Wagonjwa watano wenye mishipa ya damu iliyoziba kwa asilimia 75 kufanyiwa upasuaji wa moyo
Wataalamu wa upasuaji
wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
wakishirikiana na mwenzao kutoka Hospitali ya Jaslok iliyopo Mumbai nchini
India Upendra Bhalerao kumfanyia mgonjwa upasuaji wa kupandikiza mshipa ya damu
wa moyo bila kusimamisha moyo (off – Pump CABG) wakati wa kambi maalumu ya siku
tano inayofanyika katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Picha na Hamis Mussa
******************************************************************************************************
Wagonjwa watano wenye
mishipa ya damu iliyoziba kwa asilimia zaidi ya 75 kufanyiwa upasuaji wa
kupandikiza mishipa ya damu ya moyo bila kusimamisha moyo (off – Pump CABG).
Upasuaji huo unafanyika
katika kambi maalumu ya siku tano iliyoanza jana na kufanywa na wataalamu wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka
Hospitali ya Jaslok iliyopo Mumbai nchini India.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema kambi hiyo ni maalumu
kwa wagonjwa ambao mishipa yao ya moyo imeziba hivyo kusababisha ufanyaji kazi
wa mioyo yao kuwa chini ya asilimia 35.
“Wagonjwa tunaowafanyia
upasuaji katika kambi hii mara nyingi utuchukua ugumu kidogo kuwafanyia
upasuaji kutokana na ufanyaji kazi wa mioyo yao, hivyo ili waweze kuwa na
matokeo mazuri mara nyingi wenzetu wanafanya upasuaji huu bila ya kuusimamisha
moyo kama ambavyo tunaenda kufanya katika kambi hii”, alisema Dkt. Angela
Dkt. Angela alisema kupitia
kambi hiyo wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) watajengewa uwezo
ambao utasaidia kutoa huduma kwa ufanisi zaidi kwa wagonjwa ambao mioyo yao
imechoka kutokana na kuziba kwa mishipa ya damu kwa asilimia zaidi ya 75.
“Kambi hii itakuwa
endelevu mpaka pale wataalamu wetu watakapoweza kutoa huduma hii bila ya
kuusimamisha moyo kwani wagonjwa wanaohitaji huduma hii ni wengi lakini
kutokana na hali zao tumekuwa tukiwaweka kwenye matibabu ya dawa kwa muda mrefu
kusaidia kuboresha ufanyaji kazi wa mioyo yao”, alisema Dkt. Angela
Kwa upande wake Daktari
bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka Hospitali ya Jaslok
iliyopo Mumbai nchini India Upendra Bhalerao alisema ameona aungane na
wataalamu wa JKCI kuwasaidia wagonjwa ambao kutokana na matatizo ya mishipa ya
damu kuziba kwa asilimia zaidi ya 75 wanashindwa kujishughulisha na wakati
mwingine hupoteza maisha.
“Wagonjwa
tutakaowafanyia upasuaji kupitia kambi hii wataweza kufanya shughuli ndogondogo
ambazo hapo awali walikuwa hawezi kuzifanya”, alisema Dkt. Bhalerao
Dkt. Bhalerao alisema
kupitia kambi hiyo wataalamu watatoa huduma sambamba na kupata mafunzo
yatakayosaidia kupunguza idadi ya vifo vinavyotokana na matatizo ya mishipa ya
damu ya moyo kuziba.
“Tutaendelea
kushirikiana na Taasisi hii na kuweka kambi za matibabu ya mishipa ya damu mara
kwa mara ili ujuzi huu uweze kuwafikia wataalamu wa JKCI na hapo baadaye waweze
kufanya upasuaji wa namna hii bila ya kuusimamisha moyo”, alisema Dkt. Bhalerao
Naye Mkurugenzi wa Taasisi
ya Health & Wellness Companion Ltd (HWC) iliyofanikisha ujio wa wataalamu
hao Dkt. Priyank Punatar alisema ujio wa wataalamu hao unaakisi dhamira ya
pamoja ya kuwezesha huduma bingwa za kiwango cha kimataifa kuwafikia wataalamu
wote.
Dkt. Punatar alisema
kupitia ushirikiano huo wamelenga kufikisha huduma za juu za upasuaji wa moyo
kupatikana kwa urahisi, kwa gharama nafuu, na kwa karibu bila kulazimika
kusafiri nje ya nchi.
“HWC tunaamini huduma bora
za afya ni haki ya kila mtu na si fursa kwa wachache, kambi hii ni hatua muhimu
katika kuimarisha uwezo wa huduma za afya nchini huku tukihakikisha wagonjwa
wetu wanapata huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa”, alisema Dkt. Punatar
Comments
Post a Comment