JKCI yaokoa milioni 180 matibabu ya wagonjwa 12 nje ya nchi
Wataalam mabingwa wa moyo na matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri wakimfanyia upasuaji wa tundu dogo mgonjwa ambaye mfumo wake wa umeme wa moyo una hitilafu wakati wa kambi maalum ya siku mbili ya matibabu hayo iliyomalizkika jana jijini Dar es Salaam. Jumla ya wagonjwa 12 wenye matatizo ya hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo wametibiwa katika kambi hiyo.
***********************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeokoa zaidi ya shilingi milioni 180 ambazo zingetumiwa na Serikali iwapo ingewapeleka wagonjwa 12 wenye hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo (Atrial Fibrillation) kutibiwa nje ya nchi.
Wagonjwa hao waliokuwa na tatizo la uzalishaji wa umeme wa moyo kwa muda mrefu uliosababisha chemba mbili za moyo kufanya kazi bila mawasiliano (Atrial Fibrillation) wametibiwa katika kambi maalum ya matibabu iliyofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Hospitali ya Shifa na chuo Kikuu cha Ain Shams kilichopo Cairo nchini Misri.
Akizungumza kuhusu kambi hiyo ya siku mbili iliyomalizika jana jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo wa JKCI Yona Gandye alisema gharama ya mgonjwa mmoja kutibiwa hapa nchini ni milioni 18 na nje ya nchi ni zaidi ya milioni 30 hivyo basi kuna unaafuu mkubwa wa kutibiwa hapa nchini ukilinganisha na nje ya nchi.
Mtaalamu huyo wa mfumo wa umeme wa moyo alisema hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo inaweza
kusababisha damu kuganda na kupelekea mgonjwa kupata kiharusi (stroke) ama kifo
cha ghafla kutokana na kiharusi.
Dkt. Gandye alisema wagonjwa wenye matatizo ya moyo ambayo ni
moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure), matatizo ya shinikizo la damu na mshtuko
wa moyo (Heart Attack) mfumo wao wa umeme wa moyo mara nyingi unaweza
kuvurugika.
“Mfumo wa umeme wa moyo ukivurugika utendaji wa kazi wa moyo hupunguza
uwezo wa kufanya kazi na kuhitaji kufanyiwa marekebisho ambayo yatauwezesha
moyo kuongeza ufanisi wake na kusukuma damu kwa kiwango kinachostahili,”
alisema Dkt. Gandye.
Dkt. Gandye alisema kupitia wataalam kutoka nchini Misri
wataalam wa JKCI wamepata uwezo wa kufanya matibabu ya hitilafu ya mfumo wa
umeme wa moyo kwa kujitegemea, kujenga uhusiano katika kutoa huduma hizo,
pamoja na kupanua wigo na uwezo wa ndani wa kuwahudumia watanzania.
“Hapo awali huduma hii ilikuwa ikitolewa nje ya Tanzania,
baada ya Serikali yetu kuanzisha taasisi hii na kufunga mtambo maalum unaoweza
kusoma na kutambua matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo watanzania wameweza
kupata huduma hizi hapa nchini,”.
“Moyo una uwezo wa kutengeneza mapigo yake ambayo huanza kama
msisimko na kusambaa ndani ya misuli ya moyo hivyo kuufanya moyo kuweza
kutanuka na kusinyaa”, alisema Dkt. Gandye.
Dkt. Gandye alisema magonjwa ya moyo kuna wakati yanaweza kuwepo
ndani ya mwili bila kuonesha dalili yoyote hivyo kumfanya mgonjwa kutokutafuta
huduma za afya.
“Wananchi
tunawahamasisha wawe wanafanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kutambua
matatizo mapema kwa kufanya hivyo kutarahisisha huduma kuwa nyepesi kufanyika,
kupona haraka, na kupunguza madhara makubwa yanayotokana na uchelewaji wa
kupata huduma kwa wakati,” alisema Dkt. Gandye.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mfumo
wa umeme wa moyo kutoka Hospitali ya Shifa na chuo Kikuu cha Ain Shams kilichopo
Cairo nchini Misri Prof. Mervat Aboulmaaty alisema hii ni mara yao ya sita
kufanya kambi hiyo na madaktari wa JKCI ambapo mafanikio makubwa yameonekana
katika kutoa huduma hizo kwa wagonjwa.
Prof. Mervat alisema wamekuwa wakifanya matibabu ya kibingwa
kwa wagonjwa wenye hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo na kuwaachia utaalam huo
wataalam wa JKCI hivyo kuongeza ubingwa katika kutoa matibabu hayo hapa nchini.
“Kupitia utaalam tunaobadilishana hapa JKCI naamini Taasisi
hii inaenda kuwa taasisi bora zaidi ya kutoa huduma za matibabu ya moyo Afrika
Mashariki kwani sisi ni waafrika hivyo tunapaswa kusaidiana pale
tunapohitajiana,” alisema Prof. Mervat.
Naye mgonjwa aliyefanyiwa matibabu katika kambi hiyo aliwashukuru
wataalam hao kwa kuokoa maisha yake na kumuondolea maumivu aliyokuwa akiyapata
kutokana na tatizo la mfumo wa umeme wa moyo.
“Kabla ya kupatiwa matibabu nilikuwa nikipitia maumivu makali
ya kifua, kizunguzungu, moyo kwenda kasi, kutetemeka pamoja na kupata ganzi
maeneo ya miguuni lakini baada ya matibabu sijapata tena hizo dalili nimeamini
ugonjwa wa moyo unatibika,”.
“Namshukuru Mungu na madaktari wa Taasisi hii sasa hivi
naendelea vizuri, naomba utalaam huu walioupata uendelee kuwa faida kwa watu
wengine wenye uhitaji wa matibabu kama niliyopatiwa mimi,” alisema mgonjwa huyo.
Comments
Post a Comment