Watu 602 wafikiwa na huduma ya tiba mkoba ya moyo mkoani Rukwa
Watu 602 wakiwemo watu wazima 577 na watoto 25 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu iliyomalizika hivi karibuni mkoani Rukwa.
Huduma hiyo ya matibabu ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services ilitolewa kwa siku tano na
wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao
wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo Daktari bingwa
wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete
alisema watu 480 walifanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi
(Echocardiography – ECHO) na watu 451 walifanyiwa kipimo cha kuangalia mfumo wa
umeme wa moyo (Electrocardiography – ECG).
“Tumetoa rufaa 34 watu wazima wakiwa 25 na watoto 9 kufika
katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya uchunguzi na matibabu
zaidi na wengine kwaajili ya kufanyiwa upasuaji wa moyo”, alisema Dkt. Salehe.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto
wa JKCI Theophil Ludovic alisema watoto 25 wamefanyiwa uchunguzi katika kambi
hiyo ambapo kati yao watoto 10 wamekutwa na magonjwa ya moyo.
Dkt. Theophil alisema idadi ya watoto waliopelekwa na wazazi
au walezi wao katika hospitali hiyo kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi ni sawa na
asilimia nne ya watu wote waliofanyiwa uchunguzi katika kambi hiyo.
“Watoto tuliwakuta na matatizo ya moyo ambayo ni matundu
kwenye moyo na matatizo ya mishipa ya damu kutokuwa sawa tumewaanzishia
matibabu ambapo watoto tisa tumewapa furaa kufika JKCI kwaajili ya matibabu
zaidi”, alisema Dkt. Theophil.
Naye Afisa lishe wa JKCI Husna Faraji alisema watu waliofika
katika kambi hiyo walipata nafasi ya kufundisha umuhimu wa kula vyakula bora
ambavyo vitawasaidia kujikinga na
magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.
Husna alisema takwimu zinaonyesha mkoa wa Rukwa unatatizo la
utapiamlo huku chanzo kikiwa ni pamoja na ukosefu wa lishe unaosababishwa na
watu kutozingatia mlo kamili.
“Wataalamu wa lishe tumekuwa tukishiriki katika kambi za
matibabu ya kibingwa ya moyo ili tuweze kutoa elimu ya lishe bora kwa wananchi ambayo
itawasaidia kujikinga na magonjwa
yasiyoambukiza”, alisema Husna.
Wananchi waliopata nafasi ya kupima magonjwa ya moyo
waliishukuru Serikali kwa kuwapeleka wataalamu wa moyo katika mkoa huo ambao
wamewapa elimu ya jinsi gani ya kuepukana na magonjwa hayo pamoja na wale wenye
shida ya moyo wajue jinsi gani watapata matibabu.
“Tangu nizaliwe sijawahi kupima moyo, leo hii nimefika hapa
nimepima moyo na kukutwa moyo wangu uko safi hauna shida. Nimeelekezwa jinsi ya
kuutunza moyo wangu, elimu niliyoipata nitaenda kuwapa na wenzangu niliowaacha
nyumbani”, alisema Peter Mkosamali mkazi wa Laela.
“Mtaalamu wa lishe ametufundisha namna ya kuandaa chakula bora kwaajili ya familia zetu, sisi huku ni wakulima tuna chakula cha kutosha ninaamini elimu hii niliyoipata inanisaidia kuandaa mlo kamili kwaajili ya watoto wangu ili waepukane na ugonjwa wa utapiamlo ”, alisema Lenada Simwanza mkazi wa Mpui.
Comments
Post a Comment