JKCI yaanzisha kliniki ya maumivu ya kifua
***************************************************************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeanzisha kliniki ya matibabu ya maumivu ya kifua kwa wagonjwa wenye maumivu ya vichomi kifuani na kifua kubana ili waweze kufanyiwa uchunguzi wa haraka kwani maumivu hayo huambatana na magonjwa mbalimbali ya moyo ikiwemo shambulio la moyo.
Akizungumzia leo kuhusu kliniki hiyo inayofanyika JKCI
iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Tiba ya Moyo wa Taasisi hiyo
Dkt. Tatizo Waane alisema kuwepo kwa huduma hiyo kutawafanya wagonjwa kupata
huduma ya matibabu mapema.
Dkt. Waane ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
alisema maumivu ya kifua yamekuwepo katika jamii lakini maumivu hayo mara
nyingi yamekuwa hayatambuliki kutokana na jamii inavyofikiria kwani mtu
anapoumwa kifua hudhani ana matatizo ya nimonia au matatizo mengineyo bila
kuhisi kuwa maumivu hayo yanaweza kuwa ni dalili za magonjwa ya moyo.
“Ninawaomba wananchi wote kutokudharau pale wanapopata
maumivu ya kifua bali wapende afya zao na kuwa na utaratibu wa kupima afya pale
wanapojisikia kuwa na maumivu ya kifua,”.
“Maumivu ya kifua ni
moja ya dalili kubwa za magonjwa ya moyo hususani shambulio la moyo, kwetu sisi
ni muhimu kuwatambua wagonjwa wenye shambulio la moyo ili waweze kupata
matibabu sahihi kutoka kwa wataalam wetu wabobezi wa magonjwa ya moyo,” alisema
Dkt. Waane.
Aidha Dkt. Waane alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa taasisi
hiyo huduma mbalimbali zikiwemo huduma za upasuaji wa moyo kwa watu wazima na
watoto, huduma za matibabu ya ndani kwa wagonjwa waliolazwa, huduma za matibabu
ya upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab, huduma za kliniki kwa
wagonjwa wa nje zimekuWa zikitolewa kwa watu wote wanaofika katika Taasisi
hiyo.
“Huduma zetu za kliniki zinafanyika siku za Jumatatu hadi Jumamosi
na huanza saa 12 asubuhi hadi saa 2 usiku kwa kuona wagonjwa kati ya mia tatu
hadi mia nne kwa siku na kwa siku ya Jumamosi kliniki inaanza saa 2 asubuhi
hadi saa 8 mchana,”, alisema Dkt. Waane.
Mgonjwa anayepatiwa matibabu katika Taasisi hiyo Grace
Clement alisema yeye ni miongoni mwa wagonjwa ambao wamekua wakisumbuliwa na
maumivu ya kifua kwa muda mrefu bila kuhisi kama maumivu hayo yanaendana na
magonjwa ya moyo.
Grace alisema mwanzoni alihisi kifua kinamuuma kutokana na
shughuli alizokuwa akifanya kila siku hivyo na pale aliposikia maumivu aliacha
kufanya shughuli zake na kuamua kupumzika lakini maumivu hayakupungua na hivyo
kuamua kufika katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.
“Nawashauri watanzania wenzangu wanapojisikia maumivu ya
kifua kufika kwa wataalam wa afya ili waweze kuchunguza maumivu hayo
yanasababishwa na nini maana mimi nilifika hospitali nikachunguzwa na kufuata
ushauri wa daktari wa kutumia dawa, kufanya mazoezi ili nipunguze uzito na leo
naona maendeleo yangu kuwa mazuri,” alisema Grace.
Naye mgonjwa anayehudhuria kliniki za matibabu ya moyo JKCI Salum
Jabey alisema alikuwa na maumivu ya kifua baada ya kufanyiwa uchunguzi iligundulika
kuwa baadhi ya mishipa yake ya damu imeziba.
“Nilikuwa nachoka sana nikitembea au nikiwa nafanya shughuli
zangu za kila siku, kifua kinauma na mapigo ya moyo yanaenda kasi nikaenda
hospotali ya Apolo walivonichunguza wakanipa rufaa ya kuja hapa JKCI ambapo
waligundua baadhi ya mishipa ya damu imeziba hivyo kunipatia matibabu,”.
“Kwa sasa hivi dalili nilizokuwanazo zimepungua kwa asilimia
kubwa, nawashukuru wataalam wa afya wa hapa JKCI kwa kuendelea kutupatia matibabu,
ushauri wangu kwa jamii wanapojisikia kuumwa wasiende kwa sangoma waende hospitali
ambazo zipo kwa ajili yetu tuzitumie,”alisema
Salum.
Comments
Post a Comment