Serikali kufungua tawi la JKCI – Chato


 Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akiingia bungeni leo jijini Dodoma kwaajili ya kuwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2024/25.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu na Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel wakiwa wameshika  hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 kabla haijasoma leo bungeni jijini Dodoma.

**************************************************************************************************************************************************************************************

Serikali imepanga kufungua tawi la Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Kanda ya Ziwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (JKCI- Chato) iliyopo mkoani Geita.

Hayo yamesemwa leo bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2024/25.

Katika kutekeleza hilo Wizara ya Afya moja ya vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 ni  kuwekeza katika vifaa tiba vitakavyowezesha utoaji wa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi ikiwemo ununuzi wa mitambo ya kupima na kutibu moyo bila kufungua kifua (Cathlab) miwili kwaajili ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Chato.

Waziri Ummy alisema huduma za ubingwa na ubingwa bobezi  zinapatikana kwa gharama nafuu nchini na hivyo kuvutia wagonjwa kutoka nje ya nchi (Tiba Utalii) ambapo wagonjwa kutoka nje ya nchi wameongezeka kutoka 5,705 mwaka 2022 hadi 7,843 mwaka 2024.

“Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika Hospitali ngazi ya Taifa, Kanda, Maalum na hospitali za Mikoa, Aidha, kutokana na uwekezaji wa kimkakati uliofanywa na Serikali wa kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi”.

“Huduma mpya 16 za ubingwa bobezi zilianzishwa nchini zikiwemo za upasuaji mdogo wa moyo kwa kubadilisha Valvu ya mshipa mkubwa wa damu bila kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implamentation - TAVI), kufungua mishipa ya miguuni iliyoziba (Endovascular Procedure ) na  kuweka stent kwenye mishipa mikubwa ya damu iliyopasuka”, alisema Mhe. Ummy.

Katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi nchini kwa kutumia wataalam wa ndani, kiasi cha Shilingi 5,000,000,000 kimetolewa kwaajili ya kugharamia matibabu kwa wagonjwa wasio na uwezo wa matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi jumla ya wagonjwa 237. Huduma hizo zimetolewa katika hospitali za Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ilihudumia wagonjwa 100 ambapo kati yao wagonjwa 50 walipatiwa huduma za Valvular Replacement surgery na wagonjwa 50 walipatiwa huduma za Implantable cardiac devices.

Waziri Mhe. Ummy alisema hospitali ya Taifa ya Muhimbili wagonjwa 91 walipatiwa huduma ambapo watoto 16 wamenufaika kwa kuwekewa vifaa vya kusikia (Cochlear implants) upandikizaji wa uloto (Bone marrow transplant) wagonjwa 9, upandikizaji wa figo (Kidney transplant) wagonjwa 29 na vipandikizi vya Moyo wagonjwa 37.

Hospitali ya Benjamin Mkapa imehudumia wagonjwa 46 kati yao wagonjwa 10 walipandikizwa uloto (bone marrow transplant), wagonjwa wanne wamepandikizwa figo (kidney transplant), mgonjwa mmoja aliwekewa valve kwenye moyo na mgonjwa mmoja alifanyiwa valvular replacement. Pia, maandalizi yanaendelea kwaajili ya kupandikiza wagonjwa wengine 10 wa uloto, kupandikiza figo wagonjwa 10 na Valvular Replacement surgery wagonjwa 10.


 

Comments

Popular posts from this blog

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024

Maabara ya JKCI yapata ithibati ya kimataifa (ISO 15189:2012)