Wagonjwa 760 kunufaika na mpango wa bilioni 6.7 wa Serikali
.jpeg)
Baadhi ya viongozi wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimsikiliza Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa
(MB) wakati wa kikao kazi cha watumishi
wa sekta ya afya kilichofanyika hivi karibuni katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Picha na JKCI
Na JKCI
*************************************************************************************************
Serikali ya awamu ya sita imetenga kiasi cha shilingi bilioni
6.7 katika mwaka wa fedha 2025/2026 kwaajili ya kuwezesha upatikanaji wa huduma
za ubingwa bobezi kwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu hayo.
Fedha hizo zimelenga kuwahudumia wagonjwa takribani 760
wanaotibiwa katika Hospitali ya Taifa na Taasisi zinazotoa huduma za ubingwa bobezi ikiwemo Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI).
Akizungumza hivi karibuni na
wafanyakazi wa sekta walioko mkoa wa Dar es Salaam Waziri wa Afya Mhe.
Mohamed Mchengerwa alisema hatua hiyo ni muendelezo wa yaliyofanyika mwaka
2024/2025 ambapo serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni nane zizizogharamia
matibabu ya wagonjwa 677 wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu ya kibingwa.
Aidha Mhe. Mchengerwa alizitaka hospitali zote nchini kuboresha ubora wa huduma na kuanza mchakato
wa kupata ithibati za kimataifa zitakazowawezesha kutambulika kimataifa na
kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia katika kutoa huduma bora za afya.
Mhe. Mchengerwa alisema hospitali hizo zinatakiwa kuhakikisha
zinatoa huduma bora salama na zenye kuwajali wagonjwa ili ziweze kupata
ithibati itakayowasaidia kubeba soko la kimataifa, kutambuliwa kimataifa na
kuongeza pato la taifa.
“Naipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuanza
mchakato wa kupata ithibati za kimataifa (ISO) katika kutoa huduma za ubingwa
bobezi za magonjwa ya moyo nchini na nimesikia ipo katika hatua nzuri,
hongereni sana”, alisema Mhe. Mchengerwa.
Mhe. Mchengerwa alizitaka hospitali hizo bingwa kuimarisha
huduma za upatikanaji wa dawa kwa wagonjwa, kuimarisha afya na kinga zaidi
kuliko tiba, kuimarisha utafiti, ubunifu na tiba shirikishi na kuongeza
matumizi ya teknolojia za kisasa katika kutoa huduma.
“Kwa nini mgonjwa azunguke vitengo mbalimbali vya hospitali
kufungua faili wakati teknolojia inaruhusu kufungua faili hilo mtandaoni.
Ninawaomba kupitia TEHAMA anzisheni mfumo wa One Stop Digital Center mara moja
ambao mgonjwa anaweza kufungua faili lake akiwa mtandaoni, akapata control
namba ya malipo ya huduma akiwa mtandaoni, hii itapunguza foleni na muda wa
kukaa hospitali”, alisema Mhe. Mchengerwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema
mambo mengi yaliyosemwa na Mhe. Waziri katika hotuba yake JKCI
imeshayafanyia kazi ikiwemo hatua za kupata ithibati za kimataifa, mambo ya
kuendesha taasisi kimtandao na masuala mbalimbali ya wafanyakazi.
“Tumefurahi leo kukutana na Mhe. Waziri wa afya kwa mara ya
kwanza tangu ateuliwe, tunashukuru kwa maelekezo yake na tunaahidi kuwa JKCI
tutayatekeleza yale yote aliyoyasema”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema JKCI inaahidi kuendelea kuwahudumia
vizuri wagonjwa wake na kuyafuata yote aliyoyaelekeza Mhe. Waziri wakiwa na
lengo la kufikisha huduma bora kwa wananchi na kufuta kabisa haja ya wagonjwa
kwenda nje ya nchi kupata huduma za ubingwa bobezi za moyo.
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
Comments
Post a Comment