Kanali Abas: Kateni bima za afya kuwa na uhakika wa matibabu
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas akuzungumza na
wananchi wa Mkoa wa Mtwara waliofika katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini
(SZRH) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo wakati
wa kambi maalum ya siku tatu inayofanywa na Madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa SZRH.
Mkurugenzi wa Tiba wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Tatizo Waane akimsikiliza mwananchi aliyefika katika Hospitali ya Rufaa
Kanda ya Kusini (SZRH) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa
ya moyo wakati wa kambi maalum ya siku tatu inayofanywa na madaktari wa JKCI
kwa kushirikiana na wenzao wa SZRH.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Baraka Ndelwa akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) mwananchi aliyefika katika Hospitali
ya Rufaa Kanda ya Kusini (SZRH) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya
moyo wakati wa kambi maalum ya siku tatu inayoendelea katika Hospitali hiyo.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Robert Mallya akitoa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa ya
moyo kwa wananchi waliofika katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini (SZRH)
kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo wakati wa
kambi maalum ya siku tatu inayoendelea katika Hospitali hiyo.
Afisa Uuguzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini (SZRH)
Anitha Kaondo akimpima Shinikizo la damu mwananchi aliyefika katika Hospitali
hiyo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo wakati wa
kambi maalum ya siku tatu inayofanywa na wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa SZRH.
Na: JKCI
*******************************************************************************************************
Wananchi wa Mkoa wa Mtwara na mikoa ya jirani wametakiwa
kukata bima za afya kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwani matibabu ya
kibingwa hugharimu fedha nyingi ambapo mara nyingi wananchi hao hushindwa
kugharamia matibabu hayo pale wanapoyahitaji.
Akizungumza na wananchi hao leo wakati wa uzinduzi wa kambi
maalum ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayoendelea katika Hospitali ya Rufaa
Kanda ya Kusini (SZRH) Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas alisema
kumekuwa na changamoto kwa wananchi wengi kutokukata bima za afya hivyo
kushindwa kulipia gharama za matibabu haswa matibabu ya kibingwa.
Kanali Abbas alisema ni muhimu kwa wananchi wanaopata huduma katika Hospitali hiyo
kuhakikisha wanakata bima za afya ili
kurahisisha upatikanaji wa huduma kwani matibabu ya kibingwa hugharimu fedha
nyingi na mara nyingi sio rahisi kwa mwananchi wa kawaida kuweza kuwa na fedha
taslim anapopatwa na changamoto za afya.
“Mkoa wa Mtwara umepata bahati ya kupata Hospitali kubwa kwa
ajili ya kanda nzima ya Kusini bahati ambayo inaendelea kwa wataalam mabingwa
wa moyo kutembelea Hospitali hiyo na kutoa huduma za kibingwa za moyo ambazo
kwa asilimia kubwa wananchi wa mkoa huo ingekuwa ngumu kuzifuata Dar es
Salaam,”.
“Tunaishukuru Serikali ya Mhe. Samia Suluhu Hassani kwa
jitihada kubwa inayofanya ya kutatua changamoto mbalimbali za wananchi ikiwepo
eneo la afya kwani hii ni bahati kwa mkoa wetu kupata hospitali kubwa pamoja na
kutuletea wataalam mbalimbali wakiwemo wa magonjwa ya moyo ili huduma za
magonjwa hayo ziweze kusogea hadi kwa wananchi wasiokuwa na uwezo wa kusafiri
kufuata huduma mahali zilipo”, alisema Kanali Abbas.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kupitia mabingwa wa magonjwa ya
moyo wanaenda kutatua changamoto za wananchi sio tu kwa watu wa Mkoa wa Mtwara lakini pia katika
mikoa ya jirani ya Lindi na Ruvuma pamoja na wananchi waliopo nchi za jirani na Tanzania za Msumbiji na Comoro.
Aidha Kanali Abbas aliwataka mabingwa wa magonjwa ya moyo
kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuendelea kuwa walezi wa Hospitali
ya Rufaa Kanda ya Kusini ili hapo baadaye watalaam wa Hospitali hiyo waweze
kuendelea kutoa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo bila ya usimamizi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tiba wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete Dkt. Tatizo Waane alisema JKCI imeanzisha zoezi endelevu la kuwafuata
wananchi mahali walipo na kuwafanyia uchunguzi na matibabu ya magonjwa wa moyo
ili kuhakikisha watu wote wanaohitaji matibabu ya moyo wanafikiwa kwa wakati.
“Sisi kama JKCI Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alituelekeza
kuzilea Hospitali tatu za kanda ikiwemo Hospitali hii ya Rufaa Kanda ya Kusini,
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato na Hospitali ya Rufaa ya Kigoma ili nazo
ziweze kupata uzoefu kama tulionao JKCI na kwa kutimiza hilo hadi sasa
tumeshaifikia Hospitali ya Chato na sasa tupo hapa Kanda ya Kusini”, alisema
Dkt. Waane.
Dkt. Waane alisema kambi hiyo maalum imelenga kutoa elimu ya
namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo, elimu kwa wataalam wa afya ya namna ya
kuwahudumia wagonjwa wa moyo pamoja na kukusanya taarifa kuhusu magonjwa ya
moyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ili kuweza kuisaidia serikali katika
mikakati yake ya huduma za afya ili iweze kujua hali halisi ilivyo kuhusu
magonjwa hayo.
“JKCI itaendelea kutoa huduma za kibingwa za uchunguzi na
matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wote wa Tanzania ambapo kwa kuanzia
imejipanga kutembelea mikoa 15 ikiwemo mkoa wa Lindi, Tanga, Zanzibar,
Kilimanjaro, Katavi, Mbeya na mikoa mingine,” alisema Dkt. Waane.
Naye mwananchi aliyepatiwa huduma katika kambi hiyo George
Liwenga alisema amekuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu pamoja
kisukari kwa muda mrefu hivyo aliposikia ujio wa mabingwa wa moyo akavutiwa
kufika katika kliniki zao ili naye afanyiwe uchunguzi wa moyo kwani magonjwa
aliyonayo yanaweza yakamsababishia kupata magonjwa ya moyo.
“Nimepata huduma za kufanyiwa uchunguzi katika moyo wangu,
nimefurahi sana kuwa miongoni mwa wananchi tuliojitokeza kuchunguza afya zetu
kwani maradhi ya moyo yanampata kila mtu hivyo ni vyema wananchi wakawa na
tabia ya kuchunguza afya zao,”.
“Ninaomba huduma kama hizi ziendelee kutolewa mara kwa mara
hapa mkoani kwetu ili sisi watu wazima tusioweza kusafiri kwa muda mrefu tuweze
kupata huduma hizi karibu na maeneo tunayoishi”, alisema Liwenga.
Comments
Post a Comment