Watoto 22 wafanyiwa upasuaji wa moyo ndani ya siku sita
Wataalam wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Save a Child’s
Heart (SACH) la nchini Israel wakiangalia tundu la moyo wa mtoto kama limeziba
vizuri kwa kutumia mashine ya ECHO wakati wa kambi maalum ya matibabu ya moyo
ya siku sita iliyomalizika hivi karibu jijini Dar es Salaam.
Na: JKCI
*************************************************************************************************************************
Watoto 22 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni
matundu na mishipa ya damu wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalum ya matibabu iliyomalizika hivi
karibuni katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es
Salaam.
Kambi hiyo ya siku sita ilifanywa na wataalam wa magonjwa ya
moyo kwa watoto wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Save a
Child’s Heart (SACH) la nchini Israel.
Katika kambi hiyo mtoto mdogo aliyefanyiwa upasuaji alikuwa
na umri wa mwezi mmoja na wiki mojo huku mkubwa akiwa na umri wa miaka 12, hali
za watoto zinaendelea vizuri na wengine wameruhusiwa kurudi nyumbani.
Akizungumza kuhusu kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya
moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela alisema
mtoto mdogo aliyefanyiwa upasuaji katika kambi hiyo alizaliwa mishipa yake ya
damu ya moyo ikiwa imejigeuza hivyo kuhitaji kufanyiwa upasuaji wa kuirekebisha.
“Mtoto huyu mwenye
umri mdogo mbali na kurekebishiwa mishipa ya damu alihitaji pia kutengenezewa
tundu kubwa kwenye moyo kuleta mchanganyiko mzuri zaidi wa damu ili aweze
kupata unafuu kama sehemu ya kumuandaa kwa ajili ya matibabu makubwa zaidi ya
upasuaji wa moyo,” alisema Dkt. Stella.
Dkt. Stella alisema katika kambi hiyo watoto 13 walizibwa
matundu yaliyokuwa katikati ya mishipa mikubwa miwili ya moyo (Patent Ductus
Arteriosus - PDA) na wengine tisa walikuwa na matundu katikati ya vyumba
mbalimbali vya moyo ambapo matundu hayo yamezibwa.
“Ushirikiano wa JKCI na Shirika la Save a Child’s Heart ni
ushirikiano ambao umesaidia kuwasomesha wataalam wa kada mbalimbali wa magonjwa
ya moyo kwa watoto pamoja na kuhakikisha wanabadilishana uzoefu nasi kuhakikisha
tunaendeleza ujuzi wetu,”.
“Miaka ya mwanzoni wamekuwa wakifanya upasuaji pamoja na sisi
lakini katika siku za hivi karibuni hasa awamu hii wamekuwa ni wasimamizi wa
kuangalia nini tunafanya na kutoa ushauri pale ambapo unahitajika, kwa hakika
haya ni maendeleo makubwa,” alisema Dkt. Stella.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Save a
Child’s Heart Simon Fisher alisema anaamini kila watalam wa shirika hilo
wanapokuja JKCI wataalam wa JKCI wanapata nafasi ya kupanda angalu hatua moja
katika kutoa huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo kwa watoto.
“Tumeshuhudia maendeleo makubwa kutoka kwa wataalam wa hapa
JKCI kwani mara nyingi tulivyokuwa tunakuja tulikua tukidhamiria kufanya
upasuaji kwa watoto wengi kwa kipindi kifupi lakini kipindi hiki tulilenga
kufundisha zaidi kuliko kufanya matibabu kwa watoto wengi,” alisema Simon.
Simon alisema Ushirikiano wa shirika la Save a Childs Heart
unazidi kuendelea sio tu kwa mafunzo na kwa kufika JKCI kwa ajili ya matibabu
pia ni miongoni mwa mashirika machache hapa duniani ambalo limekuwa likichukua
watoto kutoka Tanzania bara na Visiwani na kuwapeleka nchini Israel kwa ajili
ya matibabu mbalimbali hasa ya upasuaji wa moyo.
“Ushirikiano wa shirika letu na Tanzania umekuwepo kwa zaidi
ya miaka 20, kwa sasa hivi tumepunguza kwa asilimia zaidi ya 90 kuwapeleka
watoto Israel kwa ajili ya matibabu kwasababu tayari kituo cha kutoa huduma
hizo kipo hapa Tanzania na wataalam wake wanaendelea siku hadi siku kuwa
mabingwa wabobezi wa magonjwa ya moyo kwa watoto,” alisema Simon.
Naye mama ambaye mtoto wake alifanyiwa upasuaji katika kambi
hiyo Josephina Emmanuel kutoka mkoani Kigoma alisema mtoto wake alikuwa na
matundu mawili kwenye moyo ambapo tatizo hilo liligundulika mtoto akiwa na umri
wa miezi mitatu na kuanza kupatiwa matibabu.
“Nawashukuru sana madaktari ambao wamemfanyia upasuaji
mwanangu maana mwanzoni mtoto alitibiwa kwa dawa watalaam wakasema huenda
matundu hayo yangejifunga lakini kwa bahati mbaya tundu moja tu ndio lilifunga
na lililobaki leo hii wataalamu wamemfanyia upasuaji na kulifunga na nimeambiwa
sasa mtoto kapona kabisa,”.
“Niliambiwa gharama za matibabu ni shilingi milioni nne laki
mbili na elfu sitini lakini kutokana na hali yangu nimepata msamaha wa matibabu
na kulipia shilingi laki moja tu na
kupatiwa matibabu haya kwakweli nawashukuru sana watalaam hawa maana sisi watu
wa hali ya chini sijui tungewezaje kupata hizi huduma kama Taasisi hii
isingekuwepo hapa nchini kwetu,” alisema Josephina.
Watoto hao walifanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua
kupitia tundu dogo linalotobolewa kwenye paja kwa kutumia mtambo wa Cathlab
(Catheterization Laboratory) ambayo ni maabara inayotumia mionzi maalum kwa
ajili ya uchunguzi wa matatizo na tiba za magonjwa ya moyo.
Comments
Post a Comment