21 wafanyiwa upasuaji wa moyo ndani ya siku tano
Wataalamu wa upasuaji wa
moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na
mwenzao kutoka nchini Ujerumani Benjamin Bierbach
wakimfanyia upasuaji mtoto aliyezaliwa
na mshipa mmoja badala ya miwili unaotoa damu kwenye moyo (Truncus Arteriosus),mtoto
huyo alifanyiwa upasuaji wa kutengeneza mshipa mmoja wa kupeleka damu kwenye
mwili (Aorta) na mwingine kupeleka damu kwenye mapafu (Pulmonary Artery). Upasuaji
huo umefanyika katika kambi maalum ya siku tano ya upasuaji wa moyo ambapo watoto
10 walitibiwa.
Picha na Khamisi Mussa
Wagonjwa
21 wenye matatizo ya moyo wakiwemo watoto na watu wazima wamefanyiwa upasuaji katika
kambi maalum za matibabu ya moyo zilizomalizika jana katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi wa Upasuaji wa moyo Dkt. Angela Muhozya wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambo hizo mbili za upasuaji.
Dkt.
Angela ambaye pia ni daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi alisema kwa muda
wa siku tano katika Taasisi hiyo kulikuwa na kambi mbili za matibabu ambapo wagonjwa 21 walifanyiwa upasuaji.
Alisema
watoto 10 walifanyiwa upasuaji na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na mwenzao
kutoka nchini Ujerumani ambapo watu wazima 11 walifanyiwa upasuaji na wataalamu
wa Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wenzao wa Shirika la Cardiostart
International.
“Wiki hii tumekuwa na kambi za kimatibabu mbili tofauti moja kwa watoto na nyingine ni kwa watu wazima. Katika kambi ya watu wazima tumekuwa na wataalamu kutoka Shirika la Cardiostart International ambalo ni mchanganyiko wa madaktari kutoka nchini Uingereza na Marekani tumewapandikiza wagonjwa mishipa ya damu na kubadilisha valvu kwa wagonjwa ambao valvu zao ziliharibika kabisa,”.
Dkt.Angela alisema upasuaji huo uliofanywa na madaktari hao ni ule mgumu, ambao ungewalazimu wagonjwa hao kusafirishwa ili kutibiwa nje ya nchi.Upasuaji huo umefanyika kwa wagonjwa ambao mioyo yao ilikuwa inafanya kazi chini ya asilimia 25, hivyo walilazimika kubadilishiwa valvu za moyo ambazo zilikuwa zimeharibika sana na hasa kwa watu wazima sana.
Alimshuku Dkt.Benjamin Bierbach kutoka Ujerumani ambaye alikabidhi vifaa maalumu vyenye thamani ya shilingi bilioni 2, ambavyo vimesaidia katika kufanikisha upasuaji kwa watoto waliozaliwa na mshipa mmoja mkubwa unaounganika kutoka katika vyumba viwili vya moyo.
Naye Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka JKCI Godwin Sharau alisema wiki hii wamekuwa na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka nchini Ujerumani Benjamin Bierbach ambapo watoto 10 ambao walikuwa na matatizo ya mishipa ya damu, Valvu na vyumba vya moyo walifanyiwa upasuaji.
“Tumekuwa
na Dkt Benjamin huu ni mwaka wa saba hata wakati wa UVIKO 19 Daktari huyu
aliendelea kuja JKCI na kufanya matibabu kwa watoto wenye shida ya moyo,na
katika kambi hii tumeshirikiana kwa pamoja kufanya upasuaji kwa watoto ambao
wamezaliwa na matatizo ya Valvu, vyumba vya moyo na mishipa ya damu tumewapandikizia
mishipa ya bandia ambayo watakaa nao kwa muda wa miaka kumi na tano na
watabadilishiwa mingine,”.
“Dkt
Benjamini pamoja na kuja kufanya upasuaji wa watoto pia amekuja na mishipa ya
bandia ambayo ndiyo iliyotumika kuwawekea watoto hao,mishipa hii ni ya gharama
sana na hivyo tunapopata nafasi ya kuwa na kambi kama hizi watoto wengi
wanahudumiwa na pia tunaongeza uzoefu mkubwa zaidi wa kuwahudumia watoto,” alisema
Dkt. Sharau.
Comments
Post a Comment