Siku ya Msikilizaji Habari Maalum Media yaleta uchunguzi wa Moyo bure Ngaramtoni
Matroni wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Sr. Flora Kasembe akitoa elimu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Msikilizaji yaliyoandaliwa na Habari Maalum Media na kufanyika Ngaramtoni jijini Arusha.
Wakazi wa Arusha wakisubiri kupata huduma ya upimaji wa
magonjwa ya moyo iliyokuwa inatolewa na wataalamu wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center
(ALMC) inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Msikilizaji
yaliyoandaliwa na Habari Maalum Media na kufanyika Ngaramtoni jijini Arusha.
Matroni wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC)
inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Sr. Flora Kasembe
akimpima shinikizo la damu mkazi wa Arusha wakati wa maadhimisho ya Siku ya
Msikilizaji iliyoandaliwa na Habari Maalum Media na kufanyika Ngaramtoni jijini
Arusha.
Na JKCI
***********************************************************************************************************
Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC)
inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imetoa huduma za upimaji
wa magonjwa ya moyo na elimu ya afya kwa mamia ya wananchi katika maadhimisho
ya Siku ya Msikilizaji yaliyoandaliwa na Habari Maalum Media, yaliyofanyika
Ngaramtoni mkoani Arusha.
Katika tukio hilo lililowakutanisha zaidi ya wasikilizaji 400
wa kituo hicho, wananchi walipata fursa ya kupima afya za mioyo yao, kupimwa
viashiria mbalimbali vya hatari pamoja na kupewa elimu kuhusu namna ya
kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza hususan magonjwa ya moyo.
Akizungumza wakati wa utoaji wa huduma hizo, Matroni wa
Wauguzi wa ALMC, Sr. Flora Kasembe alisema zoezi hilo limekuwa na mafanikio
makubwa kwa kuwa limewafikia wananchi wengi ambao hawapati muda wa kufika hospitalini
kwa uchunguzi wa afya.
Alisisitiza kuwa uchunguzi wa afya mara kwa mara ni muhimu
katika kugundua matatizo ya kiafya mapema na kuanza matibabu kwa wakati hatua
inayosaidia kupunguza madhara makubwa, gharama za matibabu na vifo vinavyoweza
kuzuilika.
“Wananchi wengi hupata matatizo makubwa ya kiafya kwa
kuchelewa kugundua magonjwa. Tunawahamasisha kujenga utaratibu wa kupima afya
zenu mara kwa mara ili kuzuia madhara yanayoweza kuepukika”, alisema Sr. Flora.
Aidha Sr. Flora ambaye ni Afisa Muuguzi aliwataka wananchi
kujitokeza kwa wingi katika kambi maalumu za huduma za kibingwa zitakazofanyika
bila malipo katika Hospitali ya ALMC,
ikiwemo kambi ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya mifupa na mishipa ya fahamu watakayoifanya kwa kushirikiana na wataalamu
kutoa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo
Muhimbili (MOI) tarehe 23-27/02/2026.
"Kambi nyingine ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya
moyo tutaifanya tarehe 27-28/2/2026 kwa kushirikiana na wataalamu wenzetu
kutoka Shirika la Heart to Heart Association for Sustainable Develepment la nchini
Misri", alisema Sr. Flora.
Baadhi ya wananchi waliopata huduma ya uchunguzi wa moyo
walieleza kufurahishwa kwao na upatikanaji wa huduma za bure karibu na makazi
yao huku wakisema imewasaidia kufahamu hali zao za afya na kupata ushauri wa
kitaalamu bila gharama.
Ernest Mollel mkazi wa Ngaramtoni alisema huduma hiyo imekuwa
ya manufaa makubwa kwa jamii kwani watu wengi hawana tabia ya kupima afya hadi
wanapoumwa.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, upimaji wa mara kwa mara ni
silaha muhimu katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kwani husaidia
kugundua vihatarishi mapema na kuwezesha kupata tiba na kufanya mabadiliko ya
mtindo wa maisha kabla hali haijawa mbaya.
Kupatikana kwa huduma hizo ni sehemu ya jitihada za kusogeza
huduma za kibingwa karibu na wananchi na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu
umuhimu wa kinga na uchunguzi wa mapema.




Comments
Post a Comment