JKCI, MSD kuwafuata wananchi Arusha kupima magonjwa ya moyo

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Janeth Mmari akimfafanulia mwananchi kuhusu magonjwa ya moyo mara baada ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalumu iliyofanywa na Taasisi hiyo kabla ya kuanza kwa mechi ya mpira wa miguu baina ya mashabiki wa timu za Simba na Yanga jana katika Uwanja wa mpira wa KMC uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.

****************************************************************************************************************************************************************************************************************** 

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Bohari ya Dawa (MSD)  itafanya kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa  mbalimbali yakiwemo ya moyo  kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani kuanzia Desemba 29, 2025 hadi Januari 5, 2026, katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC).

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge alisema taasisi hiyo imefanya upimaji wa magonjwa ya moyo katika mikoa zaidi ya 16, ambapo wagonjwa zaidi ya 23,000 walihudumiwa, huku mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikionesha uhitaji mkubwa zaidi wa huduma hizo.

“Tunaenda kufanya upimaji na kutoa elimu ya afya ya moyo ili kuokoa wananchi wengi wasiendelee kupata madhara yatokanayo na magonjwa haya,” alisema Dkt. Kisenge.

Alisema kambi hiyo itahusisha upimaji wa magonjwa mbalimbali yakiwemo ya  moyo na magonjwa yasiyoambukiza, kwa watoto na watu wazima, na huduma zitatolewa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni.

Dkt. Kisenge aliongeza kuwa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre imeingia ushirikiano wa miaka 20 na JKCI, ambapo kuanzia Januari 1, 2026, hospitali hiyo itasimamiwa na JKCI kwa lengo la kusogeza huduma bora za moyo na matibabu ya magonjwa mengine karibu na wananchi wa Kanda ya Kaskazini.

“Tunaendelea kuonesha utu kwa kuwafuata wananchi walipo ili kuokoa maisha yao. Tunawasihi wananchi kuhakikisha wanazingatia afya ya mioyo yao na kubadili mitindo ya maisha,” alisisitiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Matibabu ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane, alisema zaidi ya asilimia 25 ya wagonjwa wanaopata huduma JKCI wanatoka Kanda ya Kaskazini, hivyo ushirikiano huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kusogeza huduma karibu na wananchi.

“Uwepo wetu Arusha utapunguza gharama za kufuata huduma mbali, kuboresha huduma za moyo na kujiandaa kwa ongezeko la watalii wanaotembelea mbuga za wanyama, Mlima Kilimanjaro pamoja na maandalizi ya mashindano ya AFCON,” alisema Dkt. Waane ambaye pia ni baktari bingwa wa moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba.

Naye Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Bohari ya Dawa (MSD), Etty Kusiluka, alisema katika kambi hiyo MSD itahakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wakati kupitia Kanda ya Kaskazini ya MSD iliyopo Kilimanjaro, ili kuhakikisha huduma za matibabu zinatolewa kikamilifu.

“Wakati JKCI inasogeza huduma kwa wananchi, sisi tutahakikisha vifaa na dawa muhimu vinapatikana ili kukamilisha matibabu yote yanayohitajika. Tuko tayari kwa ushirikiano huu,” alisema Etty.


Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi

Msumbiji kushirikiana na JKCI katika tiba ya moyo