Tumaini jipya kwa watoto wenye magonjwa ya moyo: JKCI na China waunganisha nguv
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi wa Fedha wa International Health Exchange and Cooperation Center kutoka nchini China, Yong Yu alipotembelea taasisi hiyo kufuatilia utekelezaji wa ushirikiano katika matibabu ya moyo kwa watoto ikiwa ni ahadi ya Rais wa nchi hiyo Xi Jinping aliyoitoa katika Mkutano wa Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika mwaka 2024.
Watoto wa Kitanzania wenye magonjwa ya moyo wanatarajiwa kunufaika na huduma za uchunguzi, matibabu na upasuaji wa moyo bila malipo, kupitia ushirikiano mpya kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Watu wa China unaotekelezwa kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Ushirikiano huo ni sehemu ya utekelezaji wa
ahadi ya Rais wa China Xi Jinping
aliyoitoa katika Mkutano wa Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC)
uliofanyika mwaka 2024, akisisitiza kuimarishwa kwa ushirikiano wa sekta ya
afya kati ya China na Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati viongozi
kutoka International Health Exchange and
Cooperation Center ya nchini China walipotembelea taasisi hiyo Mkurugenzi
Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge
alisema Serikali ya China imetuma timu ya wataalamu wa afya nchini kwa ajili ya
maandalizi ya andiko la makubaliano ya ushirikiano (MoU), hatua itakayowezesha
mpango huo kuanza rasmi mwaka ujao.
Alisema lengo la ushirikiano huo ni kujenga uwezo wa wataalamu wa afya wa
Tanzania, kupitia mafunzo na elimu ya juu yatakayowawezesha kufikia
viwango vya kimataifa katika matibabu ya magonjwa ya moyo.
“Wataalamu kutoka Serikali ya Watu wa China
wamefika JKCI ili kuona kwa vitendo namna ya kuanza ushirikiano huu unaolenga
kukuza taaluma za wataalamu wetu wa afya,” alisema Dkt. Kisenge.
Aliongeza kuwa kupitia mpango huo, uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo
utafanyika kwa watoto waliopo mashuleni na wale watakaobainika kuwa na
matatizo ya moyo watapatiwa matibabu huku baadhi yao wakifanyiwa upasuaji wa moyo bila gharama yoyote.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo alisema
mafanikio hayo yametokana na uongozi
thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika kuimarisha huduma za ubingwa bobezi ndani ya nchi hatua
iliyoiwezesha Tanzania kuvutia ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya afya.
“Kupitia ushirikiano huu JKCI itanufaika kwa
kupatiwa vifaa tiba vya kisasa vitakavyotolewa bila gharama, jambo
litakaloimarisha zaidi huduma za upasuaji wa moyo nchini na kupunguza rufaa za
nje,” alisema.
Aidha Dkt. Kisenge alisema ushirikiano huo
utahusisha pia tafiti za magonjwa ya
moyo zitakazosaidia kubaini mapema vihatarishi na kulinda afya za wananchi,
hususan watoto.
Kwa mujibu wa Dkt. Kisenge, lengo la muda
mrefu la ushirikiano huo ni kuifanya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
kuwa kituo kikubwa cha rufaa cha matibabu ya moyo barani Afrika na duniani.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya
moyo kwa watoto kutoka Hospitali ya Shandong
Provincial iliyopo nchini China ambaye pia anafanya kazi JKCI Zhao Lijian alisema ushirikiano huo ni
hatua muhimu katika kuimarisha huduma za matibabu ya moyo kwa watoto barani
Afrika hususan Tanzania.
Alisema timu ya wataalamu kutoka China
imevutiwa na kiwango cha huduma kinachotolewa na JKCI hali iliyochangia
Serikali ya China kuona umuhimu wa kushirikiana na taasisi hiyo ili kuboresha
zaidi uchunguzi, matibabu na upasuaji wa moyo kwa watoto bila gharama.
“Ushirikiano huu utawapa wataalamu wa magonjwa
ya moyo wa Tanzania fursa ya kubadilishana uzoefu wa kazi, kupata mafunzo ya
vitendo na kutumia teknolojia za kisasa za matibabu ya moyo,” alisema Dkt.
Zhao.
Aliongeza kuwa hatua hiyo itaongeza uwezo wa
ndani na kuhakikisha huduma za ubingwa bobezi kwa watoto zinaendelea kutolewa
hata baada ya kukamilika kwa programu ya ushirikiano.
Dkt. Zhao alisema China itaendelea
kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania na JKCI kuhakikisha watoto
wanaogundulika kuwa na magonjwa ya moyo wanapata matibabu kwa wakati huku lengo
kuu likiwa ni kuokoa maisha ya watoto,
kuimarisha urafiki wa muda mrefu kati ya Tanzania na China, na kuchangia
maendeleo ya sekta ya afya nchini.
Comments
Post a Comment