JKCI kuisimamia ALMC, huduma za moyo na magonjwa alekezi zasogezwa Kaskazini
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha kuhusu makubaliano ya ushirikiano yaliyosainiwa kati ya taasisi hiyo na Arusha Lutheran Medical Center (ALMC).
.jpeg)
Baadhi ya Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha kuhusu makubaliano ya ushirikiano yaliyosainiwa kati ya taasisi hiyo na Arusha Lutheran Medical Center (ALMC).
**********************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imesaini makubaliano ya kuisimamia Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) kwa kipindi cha miaka 20, kwa lengo la kutoa huduma za matibabu ya moyo pamoja na magonjwa elekezi ya moyo na magonjwa mengine ya kibingwa kwa wananchi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Hayo
yamesemwa leo jijini Arusha na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge,
wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu makubaliano ya ushirikiano
yaliyosainiwa kati ya taasisi hiyo na ALMC.
Dkt.
Kisenge, ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mtaalamu wa
kuzibua mishipa ya damu ya moyo, alisema ushirikiano huo unalenga kusogeza
huduma za ubingwa na ubingwa bobezi wa matibabu ya moyo pamoja na magonjwa
tegemezi karibu na wananchi, ili kupunguza gharama na usumbufu wa kusafiri
umbali mrefu kufuata huduma hizo.
“Lengo kuu la
makubaliano haya ni kuboresha upatikanaji wa huduma za kibingwa za matibabu ya
moyo na magonjwa mengine kwa wananchi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini, ambao kwa
sasa hawatalazimika tena kusafiri hadi Dar es Salaam kufuata huduma hizi, kwani
zitapatikana hapa ALMC,” alisema Dkt. Kisenge.
Aliongeza
kuwa kuanzia Januari 1, 2026, JKCI itasimamia utoaji wa huduma zote za matibabu
katika hospitali hiyo, huku ikiendelea kutumia rasilimali watu waliopo,
sambamba na kupeleka wataalamu wake wa ubingwa bobezi, hususan madaktari bingwa
wa magonjwa ya moyo.
“Kwa upande wa huduma
za moyo, tayari tumeanza kuwahamishia baadhi ya madaktari bingwa kutoka JKCI
ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kiwango cha juu,”
alisisitiza.
Dkt.
Kisenge alisema kwa hatua hiyo, wananchi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani
hawana tena sababu ya kusafiri kwenda Dar es Salaam kufuata huduma za matibabu
ya moyo, akiahidi kuwa chini ya uongozi wa JKCI, ALMC itatoa huduma za kiwango
cha kimataifa, sawa na zile zinazotolewa katika Hospitali ya JKCI Upanga jijini
Dar es Salaam.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Arusha Lutheran Medical Center (ALMC), Dkt.
Goodwill Kivuyo, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia ombi la taasisi hiyo kushirikiana na JKCI,
akisema mchakato wa kuomba ushirikiano huo ulianza tangu mwaka 2023.
“Tunamshukuru Rais
kwa kusikiliza na kuridhia ombi letu. Ushirikiano huu na JKCI, ambayo ni
hospitali kubwa ya kibingwa nchini, tunaamini utakuwa na manufaa makubwa kwa
wananchi na kwa Kanisa,” alisema Dkt. Kivuyo.
Aliongeza
kuwa mkoa wa Arusha ni kitovu cha utalii kinachopokea wageni wengi kutoka
mataifa mbalimbali, hivyo uwepo wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika
hospitali hiyo utasaidia pia kuwahudumia watalii watakaopata changamoto za
kiafya wakiwa nchini.
Pamoja na JKCI kuisimamia ALMC katika utoaji wa huduma za matibabu, umiliki wa hospitali hiyo utaendelea kubaki chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati (DKAK).

.jpeg)
Comments
Post a Comment