Wakazi wa Dar es Salaam wapima moyo bure
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya
JKCI Dar Group Patrice Justine akimpima shinikizo la damu mwananchi
aliyejitokeza kupima wakati wa kambi maalumu ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan
Outreach Services inayofanyika katika Hospitali hiyo katika kuadhimisha siku ya
shinikizo la damu duniani inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 17 Mei.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya JKCI Dar Group Masanja James akizungumza na mwananchi aliyefika katika kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanyika katika Hospitali hiyo katika kuadhimisha siku ya shinikizo la damu duniani inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 17 Mei.
Mwakilishi kutoka kamupuni ya dawa za binadamu ya Sun Pharma Oresta Mwila akimhudumia mwananchi aliyepatiwa matibabu katika kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanyika katika Hospitali ya JKCI Dar Group katika kuadhimisha siku ya shinikizo la damu duniani inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 17 Mei.
Baadhi ya wananchi wakiwa katika foleni ya kupatiwa matibabu
wakati wa kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services
inayofanyika katika Hospitali ya JKCI Dar Group katika kuadhimisha siku ya
shinikizo la damu duniani inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 17 Mei.
Na: JKCI
************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika kuadhimisha siku
ya shinikizo la damu duniani inafanya upimaji wa magonjwa ya shinikizo la damu,
sukari na moyo kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani.
Upimaji huo ujulikanao kwa jina la Mhe. Samia Suluhu Hassan
Outreach Services umeanza kufanyika leo katika Hosptitali ya JKCI Dar Group na
utamalizika kesho tarehe 17 Mei 2024 kwa kutoa huduma bila gharama kwa wananchi
wote watakaojitokeza kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari daktari bingwa wa magonjwa
ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya JKCI Dar Group Baraka
Ndelwa alisema upimaji huo unafanyika ili kuwapa nafasi wananchi kuufahamu
vizuri ugonjwa wa shinikizo la juu la damu na namna ambavyo wanaweza kujikinga
na ugonjwa huo.
Dkt. Baraka alisema upimaji huo unatolewa bila gharama ili
kuwafikia wananchi wenye kipato cha chini kufanyiwa uchunguzi, kupatiwa
matibabu na wale watakaohitaji dawa kupatiwa bila gharama.
“Tunazishukuru kampuni za dawa za binadamu zilizoshirikiana
nasi katika kuadhimisha siku ya shinikizo la damu duniani kwa kuwaletea
wagonjwa wetu dawa bila gharama”, alisema Dkt. Baraka
Kwa upande wake mwananchi aliyepatiwa huduma katika kambi
hiyo Paulina Lwegeta alisema hakujua kama ana tatizo la shinikizo la juu la
damu lakini kwasababu ndugu yake ana tatizo hilo na amelazwa katika hospitali
JKCI Dar Group akaamua naye atumie nafasi aliyopata kuchunguza afya yake.
“Kupitia matokeo niliyoyapata hapa naona watu wengi tutakuwa
tunaumwa ugonjwa wa shinikizo la juu la damu lakini hatujui, natoa wito kwa
wananchi wenzangu kuwa na tabia ya kufanya vipimo mara kwa mara”, alisema
Paulina
Paulina alisema amekuwa akiumwa kichwa kwa muda mrefu lakini
hakujua kama ana tatizo la shinikizo la juu la damu hadi leo alipofanyiwa
uchunguzi na kugundulika kuwa na tatizo hilo ambapo amepatiwa dawa.
Omary Seif mkazi wa Temeke alisema amekuwa akisumbuliwa na
tatizo la shinikizo la juu la damu kwa muda mrefu na kupatiwa matibabu katika
hospitali tofauti bila ya mafanikio.
“Nimekuwa nikitibiwa tatizo la shinikizo la damu tangu mwaka
2023 katika hospitali tofauti lakini chaajabu hakuna siku presha yangu imeshuka
na kukaa sawa, siku zote ipo juu hadi imeniletea matatizo ya macho kwani sasa
hivi sioni vizuri”, alisema Omary
Omary alisema baada yakuona matangazo ya upimaji unaofanyika
JKCI Dar Group alichukua hatua yakufika katika upimaji huo ambapo amepata
huduma na kushauriwa vizuri kuhusu dawa alizokuwa anatumia hapo awali.
Naye meneja kutoka kampuni ya dawa za binadamu ya Hetero Lab
Ivan Edmund alisema kampuni mbalimbali za dawa za binadamu kwapamoja zimeungana
kushirikiana na JKCI kuwapatia wananchi watakaokuta na matatizo ya shinikizo la
damu, sukari na magonjwa ya moyo dawa bila gharama.
Ivan alisema kulingana na hali za wananchi wengi kampuni yake
na nyingine zilizojitokeza hazikuona shida kuadhimisha siku ya shinikizo la
damu duniani na wananchi watakaojitokeza kupima katika kambi maalumu ya Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan inayofanyika JKCI Dar Group.
“Tunaishauri jamii iache matumizi ya dawa bila ya kumuona
daktari ni vizuri kabla ya kutumia dawa ukamuona daktari akakufanyia uchunguzi
na kukuandikia dawa sahihi kwani dawa ni tiba na wakati mwingine dawa inaweza
kuwa sumu isipotumika vizuri”, alisema Ivan
Comments
Post a Comment