Wapelekeni watoto kupata matibabu ya kibingwa
Wananchi wametakiwa kuwapeleka watoto kupata matibabu ya
kibingwa pale zinapotokea kambi mbalimbali za matibabu ya moyo ili nao waweze
kupata matibabu hayo.
Rai hiyo imetolewa jana na kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Asha Izina alipotembelea huduma
ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach
Services inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Sumbawanga.
Asha ambaye pia ni mratibu wa huduma za afya ya uzazi na
mtoto mkoani Rukwa alisema mwitikio wa kupata huduma za kibingwa za matibabu ya
moyo umekuwa mkubwa kwa wananchi wa Sumbawanga lakini idadi kubwa ya watu
waliojitokeza ni watu wazima na kuwasahau watoto.
“Tukigundua matatizo ya moyo kwa watoto mapema inakuwa rahisi
kuwapa huduma kwa wakati tofauti na wakicheleweshwa kwani wapo baadhi yao
wakivuka umri fulani kama hawakutibiwa inakuwa ngumu kuwatibu”, alisema Asha
Aidha Asha amewataka wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya
afya kuwekeza katika afya ili wanapohitaji huduma za matibabu ya kibingwa
waweze kuzipata kwa urahisi.
“Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu huduma hii ya kibingwa kufanyika katika
mikoa mbalimbali nchini kuwafikia wananchi na kuongeza ujuzi kwa wataalamu wa
afya”, alisema Asha
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete alisema hadi kufikia jana jumla
ya watu 544 wanawake wakiwa 380 sawa na asilimia 90 na wanaume 164 sawa na
asilimia 10 walikuwa wamepatiwa huduma katika kambi hiyo.
Dkt. Salehe alisema takwimu zinaonyesha hata katika miji
midogo inayokuwa maradhi ya moyo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi kwani hadi
kufikia jana watu 40 walikuwa wamepatiwa rufaa kufika JKCI kwaajili ya
uchunguzi zaidi.
“Watu 90 tumewakuta na maradhi mbalimbali ya moyo ikiwemo
shinikizo la juu la damu, sukari, uzito mkubwa, kutanuka kwa moyo, matatizo ya
umeme wa moyo, mishipa ya damu kuziba, moyo kushindwa kufanya kazi na matatizo
ya valvu za moyo”, alisema Dkt. Salehe.
Dkt. Salehe alisema kupitia kambi hiyo wataacha utaalamu kwa
madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga hivyo kuwaomba kutumia
utalamu huo kuwachunguza na kuwapatia matibabu mapema wagonjwa watakaokuwa na
matatizo ya moyo.
Naye Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Sumbawanga
Dkt. Ismail Macha alisema hospitali hiyo imekuwa na upungufu wa baadhi ya
madaktari bingwa hivyo kushirikiana na Hospitali nyingine kufikisha huduma
katika jamii.
“Tumeweka kambi ya wiki moja na madaktari bingwa wa magonjwa
ya moyo kuwafikia wananchi wetu ambao wamekuwa wakihitaji huduma hii kwa muda
mrefu”, alisema Dkt. Macha
Dkt. Macha aliwashukuru wataalamu wa JKCI kwa kufika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Sumbawanga kwaajili yakutoa huduma kwa wananchi
pamoja na kuwajegea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali hiyo.
Comments
Post a Comment