Viongozi wa JKCI SACCOS watakiwa kufanya uwekezaji

Mwenyekiti wa Bodi ya SACCOS ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tulizo Shemu akizungumza na wanachama wa SACCOS hiyo wakati wa mkutano mkuu wa sita uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa PSSF uliopo Makumbusho jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwaeleza wanachama wa SACCOS ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) umuhimu wa kuwekeza wakati wa mkutano Mkuu sita wa Chama hicho uliofanyika  mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa PSSF uliopo Makumbusho jijini Dar es Salaam. 

Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Abdulhakim Haidar akitoa ufafanuzi kuhusu uwekezaji kwa wanachama wa SACCOS ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa mkutano mkuu wa sita wa SACCOS hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa PSSF uliopo Makumbusho jijini Dar es Salaam.

Mjumbe wa SACCOS ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Sophia Bishashara akichangia mada wakati wa mkutano mkuu wa sita wa SACCOS hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa PSSF uliopo Makumbusho jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu wa Sita wa SACCOS ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Engarasiya Kifai akiongoza mkutano huo uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa PSSF uliopo Makumbusho jijini Dar es Salaam.




Wajumbe wa SACCOS ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia mada zilizokuwa zikijadiliwa wakati wa mkutano mkuu wa sita wa SACCOS hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa PSSF uliopo Makumbusho jijjini Dar es Salaam.

Picha na: JKCI

*******************************************************************************************************

Uongozi wa Bodi ya SACCOS ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) umetakiwa kutumia njia za kisasa katika kuwekeza na kukuza mtaji wa SACCOS hiyo.

Rai hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa mkutano mkuu wa sita wa SACCOS hiyo uliofanyika katika ukumbi wa PSSF uliopo makumbusho jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kisenge alisema SACCOS hiyo imeonesha muelekeo mzuri wa ukuaji kwani sasa kuna ongezeko kubwa la amana na mikopo lakini pia kumekuwa na uboreshwaji wa mifumo ya utoaji huduma kwa kutumia teknolojia ya kidigitali kuwezesha mikopo kupatikana kwa wakati.

“Nichukue nafasi hii kuipongeza bodi ya JKCI SACCOS kwa kazi nzuri yenye mafanikio kwani mtaji umezidi kuongezeka, mafanikio haya hayajatokea kwa bahati nasibu bali ni matokeo ya nidhamu, uwajibikaji na maamuzi sahihi yaliyofanywa na wanachama wote”, alisema Dkt. Kisenge

“Fikirieni njia mbalimbali za uwekezaji ambazo zinaweza kukuza mtaji kwa haraka, mnaweza kuwekeza kwenye mazoezi kwa kuwa na gym ambayo inakuwa na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, hii itaifanya gym hiyo kuaminiwa na watu na hivyo kupata wateja wengi hivyo kuongeza mtaji wa SACCOS”, alisema Dkt. Kisenge

Dkt. Kisenge alisema sasa ni wakati wa bodi ya SACCOS hiyo kufikiria njia mbalimbali za uwekezaji kwa kuwa wabunifu lakini pia kuangalia namna ya kuongeza wanachama wapya katika SACCOS hivyo kuongeza mtaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya SACCOS ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tulizo Shemu alisema SACCOS hiyo imeendelea kuwavutia wengi kwani kumekuwa na ongezeko kubwa la wanachama ukilinganisha na mwaka 2025.

“Ongezeko la wanachama linathibitishwa na ongezeko la akiba kutoka bilioni 1.2 mwaka 2024 hadi kufikia shilingi Bilioni 1.8 kwa mwaka 2025, hii itakuwa fursa kwetu kuendelea kuwekeza zaidi na kutengeneza faida zinazotokana na mikopo mikubwa”, alisema Dkt. Shemu.

Akitoa mafunzo kuhusu amana na mikopo Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Mihayo Malunde alisema licha ya wanachama kunufaika na mikopo kwa riba nafuu vyama vya ushirika vina wajibu wa kuendeleza  na kuboresha huduma za jamii kama afya, maji na elimu.

“Endeleeni kuhamasishana kwa pamoja muendelee kujiwekea akiba, rejesheni mikopo kwa wakati ili kuiwezesha SACCOS yenu kuwa na mtiririko wa fedha kwa mahitaji mengine ya kijamii”, alisema Mihayo.

Naye mwanachama wa JKCI SACCOS ambaye ni Afisa Uuguzi katika taasisi hiyo Uledy Uledy alisema amevutiwa kujiunga na SACCOS hiyo ili aweze kuwekeza akiwa na uhakika wa kupata mkopo wakati wowote akiwa na uhitaji na mkopo.

“Mimi ni mwanachama mpya na nimeingia kwenye SACCOS hii baada ya kupata elimu ya kutosha kwa wanachama walionitangulia, mbali na SACCOS hii kunufaika na kutoa mikopo yenye riba nafuu pia wanachama tunafaidika na gawio linalotolewa kila mwisho wa mwaka ambalo linatusaidia kutatua changamoto za kifedha”, alisema Uledy


Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi

Msumbiji kushirikiana na JKCI katika tiba ya moyo