Serikali yagharamia milioni 758 matibabu ya Wagonjwa wa Moyo
Serikali imegharamia jumla ya shilingi milioni 758,178,091 kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa wa moyo wasiokuwa na uwezo wa kulipia huduma hizo pamoja na kusamehe gharama za miili ya marehemu waliokuwa wakipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza na mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam kuhusu siku 100 za utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kugharamia matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa wa moyo wasiokuwa na uwezo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dkt. Peter Kisenge, alisema serikali ya awamu ya sita imeendelea kuweka mkazo katika kuwasaidia wananchi wenye uhitaji maalum.
Dkt. Kisenge alisema watu 122 wakiwemo watu wazima 52 na watoto 70 walifanyiwa upasuaji wa moyo ambao uligharimu kiasi cha Tshs. 698,448,760. Watu 177 wanawake wakiwa 76 na wanaume 101 walipatiwa huduma za uchunguzi wa matibabu katika kliniki ya moyo, huduma hizo ziligharimu kiasi cha Tshs. 2,670,000.
Dkt. Kisenge alisema watu sita waliopoteza maisha wakati wakipatiwa matibabu na ndugu zao kushindwa kulipia gharama za matibabu hivyo Serikali iligharamia kiasi cha Tshs. 22,059,331 ili miili ya marehemu ichukuliwe na kwenda kuzikwa na ndugu zao.
“Kupitia upasuaji wa kisasa wa kubadilisha valvu ya moyo kwa njia ya tundu dogo bila kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation - TAVI) mgonjwa mmoja alifanyiwa upasuaji huo ambapo serikali iligharamia kiasi cha Tshs. 35,000,000/=”, alisema Dkt. Kisenge
Aidha Dkt. Kisenge alisema katika kusogeza huduma za ubingwa bobezi za uchunguzi na matibabu ya moyo ya kuwafuata wananchi mahali walipo ili kuwapunguzia gharama ya kuzifuata huduma hizo Dar es Salaam ndani ya siku 100 JKCI imewafanyia uchunguzi na matibabu ya moyo wananchi 3,053.
“JKCI ilifanya kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo katika michuano ya Chipukizi Cup iliyofanyika jijini Arusha ambapo jumla ya watu 450 walifanyiwa uchunguzi wa afya kati yao watoto walikuwa 440 na watu wazima 10”, alisema Dkt. Kisenge
Kadhalika JKCI ilifanya kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa mashibiki wa timu za mpira wa miguu za Simba na Yanga iliyofanyika jijini Dar es Salaam ambapo jumla ya watu 175 walifanyiwa uchunguzi wa afya, watu 12 walikutwa na matatizo ya moyo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa walipewa rufaa ya kufika JKCI kwaajili ya uchunguzi zaidi.
“Kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali ilifanyika katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambapo watu 3,053 walichunguzwa afya zao, watu wazima walikuwa 2,602 na watoto 451. Katika kambi hiyo watu 63 walikutwa na magonjwa ya moyo na kupewa rufaa ya kufika JKCI kwaajili ya uchunguzi na matibabu zaidi”, alisema Dkt. Kisenge
Aidha JKCI
iliweza kufikisha huduma za uchunguzi na matibabu mahali pa kazi na kutoa elimu
ya magonjwa ya moyo pamoja na kufanya uchunguzi wa magonjwa hayo kwa
wafanyakazi 211 wa Bohari ya Dawa (MSD).
.jpeg)
Comments
Post a Comment