Wananchi wa Geita tafuteni tiba sahihi kwa wataalam wa afya – Mhe. Martha Mkupasi
Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Martha Mkupasi, Mwenyekiti wa
Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Pro. William Mahalu,
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) Dkt. Brian
Mawalla wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa kliniki ya uchunguzi na matibabu
ya magonjwa ya moyo wakati wa ufunguzi wa kambi maalum ya matibabu ya moyo
inayofanywa na madaktari wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa CZRH leo katika
Hospitali hiyo iliyopo Wilaya ya Chato
**************************************************************************************
Wananchi wa Mkoa wa Geita na mikoa ya jirani wametakiwa
kufuata huduma za matibabu hospitali pindi wanapojisikia kuumwa ili waweze
kupata tiba halisi na kuondoa fikra potofu za kufuata tiba hisia zinazotolewa
na watu ambao sio wataalam wa afya.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Martha
Mkupasi wakati wa uzinduzi wa kambi maalum ya matibabu ya moyo ya siku tano
inayofanywa na wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) inayoendelea
katika Hospitali hiyo.
Mhe. Martha alisema kuwa lengo la serikali ni kusogeza huduma
karibu zaidi kwa wananchi pamoja na kuwapunguzia gharama za kufuata huduma za
matibabu mbali ya makazi yao ndio maana leo hii Hospitali ya Rufaa ya Kanda
Chato inajengewa uwezo ili nayo iwe sehemu ya kusogeza huduma na kupunguza
gharama kwa wananchi wa Mkoa wa Geita.
“Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato imewekezwa vifaa vyote
vya matibabu ya moyo vyenye gharama kubwa hivyo nawaomba wananchi wote
mtakaposikia dalili za kuumwa mfike katika Hospitali hii ili muweze kupata tiba
halisi muache kwenda kwenye tiba hisia”, alisema Mhe. Martha
Mhe. Martha alisema kuwa ujenzi wa CZRH ulianza awamu ya tano
ambapo Mhe. Rais wa awamu ya sita mama Samia Suluhu Hassan aliahidi kuhakikisha
miradi yote iliyoanza awamu ya tano inakamilika na inafanya kazi kwa asilimia
100 jambo ambalo linathibitishwa leo katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Kanda
Chato.
“Nawaomba wataalam wa
afya wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato kuweka jitihada ya pekee kupokea yale
wanayofundishwa na wataalam wa afya kutoka JKCI ili baada ya kambi hii muweze
kuwahudumia na kuwapatia matibabu wananchi wa Chato, mikoa ya jirani pamoja na
nchi zilizopo jirani na Chato”,
“Nawashukuru watumishi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo ambao hawakuona umbali wa
Wilaya yetu ilipo bali wao walidhamiria kuja kutoa huduma za matibabu ya moyo
na kuleta faraja kwetu sisi wananchi wa kanda ya ziwa”, alisema Mhe. Martha
Akizungumzia kambi hiyo ya uchunguzi na matibabu ya moyo Mwenyekiti
wa bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Prof. William Mahalu
alisema kuwa wataalam wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato wamekua na
utayari wa kupokea ujuzi unaotolewa na watalaam wa JKCI kwa kuwa mstari wa
mbele kufanya kazi kwa pamoja na wataalam hao jambo ambalo linatoa motisha ya
kuendelea kuwajengea uwezo.
Prof. Mahalu alisema kuwa jitihada zinazofanywa na wataalam
wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato kama zitaendelezwa kwa kujengewa
uwezo mara kwa mara na kupelekwa masomoni kwa ajili ya kuwa wataalam wabobezi wa
magonjwa ya moyo kutaifanya hospitali hiyo kuwa hospitali bingwa ya magonjwa
moyo nchini na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa ajili
ya matibabu
“Nilivoteuliwa na Rais wa awamu ya tano kuwa mwenyekiti wa
bodi ya wadhamini ya JKCI nilipewa agizo la kupunguza idadi ya wananchi wanakwenda
nje ya nchi kutibiwa moyo ambapo hadi sasa tumebakiza asilimia nne tu ya
wagonjwa wa moyo wanaokwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya moyo,
asilimia hii nne tunaweza kuifuta kabisa kama wataalam wa CZRH mtajitoa
kuifanya hospitali hii kuwa hospitali bingwa ya magonjwa ya moyo”, alisema
Prof. Mahalu
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kuwa JKCI imejipanga kuwafuata
wananchi walipo ambapo kwa kuanza JKCI itaanzisha vituo viwili vya kuchunguza
magonjwa ya moyo kwa lengo la kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo
kwa wananchi.
“Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato ni moja ya kitua cha
uchunguzi na matibabu ya moyo ambapo leo hii tumezindua kliniki ya matibabu ya
moyo lakini pia Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mtwara nayo itakua kituo kingine
cha kuhudumia wagonjwa wa moyo”
“Tumekuwa tukifanya kambi maalum za matiabu (outreach) katika
mkoa wa Dar es Salaam na kuwafanya wananchi wa mikoa mingine kusafiri kufuata
huduma hizo, lakini sasa tumeona nimuhimu kuwafuata wananchi walipo ili pia
tuweze kutoa mafuzo kwa wataalam wa afya tutakaowakuta sehemu tunazopeleka
huduma hizi”
Aidha Dkt. Kisenge alisema kuwa Kituo cha uchunguzi na
matibabu ya moyo cha Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato kitakapoimarika
kitakua kikitoa huduma za upasuaji mkubwa wa moyo na kuwekeza mtambo wa Cathlab
ambao utatumika kutoa huduma za upasuaji wa moyo wa tundu dogo.
“Tunakwenda kutengeneza mpango mkakati wa kuhakikisha katika
miaka mitano huduma za upasuaji wa moyo na matibabu kwa kutumia mtambo wa
Cathlab zinafanyika hapa Chato ikiwa ni njia ya kuwasaidia wananchi wa kanda ya
ziwa na nchi za jirani”, alisema Dkt. Kisenge
Naye mwananchi wa Chato aliyepatiwa huduma wakati wa kambi
hiyo Omary Maulid alisema kuwa hakuwahi kujua kama anamatatizo ya shinikizo la
damu na kisukari kwani mara zote alizokua akienda hospitali na kumweleza daktari
kuwa macho hayaoni vizuri hakupimwa shinikizo la damu wala sukari hivyo kujikuta
anatibiwa vitu vingine.
“Nimefurahi kupata fursa hii ya kuja kuchunguza afya ya moyo
wangu kwasababu nimekua nikiumwa siku nyingi, macho yangu hayaoni vizuri kumbe
nina shinikizo la juu la damu ambalo sikuwahi kupimwa leo hii ndio
nimejitambua”,
“Elimu ya afya hasa hii ya magonjwa yasiyoambukiza inatakiwa
kutolewa zaidi sio tu kwa wananchi lakini pia na kwa wataalam wa afya waliopo
katika vituo vya afya katika jamii zetu ili wananchi tuweze kupata tiba sahihi
pale tunapoumwa”, alisema Omary
Comments
Post a Comment