Asilimia 60 ya wagonjwa wa presha hawajitambui
Kaimu Mkuu wa Hospitali ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Dar Group Dkt. Tulizo Shemu akizungumza na waandishi wa habari leo
jijini Dar es Salaam kuhusu upimaji utakaofanyika tarehe 16 na 17 Mei 2024
katika Hospitali hiyo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya shinikizo la damu
duniani inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 17 mwezi Mei.
Na: JKCI
*************************************************************************************************
Zaidi ya asilimia 60 ya watu wenye shinikizo la juu la damu
hapa nchini hawajitambui kama wana tatizo hilo kwani tafiti zinaonesha kati ya
watu kumi watu watatu ndio wanatambua kuwa na tatizo hilo.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Hospitali ya Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dar Group Dkt. Tulizo Shemu leo jijini Dar es Salaam
wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu siku ya shinikizo la damu
duniani inayoadhimishwa kila ifikapo Mei 17.
Dkt. Shemu alisema Ugonjwa wa shinikizo la juu la damu
unatokana na madhara ya kiwango cha presha kuwa kikubwa katika mwili wa
binadamu hivyo kusababisha shinikizo la damu kuwa juu.
“Ugonjwa wa shinikizo la juu la damu hauna dalili maalumu
lakini zipo dalili chache zinazoweza kujitokeza endapo mtu atapata ugonjwa huu
zikiwemo dalili ya kuumwa kichwa mara kwa mara, macho kutoona vizuri, moyo
kwenda haraka, pamoja na kubanwa na kifua”, alisema Dkt. Shemu
Dkt. Shemu alisema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete inaenda
kuadhimisha siku hiyo kwa kufanya upimaji bila gharama tarehe 16 na 17 May 2024
katika Hospitali ya JKCI Dar Group lengo likiwa kuleta uelewa na ufahamu katika
jamii kuhusu tatizo la shinikizo la juu la damu.
“Kauli mbiu ya mwaka huu inatutaka kuzifahamu tarakimu za
shinikizo la damu kwa kupima presha kwa usahihi na endapo utakutwa na ugonjwa
huu hakikisha unapata matibabu na kudhibiti ugonjwa ili usiweze kukuletea
madhara mengine yatokanayo na tatizo la presha”, alisema Dkt. Shemu
Dkt. Shemu alisema kwa takwimu zilizofanyika kwa wagonjwa
wanaotibiwa JKCI mwaka 2023 kati ya wagonjwa 125,927 waliopatiwa matibabu
asilimia 42 walikuwa na shinikizo la juu la damu.
“Madhara ya ugojwa huu ni pamoja na kupata kiharusi,
kusababisha figo kushindwa kufanya kazi, kupata magonjwa ya mshtuko wa moyo,
tatizo la moyo kushindwa kufanya kazi, kuvimba miguu, kupata ganzi sehemu za
mwili, kupumua kwa shida, kukosa nguvu pamoja na shida za uzazi”, alisema Dkt.
Shemu
Naye daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Sulende Kubhoja alisema tatizo la shinikizo la
juu la damu huwapata pia watoto na tatizo hilo hutokana na matatizo mengine
ambayo mtoto anakuwa nayo.
Dkt. Kubhoja alisema tunapoenda kuadhimisha siku ya shinikizo
la damu tusiwasahau watoto kuwashirikisha upande wa kufanyiwa uchunguzi na hata
eneo la kupata elimu kuhusu ugonjwa huo ili pale wanapoweza kujikinga
wajikinge.
“Mara nyingi ukimkuta mtoto ana shinikizo la juu au la chini
la damu hutokea kama mtoto ana matatizo ya figo, au matatizo mengine katika viungo
vinavyowasiliana mwilini”, alisema Dkt. Kubhoja
Dkt. Kubhoja alisema kuna watoto wamekuwa wakipata tatizo la
shinikizo la juu la damu kutokana na magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa pamoja na
matatizo ya mishipa ya damu kuwa na hitilafu.
“Sisi tunapopata mtoto ana tatizo la shinikizo la juu la damu
tunamfanyia uchunguzi kwa kuangalia kila kiungo cha mwili wa mtoto ili tuweze
kutambau sehemu yenye matatizo na kuweza kuitibu” alisema Dkt. Kubhoja
Comments
Post a Comment