Safari ya Uhai: Ushirikiano wa JKCI na NMB waokoa maisha ya watoto
Mtoto aliyelazwa katika wodi ya watoto wenye magonjwa ya moyo
katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ester Ezekiel akimkabidhi ua Mtendaji Mkuu wa benki ya NMB Ruth Zaipuna
alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kabla ya hafla fupi ya kuipongeza
benki hiyo kwa mchango wanaoutoa katika matibabu ya moyo kwa watoto leo jijini
Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi zawadi Mtendaji Mkuu wa benki ya NMB Ruth
Zaipuna wakati wa hafla fupi ya kuipongeza benki hiyo kwa mchango wanaoutoa
katika matibabu ya moyo kwa watoto leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge, na Mtendaji Mkuu wa benki ya NMB Ruth Zaipuna wakiwa katika
picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi JKCI baada ya kumalizika kwa hafla
fupi ya kuipongeza benki hiyo kwa mchango wanaoutoa katika matibabu ya moyo kwa
watoto leo jijini Dar es Salaam.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kushirikiana na Benki
ya NMB kuwafuata wanachini mahali walipo kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya
moyo.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa hafla fupi ya kuipongeza
benki hiyo kwa mchango wanaoutoka katika matibabu ya moyo kwa watoto
wanaotibiwa JKCI.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo alisema NMB imedhamiria
kufikisha elimu ya magonjwa ya moyo kupitia mikutano ya elimu ya fedha
wanayofanya katika jamiii mbalimbali nchini.
"NMB inawajali wananchi, tunawashukuru sana kwa kuwa
sehemu ya JKCI kuhakikisha jamii inayohitaji matibabu ya moyo inayapata kwa
wakati", alisema Dkt. Kisenge.
Naye Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna alisema baada
ya kuona uhitaji uliopo katika huduma za matibabu ya moyo benki hiyo iliona ni
vyema kushiriki katika kuokoa maisha ya watoto na kurudisha furaha kwa wazazi
wanaopitia changamoto za kuuguza.
“Kutokana na ukubwa wa matatizo haya ya moyo na jamii kubwa
kushindwa kugharamia matibabu, wakati wa hafla ya chakula cha jioni
iliyofanyika mwaka jana tuliahidi kuchangia shilingi bilioni 1 kwa kipindi cha
miaka minne lakini leo tumetimiza mwaka mmoja tu na tumeshatoa nusu ya fedha
tuliyoahidi”, alisema Ruth.
Ruth alisema NMB itaendelea kushirikiana na JKCI kwa karibu
kuwasaidia watoto wanaohitaji upasuaji wa moyo kwani Taasisi hiyo ni tegemeo
kwa watanzania na watu kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Shirika lisilo la Kiserikali la Heart Team Africa Foundation (HTAF) ambalo liliratibu chakula cha jioni cha kuchangisha fedha za matibabu ya moyo kwa watoto Dkt. Naizihijwa Majani alisema kwa kipindi cha mwaka mmoja NMB imeweza kuchangia shilingi milioni 500 katika matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.
Dkt. Naizihijwa alisema kupitia
HTAF jumla ya watoto 185 wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo watoto 125 wametibiwa
kupitia fedha zilizotolewa na NMB.
“NMB wamekuwa kinara katika kuchangia matibabu ya watoto,
kupitia hafla ya chakula cha jioni iliyofanyika mwaka 2024 waliahidi shilingi
billion 1 kwaajili ya matibabu ya watoto 250 ambapo hadi Leo wameshatoa fedha
za matibabu ya watoto 125 na wote wameshapatiwa matibabu", alisema Dkt.
Naizihijwa
Akitoa neno la shukrani mzazi ambaye mtoto wake ametibiwa na
fedha zilizotolewa na NMB Veronica Temba aliishukuru JKCI na NMB kuwasaidia
kupata huduma za matibabu ya moyo kwani gharama za matibabu hayo kwake zilikuwa
kubwa hivyo familia yake isingeweza kuzimudu.
“Mwanangu amefanyiwa upasuaji, namshukuru Mungu anaendelea
vizuri kwani gharama za matibabu zilikuwa kubwa hivyo sikuweza kuzimudu lakini
kupitia NMB mwanangu ameweza kutibiwa”, alisema Veronica.
Veronica aliiomba NMB kuendelea kuwasaidia watoto wengine
wanaohitaji matibabu ya moyo kwani watoto wengi wanatoka katika familia
zisizokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu hayo.
Comments
Post a Comment