Wafanyabiashara Kariakoo Kunufaika na Huduma za Afya Baada ya JKCI Kufungua Kliniki Mpya
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Alex Msoka akiwaelezea viongozi huduma zitakazotolewa katika
kliniki mpya ya JKCI iliyofunguliwa leo katika Soko Kuu la Kariakoo lililopo
jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wadau waliofika katika ufunguzi wa kliniki
mpya ya JKCI iliyopo katika Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Hassan Mahmoud Mshinda akizungumza na waandishi wa habari
wakati wa ufunguzi wa Kliniki mpya ya JKCI leo katika Soko Kuu la Kariakoo
jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa
Kliniki mpya ya JKCI leo katika Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo CPA. Ashraph
Abdulkarim akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa Kliniki
mpya ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo katika Soko Kuu la Kariakoo
jijini Dar es Salaam.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Faizat
Ndosa akimpima joto la mwili mwananchi aliyefika katika Kliniki mpya ya JKCI
iliyopo katika Soko Kuu la Kariakoo wakati wa ufunguzi wa kliniki hiyo
uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Hassan Mahmoud Mshinda akiwa katika picha ya pamoja na
viongozi wa Taasisi hiyo mara baada ya kufanya ufunguzi wa Kliniki mpya ya JKCI
iliyopo katika Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Picha na JKCI
***************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) imefungua kliniki mpya katika eneo la Soko Kuu la Kariakoo,
hatua inayolenga kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo
karibu na wafanyabiashara na wananchi wa eneo hilo.
Kliniki hiyo imeanza
kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo bure kwa siku saba kwa
wananchi wote watakaotembelea kabla ya kuendelea na utoaji wa huduma kwa
utaratibu uliopangwa.
Akizungumza wakati wa
uzinduzi huo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya JKCI, Dkt. Hassan Mahmoud
Mshinda alisema uamuzi wa kuanzisha kliniki hiyo umetokana na umuhimu wa
kulinda afya ya wafanyabiashara katika eneo hilo ambalo hupokea maelfu ya watu
kila siku.
“Tunatambua kuwa afya
ni mtaji mkubwa kwa mfanyabiashara hivyo Serikali kupitia JKCI imewekeza katika
miundombinu, wataalamu na vifaa tiba vya kisasa ili kuhakikisha huduma bora zinapatikana
karibu na wananchi”, alisema Dkt. Mshinda.
Dkt. Mshinda aliwahimiza
wafanyabiashara na wakazi wa Kariakoo kutumia kikamilifu kliniki hiyo kwa
uchunguzi wa afya, matibabu pamoja na kupata elimu ya kujikinga na magonjwa
yasiyoambukiza hususan magonjwa ya moyo.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema kliniki hiyo imewekewa
vifaa tiba vya kisasa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja vikiwemo
vinavyotumia teknolojia ya kisasa kuchunguza na kugundua magonjwa katika hatua
mbalimbali.
Dkt. Kisenge alisema
lengo la taasisi hiyo ni kuhakikisha watu wenye vipato vya aina zote wanapata
huduma kwa urahisi kwani JKCI inafuata kauli mbiu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan ya Kazi na Utu hivyo inajali utu wa watu.
“Kliniki hii pia itatoa
huduma za tiba mtandao kwa wagonjwa watakaohitaji ushauri au ufuatiliaji bila
kufika moja kwa moja hospitalini. Tunataka kuhakikisha hakuna mfanyabiashara
anayepoteza muda au kupata madhara ya kiafya wakati huduma zipo karibu”,
alisema Dkt. Kisenge.
Aliongeza kuwa kliniki
hiyo itakuwa na dawati maalumu kwa wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali
wanaofika Kariakoo kwa shughuli za biashara hivyo wasisite kupata huduma katika
kliniki hiyo.
Naye Meneja Mkuu wa
Shirika la Masoko ya Kariakoo, CPA Ashraph Abdulkarim aliishukuru JKCI kwa
kuwasogezea huduma za kibingwa wafanyabiasha wa Kariakoo na kuwataka
wafanyabiashara hao kutumia fursa hiyo kupima afya zao mara kwa mara.
“Tunawaomba jumuiya ya
wafanyabiashara kuwahamasisha watu wa kariakoo kutumia fursa hii kupima afya
zenu na kupata elimu itakayowasaidia kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza”,
alisema CPA Ashraph
Akitoa neno la shukrani
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo Severin Mushi alisema uwepo
wa kliniki hiyo ni msaada mkubwa kwa eneo hilo ambalo hupokea zaidi ya watu
laki moja kwa siku na ambalo awali halikuwa na huduma ya karibu ya kibingwa ya
magonjwa ya moyo.
“Kariakoo ni eneo lenye
shughuli nyingi za kibiashara na linaweza kukumbwa na dharura za kiafya wakati
wowote uwepo wa huduma hizi utasaidia kuokoa muda na maisha ya watu wengi”,
alisema Mushi.
Aliongeza kuwa
wafanyabiashara wa Kariakoo watapata huduma kwa gharama nafuu kulingana na
utaratibu uliowekwa na JKCI huku akibainisha kuwa pia watashirikiana na taasisi
hiyo katika kampeni za uchangiaji damu wakati wa Wiki ya Wafanyabiashara
inayotarajiwa kufanyika mwezi Aprili mwaka huu.
Kliniki ya JKCI
Kariakoo ni tawi la saba la Taasisi hiyo ukiacha matawi yake mengine ambayo ni
JKCI makao makuu, Kliniki ya Kawe, Kliniki ya Oysterbay, Kliniki ya Chato,
Hospitali ya JKCI Dar Group na Hospitali ya Arusha Lutherani Medical Centre
inayosimamiwa na JKCI.

Comments
Post a Comment