77 Wapewa rufaa kufika JKCI kwaajili ya matibabu zaidi
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Odilia Njau akimpa elimu kuhusu shinikizo la damu mwananchi aliyetembelea banda la taasisi hiyo wakati wa kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services iliyokuwa ikifanyika katika maonesho ya Kimataifa ya usalama na afya mahali pa kazi na kumalizika jana jijini Arusha. Jumla ya watu 672 wamepatiwa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.
Wananchi wa mkoa wa Arusha wakiendelea kupata huduma katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services iliyokuwa ikifanyika katika maonesho ya Kimataifa ya usalama na afya mahali pa kazi na kumalizika jana jijini Arusha. Jumla ya watu 672 wamepatiwa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.
*************************************************************************************************************
Watu 77 wamepewa rufaa kufika katika Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kwaajili ya kufanyiwa vipimo vikubwa vya kuchunguza moyo na
wengine kufanyiwa upasuaji wa moyo.
Rufaa hizo zimetolewa wakati wa kambi maalumu ya siku 8
ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services iliyokuwa
ikifanyika katika maonesho ya kimataifa ya usalama na afya mahali pa kazi na
kumalizika jana katika viwanja vya General tyre vilivyopo jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari daktari bingwa wa magonjwa
ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dickson Minja alisema watu
wengi waliowahudumia na kuwakuta na matatizo ya shinikizo la damu, sukari na
magonjwa ya moyo walikuwa hawajijui na hawakuwa wakitumia dawa.
“Kupitia vipimo tulivyovifanya wakati wa maonesho haya, watu
147 tumewakutwa na shinikizo la damu ambapo kati yao watu 85 hawakuwa wanajua
kama wana matatizo ya shinikizo la damu hivyo hawakuwa wanatumia dawa”,
“Watu 23 tuliwakuta na magonjwa ya moyo ambayo ni matatizo ya
valvu za moyo (Rheumatic heart disease), changamoto za mfumo wa upelekaji wa
damu kwenye moyo (Ischemic heart disease), moyo kutanuka, na shinikizo la juu
la damu”, alisema Dkt. Dickson
Dkt. Dickson alisema katika maonesho hayo wameweza kuwafanyia
vipimo vya magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na sukari kwenye damu wananchi
672 ambapo kati yao watu 170 sawa na asilimia 25 wamekutwa na magonjwa
mbalimbali ya moyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa Arusha
wameishukuru taasisi ya JKCI kwa kuwafikishia huduma karibu, kuwapa nafasi ya
kupima afya na kupata elimu ya kujikinga na magonjwa ya moyo.
John Eliud alisema haikuwa rahisi kwake kuchukua uamuzi wa
kupima moyo kutokana na mtindo wa maisha yake kwani amekuwa akitumia vilevi
mbalimbali ambavyo mara nyingi amekuwa akiambiwa si salama kwa afya.
“Nawashukuru sana JKCI nimepima sukari, presha na moyo na
vyote nimekuta viko sawa, daktari kanishauri kupunguza na baadaye kuacha kabisa
kutumia vilevi ninavyotumia ili kuulinda moyo wangu”, alisema John
Naye Denis Nyakutanwa aliipongeza Taasisi ya JKCI kwa kazi
kubwa inayofanya ya kutoa huduma za uchunguzi wa afya kwa jamii na kuiomba
kuendelea kuwafikia wananchi kwani wengi wao hawana uwezo wa kuifikia kwaajili
ya kufanya uchunguzi wa afya.
“Nawapongeza sana kwa kutufikia, lakini nimesikia gharama za
matibabu ya moyo ni kubwa. Naiomba Serikali iangalie namna ya kuwezesha
upatikanaji wa vifaa vya matibabu ya moyo kirahisi ili kupunguza gharama za
matibabu ya moyo”, alisema Denis.
Comments
Post a Comment