JKCI SACCOS mkombozi wa maisha ya wafanyakazi


Mwenyekiti wa Chama cha kuweka akiba na mikopo (Saccos) cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tulizo Shemu akiwashukuru wanachama wa Saccos hiyo kwa kumuamini na kumchangua tena kuwa mwenyekiti wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa kuchagua viongozi wapya na kuangalia maendeleo ya chama hicho uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wanachama wa Chama cha kuweka akiba na mikopo (Saccos) cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa kuchagua viongozi wapya na kuangalia maendeleo ya chama hicho uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.





Wanachama wa chama cha kuweka akiba na mikopo (Saccos) cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa kuchagua viongozi wapya na kuangalia maendeleo ya chama hicho uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Na: JKCI

****************************************************************************************************

Kiasi cha mkopo wa shilingi bilioni 1.6 zimetolewa na chama cha akiba na mikopo (SACCOS) cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa wanachama wa SACCOS hiyo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa kuchangua viongozi wapya pamoja na kuangalia maendeleo ya chama hicho uliofanyika jana katika ukumbi wa Taasisi hiyo.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni mlezi wa Saccos hiyo aliwapongeza wanachama wa SACCOS hiyo kwa kuchukua maamuzi ya kujiunga na chama hicho kinachowawezesha kuwekeza na kumudu mahitaji yao kiuchumi.

“Uongozi wa taasisi utasaidia kuweka mazingira mazuri kwa wafanyakazi wake ili wote waweze kujiunga na SACCOS hii kwani inawasaidia kupata mikopo ya haraka kwa riba nafuu na kupunguza changamoto za wafanyakazi”, 

 “Nia yangu ni kuhakikisha kuwa SACCOS ya JKCI inakuwa moja ya Saccos kubwa nchini, nawashauri muanze kufikiria kwenye uwekezaji ambao utasaidia kukuza Saccos na kuwafaidisha wanachama wake”, alisema Dkt. Kisenge

Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama cha kuweka na kukopa (Saccos) cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tulizo Shemu alisema Saccos hiyo ilianzishwa mwaka 2019 ikiwa na wanachama 24 ambapo hadi kufikia Machi mwaka huu Saccos hiyo ina wanachama 288.

Dkt Shemu alisema lengo la Saccos hiyo ni kufikisha wanachama 500 ili kwapamoja wafanyakazi wa JKCI waweze kufanya maendeleo yapamoja yatakayowaunganisha na kuwajengea uaminifu baina yao.

“Uongozi wa JKCI ndio ulikuwa chachu ya kuanzisha Saccos hii kwa kutoa mtaji wakwanza wa shilingi milioni tano na kuifanya Saccos yetu kuwa suluhisho la mitaji ya wafanyakazi wa JKCI”, alisema Dkt. Shemu

Dkt. Shemu alisema Saccos hiyo imekuwa ikitoa mikopo kwa wananchawa wake ndani ya masaa 12 endapo vigezo vyote vya muombaji wa mikopo vitakuwa vimekamilika.

Dkt. Shemu alisema akiba za wanachama wa Saccos ya JKCI zinaendelea kukuwa kutoka shilingi milioni moja mwaka 2020 hadi kufikia shilingi milioni 134 kwa mwaka 2024.

“Kwa kipindi cha miaka minne hadi kufikia Machi mwaka huu jumla ya shilingi milioni 220 ilikuwa imekusanywa kama riba ya mikopo yote iliyotolewa na Saccos sawa na ongezeko la wastani wa shilingi milioni 44 kwa kila mwaka ukilinganisha na shilingi 326,000 zilizokusanywa mwaka 2020”, alisema Dkt. Shemu.

Naye mwanachama wa Saccos hiyo Magdalena Chikawe alisema kupitia Saccos ameweza kukopa mikopo ambayo imekuwa ikimnufaisha katika maisha yake na kuweza kuleta tija katika familia yake.

“Mimi kama mwanachama hai nimeweza kuchukua mikopo mara kwa mara mikopo ambayo nimeitumia kujenga nyumba yangu, kulipia ada za shule za watoto wangu pamoja na kuwekeza katika biashara yangu”, alisema Magdalena.

Magdalena alisema manufaa anayoyapata anaamini wanachama wenzake pia wanayapata kwani kumekuwa na uwazi na taarifa za mara kwa mara zinazoonesha mapato na matumizi ya Saccos hiyo.


Comments

Popular posts from this blog

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024

Maabara ya JKCI yapata ithibati ya kimataifa (ISO 15189:2012)