Maabara ya JKCI yapata ithibati ya kimataifa (ISO 15189:2012)
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizunguma na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu maabara ya Taasisi hiyo kupata ithibati ya viwango vya ubora wa kimataifa (ISO 15189:2012) katika kutoa huduma za vipimo vya magonjwa ya moyo pamoja na magonjwa mengine.Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa JKCI Anna Nkinda.
Kaimu Mkuu wa Maabara ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Emmanuel Mgao akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu maabara hiyo kukidhi vigezo vilivyowekwa kimataifa katika kutoa huduma na kupata ithibati yenye namba ISO 15189:2012.
Wafanyakazi wa Maabara ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akizunguma na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu maabara hiyo kupata ithibati ya viwango vya ubora wa kimataifa (ISO 15189:2012) katika kutoa huduma za vipimo vya magonjwa ya moyo pamoja na magonjwa mengine.
****************************************************************************************************************************************************************************************************
Maabara ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepata ithibati ya viwango vya ubora wa kimataifa katika kutoa huduma za vipimo vya magonjwa ya moyo pamoja na magonjwa mengine.
Shirika la Kimataifa la Viwango (ISO) ndilo lililotoa
ithibati hiyo yenye namba ISO 15189:2012 kwa maabara ya JKCI yenye mashine za
kisasa inayotoa vipimo zaidi ya 86 vya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali yakiwemo
ya moyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
alisema kutolewa kwa ithibati hiyo kunamaanisha
majibu ya vipimo vyote vinavyotolewa na maabara hiyo vinaaminika kimataifa na
vinaweza kutumika popote pale duniani.
Dkt.Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
alisema upatikanaji wa ithibati hiyo unaonesha usalama kwa wagonjwa wanaopatiwa
huduma za matibabu ya moyo na hasa kwa wagonjwa watu wazima na watoto waofanyiwa
upasuaji mkubwa wa moyo.
“Tunaishukuru Wizara ya Afya kwa ushirikano wanaotupatia
katika kufanikisha matibabu ya moyo nchini na hasa upande wa maabara”.
“Tumekuwa tukipokea vipimo vya maabara kutoka hospitali na
maabara zingine ambazo hazifanyi vipimo vikubwa vya uchunguzi wa magonjwa ya
moyo na magonjwa mengine, ninawaomba wale ambao hawawezi kufanya vipimo hivyo
wavilete JKCI tutavifanya kwa uharaka na gharama naafuu”.
“Jengo letu la utawala na vipimo limekamilika na limeanza
kutumika, siku chache zijazo tutafungua maabara kubwa ya kisasa katika jengo
hilo hivyo basi wagonjwa wetu pamoja na wadau wetu wanaofanya vipimo kwetu
watarajie kupata huduma bora zaidi”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Taasisi hiyo kuwa na
maabara ya kisasa yenye wataalamu wa kutosha ambao wanatoa huduma za kiwango
cha kimataifa katika kufanya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali.
Kwa
upande wake Kaimu Mkuu wa maabara hiyo Emmanuel Mgao alisema hadi kupata
ithibati hiyo maabara ilifanyiwa ukaguzi na bodi ya ukaguzi wa maabara ya
Kusini mwa Jangwa la Sahara (Southern African Development Community
Accreditation Services - SADCAS) na kukidhi vigezo vilivyowekwa kimataifa kwa maabara katika kutoa huduma.
“Maabara hii ilianza kufanya kazi mwaka 2019, baada ya miaka sita imeweza kukidhi viwango vya kimataifa, tutahakikisha ubora wa huduma tunazozitoa unawasaidia wagonjwa wetu kupata matibabu sahihi na kwa wakati kutokana na matatizo waliyonayo”, alisema Mgao.
Comments
Post a Comment