Msomali aishukuru JKCI kwa upasuaji wa mtoto wake
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto Evelyn Furumbe na Afisa Muuguzi Mariam Makapu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimuhudumia mtoto kutoka nchini Somalia ambaye amefanyiwa upasuaji wa kuzibwa tundu la moyo katika Taasisi hiyo ambaye ameruhusiwa kutoka wodini leo tarehe 07/11/2022. Kulia ni bibi wa mtoto huyo Halimo Isse.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto Evelyn Furumbe na Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mariam Makapu wakimuhudumia mtoto kutoka nchini Somalia ambaye alifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na kuzibwa tundu la moyo katika Taasisi hiyo, mtoto huyo ameruhusiwa kutoka wodini leo tarehe 07/11/2022.
Hirs Ally ambaye ni baba mdogo wa mtoto aliyefanyiwa
upasuaji wa moyo kutoka nchini Somalia akimtazama kwa furaha mtoto huyo mara baada ya
kuruhusiwa kutoka wodini katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa
anapatiwa matibabu.
*******************************************************************************************************************************************************************************************************************
Raia wa Somalia ameshukuru kwa huduma ya upasuaji wa kuziba tundu la moyo aliofanyiwa mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Shukrani hizo amezitoa leo jijini Dar es Salaam wakati akiongea
na mwandishi wa habari hizi mara baada ya mtoto huyo kuruhusiwa kutoka wodini
ambako alikuwa anapatiwa matibabu.
Hirs Ally ambaye ni baba mdogo wa mtoto alisema baba wa mtoto
huyo aliyeko nchini Somalia alipata taarifa ya kupatikana kwa huduma ya
upasuaji wa moyo JKCI na hivyo kumtuma mtoto huyo aliyeambatana na bibi yake kuja hapa nchini kwa ajili ya
kupatiwa matibabu.
“Tunashukuru huduma tuliyoipata ni nzuri kuna vifaa vya
kutosha pia madaktari na wauguzi ni marafiki kila unachowauliza wanakujibu na
wanakwambia kila kitu ambacho mtoto anaenda kufanyiwa,”.
“Tuliamua kumleta mtoto wetu JKCI kwani gharama za matibabu ni
ndogo ukilinganisha na nchini Somalia pia kuna wataalamu wenye ujuzi wa hali ya
juu na vifaa viko vya kutosha, ninawasihi wazazi wenye watoto ambao
wanamatatizo ya moyo wawalete hapa kwa ajili ya matibabu,”alisema Hirs.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Evelyn Furumbe alisema walimpokea
mtoto huyo mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili tarehe 10/10/2022 na baada
ya kumfanyia vipimo waligundua moyo wake una tundu.
Dkt. Evelyn alisema tarehe 11/10/2022 mtoto alifanyiwa
upasuaji wa kuziba tundu hilo ambapo hadi sasa anaendelea vizuri na leo hii
ameruhusiwa na atarudi kwa ajili ya kliniki baada ya wiki mbili ili kuangalia
maendeleo yake.
“Mtoto alikuwa na tundu ambalo linakuwa kati ya mshipa wa kupeleka
damu kwenye mwili (Aorta) na wa kupeleka damu kwenye mapafu (Pulmonary) hili
tundu mtoto akizaliwa huwa linafunga lakini la kwake halikufunga na lilikuwa na
ukubwa wa milimita 6. Pia alikuwa na nyama chini ya Valvu ambayo ilikuwa
inasababisha damu kupita kwa kasi katika Aorta na kusababisha mlango wa Aorta kuharibika
na kuanza kuvuja damu hivyo basi tiba yake ilikuwa ni kukata nyama na kuziba tundu,”.
“Watoto wenye shida kama hizi huwa tunawapokea mara kwa mara
na wanafanyiwa upasuaji na kupona na kuendelea na maisha kama watoto wengine,”
alisema Dkt. Evelyn.
Comments
Post a Comment