Dkt. Pedro: Mwafrika wa kwanza kushinda tuzo ya kimataifa ya Moyo




Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo akionesha moja ya tafiti aliyoiwasilisha  katika mkutano wa American Heart Association (AHA) uliofanyika hivi karibuni  New Orleans jimbo la Louisiana nchini  Marekani.

**************************************************************************************************************

Mtanzania na Mwafrika wa kwanza kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Palangyo ameweka historia duniani baada ya kutunukiwa tuzo ya kimataifa ya Dr. Jay Brown International Best Abstract Award.

Mbali na tuzo hiyo  Dkt. Pedro ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo wa JKCI pia ametunukiwa tuzo ya Paul Dudley White International Scholar Award  ambayo haijawahi kutolewa kwa Mtanzania tangu ianzishwe.

Tuzo hizo zilitolewa katika Mkutano wa American Heart Association (AHA) uliofanyika hivi karibuni  mjini New Orleans, Jimbo la Louisiana nchini Marekani.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii Dkt. Pedro alisema kutambuliwa kwake kimataifa kumetokana na utafiti wa miaka 10 uliofanywa na taassi hiyo kuhusu magonjwa ya moyo yanayoathiri uzazi, yanayojulikana kitaalamu kama Peripartum Cardiomyopathy (PPCM).

“Nimekuwa Mtanzania na Mwafrika wa kwanza na pekee kupata tuzo hizi mbili za heshima, baada ya utafiti wangu kutambulika kwa kiwango cha juu katika mkutano wa AHA. Hii ni kwa sababu ya ubora wa kisayansi, uvumbuzi, na athari za utafiti huu katika kuelewa magonjwa ya moyo yanayoathiri uzazi duniani,” alisema Dkt. Pedro.

Amefafanua kuwa ushindi wa tuzo hizo katika mwaka mmoja ni mafanikio makubwa na ya nadra, sio tu kwa Taasisi ya  Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  bali pia kwa taifa, hatua iliyowashangaza wataalamu na wanasayansi wa kimataifa waliokuwepo kwenye mkutano huo.

Dkt. Pedro alisema kuwa ugonjwa wa PPCM ni nadra lakini hatari, na huwapata wanawake katika kipindi cha mwisho cha ujauzito au muda mfupi baada ya kujifungua.

“Utafiti huu wa muda mrefu umebaini kundi kubwa zaidi la wagonjwa wa PPCM duniani na umeleta mwanga mpya katika utambuzi, usimamizi na matokeo ya ugonjwa huu,” aliongeza.
Mafanikio hayo alisema yanaiweka Tanzania na Afrika Mashariki katika ramani ya kimataifa ya sayansi, hasa katika eneo la afya ya mama na magonjwa ya moyo.

Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi

Msumbiji kushirikiana na JKCI katika tiba ya moyo