Ziara ya Kujifunza: Viongozi wa Congo wapata huduma za kibingwa za Moyo JKCI
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpima Shinikizo la damu (BP) Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Said Juma Mshana alipofika katika Taasisi hiyo leo kwaajili ya kufanya uchunguzi wa afya.
Mtaalamu wa vipimo vya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Loyce Victor akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanyakazi
(Echocardiograph – ECHO) mjumbe kutoka jimbo la Maniema wakati wajumbe hao
walipotembelea JKCI tawi la Oysterbay leo kwaajili ya kufanya uchunguzi wa afya
Gavana wa jimbo la Maniema Mhe. Mussa Kabwankubi Moise pamoja na wajumbe kutoka jimbo hilo wakisubiri kupata huduma alipofika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tawi la Oysterbay leo kwaajili ya kufanya uchunguzi wa afya.
Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(DRC) Mhe. Said Juma Mshana akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na wafanyakazi wa
Taasisi hiyo mara baada ya kupata huduma za uchunguzi wa afya leo katika Tawi
la Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Na JKCI
**************************************************************************************************
Uwekezaji wa Tanzania katika sekta ya afya umeendelea kuvuka
mipaka baada ya ujumbe wa viongozi 15 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(DRC), ukiongozwa na Gavana wa Jimbo la Maniema kufanyiwa uchunguzi wa moyo na
kuvutiwa na ubora wa huduma katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Ujumbe huo ulipatiwa huduma katika tawi la JKCI lililopo
Oysterbay, jijini Dar es Salaam kufuatia ziara yao ya kujifunza kuhusu
mafanikio ya Tanzania katika huduma za afya bingwa na bobezi zikiwemo za
matibabu ya moyo.
Akizungumza baada ya kufanyiwa uchunguzi huo Balozi wa
Tanzania nchini DRC, Mhe. Said Juma Mshana alisema ziara hiyo imelenga kuwaonesha
viongozi hao namna Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan ilivyowekeza kwa kiwango kikubwa katika hospitali za umma.
Balozi huyo ambaye pia anaiwakilisha Tanzania katika nchi za
Congo Brazzaville, Afrika ya Kati, Cameroon, Cab Bon na Equatorial Guinea
alisema anakusudia mwezi ujao kuwaleta magavana kutoka majimbo ya Lualaba na
Haut Katanga yaliyopo nchini DRC ili kujifunza jinsi ambavyo Tanzania imesonga
mbele katika sekta ya afya.
Alibainisha kuwa mwezi ujao anatarajia kuwaleta magavana
kutoka majimbo ya Lualaba na Haut Katanga kwa ziara kama hiyo ya kujifunza na
kubadilishana uzoefu.
"Kwa niaba ya ujumbe wangu, tunamshukuru Dkt. Kisenge na
menejimenti ya JKCI kwa mapokezi mazuri na kwa kutupatia huduma ya uchunguzi na
matibabu ya moyo bila gharama. Huu ni ushahidi wa moyo wa kiungwana na ubora wa
huduma zinazotolewa hapa", alisema Mhe. Balozi Mshana.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge alisema ujumbe huo umefurahishwa na
uwekezaji wa Serikali katika hospitali za umma huku akibainisha kuwa katika DRC
sekta binafsi ndiyo yenye mchango mkubwa zaidi katika huduma za afya.
"Tuna kila sababu ya kujivunia uongozi wa Mhe. Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika huduma za afya, hususan
huduma za kibingwa na kibobezi ambazo sasa zinavutia hata wageni kutoka nje ya
nchi", alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema ujumbe kutoka Congo umefurahia huduma za
JKCI, mapokezi, vipimo walivyofanyiwa na kuahidi kuwa mabalozi wazuri kwa
kuelezea uwekezaji uliofanywa Tanzania katika sekta ya afya watakaporudi nchini
kwao.
Naye Mshauri wa Masuala ya Biashara kutoka DRC, Dkt. George
Oyema alisema licha ya kutembelea nchi nyingi ikiwemo Marekani, India na China
amevutiwa na kiwango cha teknolojia na utaalamu aliouona JKCI.
"Nimeona mashine za kisasa na huduma zenye viwango vya
juu kabisa matibabu ya moyo. Hii ni taasisi inayoweza kushindana kimataifa”.
“Tunawashukuru sana Taasisi hii inayojihusisha na matibabu ya
moyo kwa kutupatia nafasi ya kuangalia afya zetu tumefurahi sana, watu hawa
wana upendo wa aina yake”, alisema Dkt. Oyema
Ziara hiyo imeongeza sura ya Tanzania kama kitovu cha huduma
za afya za kibingwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huku ushirikiano
kati ya nchi hizo mbili ukiendelea kuimarika katika nyanja za afya na
uwekezaji.





Comments
Post a Comment