Wananchi 50,000 kupata huduma za kibingwa za moyo kwa kufuatwa mahali walipo


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa habari za Afya Aveline Kitomari kutoka gazeti la HabariLeo na James Kandoya wa gazeti la The Guardian kuhusu matokeo ya upimaji wa magonjwa ya moyo uliofanywa na Taasisi hiyo mkoani Arusha wakati wa mkutano wa nne wa kisayansi wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza uliomalizika jana jijini Mwanza.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya Prof. Paschal Ruggajo akimkabidhi Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Janeth Mmari tuzo ya utafiti bora alioufanya kuhusu teknolojia na mbinu za ubunifu za kuzuia na kutibu magonjwa yasiyoambukiza wakati wa mkutano wa nne wa kisayansi wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza uliomalizika jana katika  Hoteli ya Malaika jijini Mwanza. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akijibu maswali kuhusu utafiti uliofanywa na Taasisi hiyo kuhusu magonjwa ya moyo na uelewa wa sababu hatarishi za magonjwa hayo mkoani Arusha katika mkutano wa nne wa kisayansi wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza uliomalizika jana jijini Mwanza. Kulia ni Dkt. Elice Mnunga. 

Baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari za mkoa wa Mwanza wakitazama TV iliyokuwa inaonesha  huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa mkutano wa nne wa kisayansi wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza uliomalizika jana katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza.


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Taasisi hiyo waliohudhuria mkutano wa nne wa kisayansi wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza uliomalizika jana jijini Mwanza. Katika mkutano huo Taasisi hiyo iliwasilisha tafiti sita walizozifanya ambapo tafiti moja ya teknolojia na mbinu za ubunifu za kuzuia na kutibu magonjwa yasiyoambukiza ilishinda.

*****************************************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imejipanga kuwafikia wananchi 50,000 kwa kuwafuata mahali walipo na  kutoa huduma za kipingwa za upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo.

Hayo yamesemwa jana jijini Mwanza na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taasisi hiyo ilivyojipanga kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza katika mkutano wa nne wa kisayansi wa magonjwa hayo uliomalizika jana jijini humo.

Dkt. Kisenge alisema kwa mwaka huu wa fedha wa 2022/23 wamejipanga kuwafikia  wananchi 50,000 katika mikoa 15 ikiwemo Zanzibar ambapo hadi sasa wameshaifikia mikoa miwili ya Arusha na Geita na mwishoni mwa mwezi huu wataifikia mikoa ya Lindi na Mtwara.

Alisema lengo la kuwafuata wananchi na kutoa huduma hizo ni kuhakikisha watu wenye matatizo ya moyo wanatambulika mapema na kuweza kupata matibabu kwa wakati tofauti na ilivyo sasa ambapo wananchi wenyewe wanaifuata huduma hiyo jijini Dar es Salaam na wengine wanaanza kupata matibabu ya kibingwa wakiwa wamechelewa.

“Upimaji huu tunaufanya kwa kushirikiana na wenzetu wa Hospitali za mikoa husika, licha ya kutoa huduma za upimaji  tunatoa pia mafunzo kwa wataalamu wa afya ya jinsi ya kuwatambua wagonjwa wa moyo pamoja na kufanya vipimo kwani Serikali ya awamu ya sita imenunua mashine za kisasa za vipimo vya moyo na mashine hizi ziko katika Hospitali za mikoa,”.

“Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo ni magonjwa yanayoweza kuepukika kama wananchi watafuata ushauri wa kitaalamu ikiwemo kufanya mazoezi, kula vyakula bora, kutotumia bidhaa za tumbaku na kuacha unywaji wa pombe uliopitiliza. Katika upimaji tunaoufanya tunakuwa na wataalamu wa lishe ambao wanatoa elimu ya lishe kwa wananchi,”alisema Dkt. Kisenge.

Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema katika upimaji wanaoufanya asilimia kubwa ya watu wanakutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu huku wengine wakiwa hawajijui kabisa kuwa na ugonjwa huo.

“Wagonjwa wengine wanaokutwa na shinikizo la juu la damu wanakutwa wameshapatwa na madhara ya ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kutanuka kwa misuli ya moyo pia tunawapata watoto wenye matatizo ya  moyo ambayo ni matundu, mishipa ya damu ya moyo  na valvu hivyo basi ninawaomba wananchi mjenge tabia ya kupima afya zenu japo mara moja kwa mwaka,”alisisitiza Dkt. Kisenge.

Aidha Taasisi hiyo pia ilitoa  elimu kwa umma ya jinsi ya kuyatambua magonjwa ya moyo pamoja na huduma za matibabu ya moyo wanazozitoa kwa washiriki wa mkutano huo.

Baadhi ya wanafunzi kutoka kutoka shule za sekondari za mkoa wa Mwanza  walijifunza dalili za ugonjwa wa moyo, jinsi ya kujizuia usipate ugonjwa huo pamoja na tiba ya ugonjwa wa moyo.

David Patrick mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya Sekondari Pamba alisema alijifunza kuhusu betri la moyo (Pacemaker) jinsi linavyowasaidia wagonjwa ambao mapigo yao ya moyo yako chini na baada ya wagonjwa hao kuwekewa betri hilo mioyo yao inafanya kazi vizuri.

“Mimi ninaishi na wazazi wangu ambao ni watu wazima haya niliyojifunza leo  nitawafundishwa ili wafuate mtindo bora wa maisha kwa kula vyakula bora, kufanya mazoezi, kutokunywa pombe kupitiliza na kuacha kuvuta sigara ili wasipate matatizo ya moyo wakiwa wazee,”alisema David.

Nimejifunza dalili za magonjwa ya moyo pia jinsi ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi  unavyoweza kusababisha mishipa ya damu ya moyo kuziba na madhara yake ni mtu kufa ghafla, nitawafundisha wenzangu nyumbani na shuleni ili wasifanye mambo yanayoweza kuharibu mioyo yao”,.

“Sikuwa najua  hata watoto wanashida ya moyo, sasa hivi  nikiona mtoto hakui vizuri, akicheza kidogo anachoka na kutoka jasho jingi na kushindwa kupumua vizuri nitamwambia mzazi wake ampeleke hospitali ili wakampime moyo wake inawezekana ukawa na shida,” alisema Musa George mwanafunzi wa kidato cha tatu  shule ya sekondari  Buhongwa.

 

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024