“Watakaotoa kauli mbaya kwa wagonjwa kuchukuliwa hatua kali”
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akizungumza na viongozi wa Taasisi hiyo wakati wa kufungua
mafunzo ya siku mbili ya uadilifu kwa viongozi wa JKCI jana katika ukumbi waTaasisi
hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Afisa uchunguzi kutoka Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa
Umma Grace Kwambiana akiwafundisha viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) maadili ya watumishi wa umma wakati wa mafunzo ya uadilifu kwa viongozi
wa Taasisi hiyo yaliyofanyika jana katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Picha na: Khamis Mussa
**************************************************************************************************************
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) watakaobainika
kujihusisha na vitendo vya kutoa kauli mbaya kwa wagonjwa, kuwatoza fedha
kinyume na utaratibu,kanuni, sheria na uadilifu katika utumishi wa umma
watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
Onyo hilo limetolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya uadilifu kwa viongozi
wa umma yanayotolewa na Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa
Umma.
Dkt. Kisenge alisema JKCI imeandaa mafunzo hayo kwa
kuzingatia maelekezo ya Serikali kwa mujibu wa waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi
wa mwaka 2017 ukilenga kutekeleza mkakati wa Taifa wa kudhibiti uadilifu na
mapambano dhidi ya rushwa awamu ya tatu ili watumishi wa umma washiriki
kikamilifu na kwa vitendo kupambana na rushwa.
“Lengo la Taasisi yetu ni kuwa na watumishi wenye maadili
mema na mfano wa kuigwa, Mtumishi mwadilifu atatumikia watanzania muda wote
bila upendeleo, kujali hali zao wala kipato chao kwa kuzingatia sheria, kanuni,
taratibu na miongozo mbalimbali ya utumishi wa umma,”.
“Ninaamini mafunzo haya yatatuwezesha kujifunza namna ya
kuishi kwa uadilifu katika kuhakikisha shughuli za serikali zinafikia malengo
yaliyowekwa huku watumishi wakizingatia misingi ya uadilifu na maadili,” alisema
Dkt. Kisenge.
“Ni matumaini yangu
mafunzo haya yatawajengea uwezo wa kusimamia vyema maeneo yenu na kuwaongezea
ari watumishi mnaowaongoza ili waweze kuwa na uadilifu mahala pa kazi na
kuzingatia miiko ya kiutumishi na mwenendo mwema wa utumishi wa umma,”alisema
Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma George Mwendamseke alisema lengo
kuu la mafunzo hayo ni kuhakikisha viongozi wanatekeleza majukumu yao katika
hali ya uadilifu, kujenga imani kwa wananchi, serikali na kuhakikisha kuwa
hawajiingizi kwenye matatizo ya mgongano wa maslahi.
“Mafunzo tunayotoa yanahusu masuala ya kimaadili hususani
eneo la maadili ya viongozi wa umma, kufahamu miongozo makatazo na nini cha
kuzingatia katika kutekeleza majukumu ya kazi za kuwatumikia wananchi,”.
“Mafunzo haya pia yatahusisha mgongano wa maslahi kuhakikisha
kwamba viongozi hawa wanatambua na kufahamu ni maeneo gani yanaweza kuwaingiza
katika mgongano wa maslahi na kuweza kujikwamua nayo,” alisema Mwendamseke.
Mwendamseke alitoa wito kwa taasisi zote za umma kuhakikisha
mafunzo kama hayo yanaandaliwa kwa viongozi wake kama ambavyo agizo la waraka
wa mkuu wa utumishi wa umma ambao unataka elimu ya maadili itolewe kwa
watumishi wote.
“Tunazikumbusha taasisi kuzingatia maelekezo ya viongozi
kuhakikisha kwamba zinaandaa mafunzo ya kimaadili kwasababu maadili ni kinga ya
maovu na husaidia katika kutoa huduma bora, kuboresha taasisi na kutekeleza
mipango mikakati,” alisema Mwendamseke.
Naye Mkuu wa kitengo cha rasilimali watu wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Abdulrahman Muya alisema Taasisi hiyo imeanza kutoa mafunzo
hayo kwa viongozi na baadaye yatafanyika kwa watumishi wote.
“Tunategemea baada ya mafunzo haya tutaimarisha uadilifu kwa
watumishi, kutokuwa na mazingira ya rushwa na kuendelea kutoa huduma bora kwa
wagonjwa wetu kwani utekelezaji wa mpango mkakati wa kudhibiti uadilifu na
mapambano dhidi ya rushwa mahali pa kazi ni sehemu ya utekelezaji wa Taasisi
yetu,” alisema Muya.
Comments
Post a Comment