Watu 138,699 wapata huduma za matibabu Hospitali ya Dar Group mwaka 2025
Mkurugenzi wa Hospitali
ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Dkt. Tulizo
Shemu akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya hospitali hiyo kwa
mwaka 2025 leo wakati wa mkutano huo uliofanyika katika hospitali hiyo iliyopo
Tazara jijini Dar es Salaam.
Na: JKCI
***********************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group imetoa huduma za upimaji na matibabu ya magonjwa
mbalimbali kwa watu 138,699 kwa mwaka 2025.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Hospitali ya Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Dkt. Tulizo Shemu alisema watu wazima 124,959 na watoto 13,740
walipatiwa matibabu mwaka 2025 huku wagonjwa 4,144 kulazwa
katika hospitali hiyo kwaajili ya matibabu.
Dkt. Shemu alisema ukilinganisha na mwaka 2024 Hospitali hiyo ilitoa huduma kwa wagonjwa 133,756 kati yao watu wazima walikuwa 109,931 na watoto 23,825 hivyo kuwa na ongezeko la wagonjwa 4,943 huku idadi ya watoto ikipungua na idadi ya watu wazima ikiongezeka.
“Huduma
zilizotolewa kwa wagonjwa zilikuwa ni za matibabu ya moyo,
matibabu ya kinywa na meno, kliniki ya magonjwa ya ngozi, matibabu ya magonjwa yanayoambukiza
ikiwemo malaria, huduma za magonjwa ya dharura, kliniki ya wanawake na
wajawazito, kliniki ya macho, kliniki ya pua, masikio na koo”,
“Huduma nyingine
zilikuwa ni kliniki ya mfumo wa mkojo, kliniki ya magonjwa ya tumbo na ini,
kliniki ya magonjwa ya figo, upasuaji mkubwa na mdogo, huduma za fiziotherapia
(mazoezi tiba) na huduma za maabara”, alisema Dkt. Shemu
Aidha Dkt. Shemu
alisema kwa mwaka 2025 JKCI Hospitali ya Dar Group ilitoa huduma mpya ambazo hapo
awali zilikuwa hazitolewi ikiwemo kuangalia shinikizo la damu kwa masaa 24
(ambulatory blood pressure monitoring), matibabu ya kuangalia umeme wa moyo kwa
masaa 24 (ECG Halter Monitoring)
na kipimo cha kuchunguza mishipa ya damu ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo
katika hali ya mazoezi kwa kutumia mashine ya treadmill (Treadmill stress
test).
Kwa
upande mwingine Dkt. Shemu alisema watu 251 walifanyiwa uchunguzi na matibabu
ya magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya moyo, ngiri, vidonda sugu, matatizo
ya mifupa na mgongo pamoja na tiba ya kinywa na meno kupitia huduma
za tiba mkoba zijulikanazo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach
Services zilizofanyika
katika viwanja vya Mbagala wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
“Kupitia
kambi hiyo jumla ya watu 198 walikutwa na magonjwa mbalimbali na hivyo kupewa
rufaa ya kufika JKCI Hospitali ya Dar Group kwaajili ya vipimo zaidi na
kuanzishiwa matibabu”, alisema Dkt. Shemu
Dkt. Shemu alisema mwaka 2025 JKCI Hospitali ya Dar Group ilifanya upasuaji kwa wagonjwa 1,874 ikiwemo upasuaji wa mfumo wa mkojo, upasuaji wa mifupa, Upasuaji wa uzazi, Upasuaji wa pua, masikio na koo, Upasuaji wa matatizo mbalimbali ya wanawake na upasuaji wa jumla.
“Hospitali hii imeongeza urahisi wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi waishio Temeke, Tabata, Mbagala, Chanika, Gongo la Mboto na maeneo mengine ya ukanda huu”, alisema Dkt. Shemu
Upande
wa ajira Dkt. Shemu alisema Serikali kupitia Tume ya Ajira katika Utumishi wa
Umma kwa mwaka 2025 ilitoa ajira mpya kwa wafanyakazi 149 katika kada
mbalimbali zikiwemo za afya, utawala, uhasibu, ugavi, ICT, na nyinginezo.



Comments
Post a Comment