Watu 253 wafanyiwa uchunguzi wa afya mkutano wa e-GA
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
Ridhiwani Kikwete akimpatia tuzo Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Hospitali ya
Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo kwa sasa inasimamiwa na Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Salehe Mwinchete kutambua na kuthamini mchango
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa kufunga kikao kazi cha sita
cha Serikali Mtandao kilichofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa
Arusha (AICC) jijini Arusha.
Daktari
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Sahiya Yahya akimsikiliza mmoja wa
wafanyakazi aliyepata huduma wakati wa kambi maalumu ya siku tatu ya uchunguzi
na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha sita cha Serikali Mtandano
kilichofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Arusha (AICC) jijini
Arusha.
Mtaalamu wa vipimo vya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Beatrice Mwakabende akimpima mmoja wa wafanyakazi aliyefika katika kambi maalumu ya siku tatu ya uchunguzi na matibabu ya moyo kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi wakati wa Kikao kazi cha sita cha Serikali Mtandao kilichofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC) jijini Arusha.
Daktari
wa Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo kwasasa inasimamiwa na Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Advotus Kimomogoro akizungumza na mmoja wa
wafanyakazi aliyefika kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo wakati wa kambi
maalumu ya siku tatu ya uchunguzi na matibabu ya moyo katika Kikao kazi cha sita
cha Serikali Mtandao kinachofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano
(AICC) jijini Arusha.
Na JKCI
*************************************************************************************************************
Watu
253 wakiwemo wanaume 140 na wanawake 113 wamepatiwa huduma za uchunguzi na
matibabu ya magonjwa ya moyo katika kambi maalumu ya siku tatu iliyofanyika
wakati wa kikao kazi cha sita cha Serikali Mtandao (e-GA) katika Ukumbi wa
Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC).
Katika
kambi hiyo watu 49 walihitaji uchunguzi wa kitaalamu zaidi hivyo kupewa rufaa
ambapo watu 28 walipewa rufaa kwenda JKCI, watu 13 walipewa rufaa kwenda Arusha
Lutheran Medical Centre (ALMC) na watu nane walipewa rufaa kwenda hospitali
nyingine kwa ajili ya matibabu zaidi.
Akizungumza
wakati wa kuhitimisha kambi hiyo Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Hospitali ya
Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo kwasasa inasimamiwa na JKCI Dkt.
Salehe Mwinchete alisema mwitikio wa washiriki wa kikao hicho umekuwa mkubwa ambao
umetoa fursa kwa washiriki hao kuweza kupata taarifa sahihi zinazohusu magonjwa
yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.
“Washiriki
wa mkutano huu wameweza kufanyiwa uchunguzi wa afya kwa kuwapima vipimo vya
awali kuangalia viashiria vya magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, sukari
kwenye damu, magonjwa ya moyo na mishipa ya damu ya moyo lengo likiwa
kuwasaidia washiriki kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa ya moyo”,
“Wapo
watu tuliowakuta na matatizo ya mishipa ya damu ya moyo kuziba, mapigo ya moyo
kutokuwa sawa pamoja na ugonjwa wa kisukari hali inayoashiria uwepo wa
vihatarishi vya magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Salehe
Dkt.
Salehe alisema kumekuwa na changamoto ya mwitikio mdogo wa vijana kujitokeza
kufanya uchunguzi wa afya, lakini Taasisi hiyo imejipanga na kutengeneza mbinu
za kuwafikia vijana kupitia mikutano na majukwaa ya kijamii.
Kwa
upande wake Afisa TEHAMA wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Emina Mbele alisema
kupitia kambi hiyo ameweza kufaidika na huduma zilizokuwa zinatolewa kwani
ameweza kupima shinikizo la damu, sukari kwenye damu, uzito na kufanyiwa kipimo
cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO).
“Nawahamasisha
watu wapime afya zao hata kama hawana dalili kwa sababu huduma hii imeletwa
karibu nasi kupitia kikao chetu, tusiogope tujitokeze kwa wingi kuchunguza afya
zetu”, alisema Emina.
Naye
Afisa TEHAMA wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Geofrey Justine alisema
ameridhishwa na mapokezi na huduma alizopata kutoka kwa wataalamu wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kuishauri Taasisi hiyo kuendelea kuwafikia
wananchi wengi zaidi ili waweze kupungua idadi ya watu wanaopata magonjwa ya
moyo.
“Ninaomba
huduma kama hizi zisiishie kwenye mikutano mikubwa tu, bali ziende hadi mikoani
ambako watu wengi wana changamoto za afya ikiwemo magonjwa ya moyo”, alisema Geofrey
Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa ikifanya kambi maalumu katika mikutano
mbalimbali nchini ikiwa ni mkakati wa kusogeza huduma karibu na wananchi,
kuongeza uelewa, kuhamasisha uchunguzi wa afya mapema na kupunguza tatizo la
magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.




Comments
Post a Comment