Wanamichezo 450 Wapimwa Afya ya Moyo Katika Mashindano ya Chipukizi Cup Arusha



Wataalamu wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group wakiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa PE academy ya nchini Zimbabwe wanaoshiriki katika mashindano ya 16 ya Chipukizi Cup yanayofanyika katika viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT) vilivyopo jijini Arusha.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi mchezaji aliyeshiriki mashindano ya 16 ya Chipukiz Cup  yaliyomalizika hivi karibuni katika viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT) vilivyopo jijini Arusha.


Mtalaamu ya vipimo vya moyo  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nelson Kolukwi akimpima kipimo cha kuangalia jinsi mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi mchezaji aliyeshiriki mashindano ya16 ya Chipukizi Cup yaliyomalizika hivi karibuni katika viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT) vilivyopo jijini Arusha.

Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group, Mkurugenzi wa Future Stars Alfred Itaeli, Kocha wa timu za vijana kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Haruna Adolph na kamati ya mashindano mkoa wa Arusha wakiwa katika  picha ya pamoja wakati wa mashindano ya 16 ya Chipukizi Cup yaliyomalizika hivi karibuni katika viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT) vilivyopo jijini Arusha.

*********************************************************************************************************************************************************************************************

Wanamichezo 450 kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika walioshiriki mashindano ya 16 ya Chipukizi Cup yaliyofanyika jijini Arusha wamefanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo, hatua inayolenga kuimarisha usalama na ustawi wa wanamichezo chipukizi.

Zoezi hilo lilifanyika hivi karibuni katika viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT), ambapo wataalamu wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group waliwahudumia wanamichezo hao kwa kufanya vipimo mbalimbali vya moyo.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha zoezi hilo Daktari bingwa wa bagonjwa ya moyo kwa watoto wa JKCI  Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda alisema matokeo ya awali yalionyesha hali nzuri ya afya ya moyo kwa wanamichezo wengi, hali iliyowawezesha kuendelea na mazoezi pamoja na kushiriki mashindano bila kikwazo.

Alisema wanamichezo hao walifanyiwa vipimo muhimu ikiwemo kipimo cha kuchunguza mfumo wa umeme wa moyo (ECG) pamoja na kipimo cha kutathmini muundo na utendaji wa moyo (ECHO), vipimo vinavyosaidia kugundua mapema changamoto za kiafya.

“Vipimo vya awali vilionesha kuwa wanamichezo wengi wako salama kiafya, hivyo tuliwaruhusu kuendelea na michezo. Hata hivyo, wachache tulibaini kuwa na changamoto zilizohitaji uchunguzi wa kina zaidi,” alisema Dkt. Eva.

Aliongeza kuwa baadhi ya wanamichezo waliripoti dalili kama maumivu ya kifua na kizunguzungu wakati wa mazoezi hali iliyowalazimu kufanyiwa vipimo zaidi na kushauriwa kufika JKCI kwa uchunguzi wa kina ikiwemo kipimo cha Stress ECG.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Future Stars Academy, Alfred Itaeli aliipongeza JKCI kwa mchango wake mkubwa katika kulinda afya za wanamichezo, akisema huduma hiyo imewasaidia vijana kutambua mapema hali zao za kiafya na kuzuia madhara makubwa ya baadaye.

“Hii ni fursa muhimu kwa vijana kutambua afya zao mapema. Kuingiza huduma za Sports Medicine kuanzia ngazi za chini ni hatua kubwa katika maendeleo ya michezo nchini,” alisema Itaeli.

Wanamichezo walioshiriki mashindano hayo nao wameeleza kuridhishwa na huduma ya uchunguzi wa moyo, wakisema imewaongezea uelewa kuhusu umuhimu wa afya katika taaluma ya michezo.

Mchezaji wa Dream Catchers Academy kutoka Zimbabwe, Beloved Rusakaniko alisema kupima afya ya moyo kumempa uhakika wa kuendelea na michezo kwa kujiamini zaidi.

“Nimefurahi sana kupima moyo wangu na kupata majibu kuwa uko salama. Kwa wanamichezo, afya ya moyo ni msingi wa mafanikio,” alisema Rusakaniko.

Naye mchezaji wa Arusha Youth Development Organization Academy, Aisha Ramadhan, alisema afya ndiyo mtaji mkubwa kwa mchezaji yeyote.

“Ni mara yangu ya kwanza kupima moyo na nimejifunza kuwa bila afya huwezi kufikia malengo yako kama mchezaji,” alisema Aisha.

Mashindano ya 16 ya Chipukizi Cup yalifanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 15 hadi 21 Desemba 2025 katika viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT) jijini Arusha.

Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi

Msumbiji kushirikiana na JKCI katika tiba ya moyo