika katika ofisi za MSD Kanda ya Mabibo jijini Dar es Salaam.

Jaqline alisema mtu anatakiwa kuvaa viatu vyenye kisigino kifupi ili unyayo uweze kunyanyuka kidogo kusaidia ugawanyishwaji wa uzito kwenye mwili hivyo kutoleta maumivu katika mwili.

“Tunashauri wanawake wasivae viatu virefu au vile ambavyo ni flati bali wavae viatu ambavyo vina kisigino kifupi ili unyayo uweze kunyanyuka kidogo, kwani uvaaji wa viatu vyenye kisigino kirefu unaweza kusababisha ulemavu wa miguu”, alisema Jaqcline

Aidha, mtaalamu huyo alihimiza wafanyakazi kuwa na utamaduni wa kunywa maji ya kutosha ili kuuweka mwili katika hali bora ya kiafya, akieleza kuwa ukosefu wa maji mwilini unaweza kusababisha maumivu ya kichwa, uchovu na kupungua kwa ufanisi wa kazi.

“Kama tunavyofahamu wafanyakazi wengi maofisini hawapendelei kunywa maji mengi kwasababu muda mwingi wanautumia wakiwa wamekaa, jambo ambalo linaweza kusababisha maumivu ya kichwa na kupunguza ufanisi wa kufanya kazi”, aliongeza Jaqckline.

Kwa upande wao wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD) waliopatiwa mafunzo hayo wameshukuru kwa kupatiwa uelewa mpana kuhusu afya ya moyo, viungo vya mwili pamoja na matumizi sahihi ya dawa za kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

“Nilikuwa sifahamu kabisa kama ugonjwa wa homa ya ini unaweza kusababisha saratani, kupitia mafunzo hayo nitahakikisha nakuwa makini kwa kuchukua hatua ya kupima na kupata chanjo”, alisema Haika Regnald

“Binafsi mafunzo haya na upimaji huu ni fursa nzuri kwangu kuweza kujua hali yangu ya moyo, kisukari na uzito kwani katika mafunzo haya tumesisizwa kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi ya mara kwa mara” alisema Ally Mlete.


Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi

Msumbiji kushirikiana na JKCI katika tiba ya moyo