Afya kwanza: JKCI yahakikishia usalama wa mioyo ya wanamichezo Chipukizi Cup Arusha

Wataalamu wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar wakiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Duwa Sports Club wanaoshiriki katika mashindano ya16 ya Chipukizi Cup yanayofanyika katika viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT) vilivyopo jijini Arusha.


Mtalaamu ya vipimo vya moyo  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Nelson Kolukwi akimpima kipimo cha kuangalia jinsi mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi mchezaji wa  PE Academy ya nchini Zimbabwe wakati wa mashindano ya16 ya Chipukizi Cup vilivyopo katika viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT) vilivyopo jijini Arusha.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group ambaye pia ni mratibu wa magonjwa ya moyo kwa wanamichezo Eva Wakuganda akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi mchezaji wa Future Stars Academy (FSA) anayeshiriki mashindano ya 16 ya Chipukizi Cup katika viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT) vilivyopo jijini  Arusha.


Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda akitoa elimu ya kujikinga na magonjwa ya moyo kwa wachezaji wa Singida Green Sport Academy katika mashindano ya16 ya Chipukizi Cup yanayofanyika katika viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT) vilivyopo jijini Arusha.

 Afisa Muuguzi Msaidizi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Mumtaaz Farid akimpima shinikizo la damu mchezaji wa Future Starts Academy (FSA) anayeshiriki mashindano ya16 ya Chipukizi Cup yanayofanyika katika viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT) vilivyopo jijini Arusha.

************************************************************************************************************************************************************

Zaidi ya wanamichezo 176 wamenufaika na huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa bila malipo na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika mashindano ya 16 ya Chipukizi Cup yanayofanyika katika  viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT) jijini  Arusha.

Zoezi hilo la siku nne limekuwa msaada mkubwa kwa wanamichezo chipukizi, kwa kuwa limewasaidia kutambua mapema hali za afya ya mioyo yao na kuepuka hatari ya kupata matatizo ya moyo yanayoweza kujitokeza ghafla wakati wa mazoezi makali au mashindano.

Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka JKCI, Hospitali ya Dar Group Dkt. Eva Wakuganda alisema  wanamichezo waliopatiwa huduma hizo wanatoka mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda na Zimbabwe.

Alisema uchunguzi wa awali wa afya ya moyo ni hatua muhimu kwa wanamichezo hasa katika mashindano makubwa, kwani baadhi yao huzaliwa na matatizo ya moyo yasiyoonekana kwa macho lakini yanaweza kusababisha madhara makubwa wanapofanya mazoezi makali.

“Mazoezi yana faida nyingi kiafya; huimarisha afya ya mwili, huongeza uwezo wa kufikiri na hupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo. Hata hivyo faida hizo hupatikana zaidi endapo uchunguzi wa afya utafanyika mapema,” alisema  Dkt. Eva.

Hata hivyo alisisitiza umuhimu wa kuzingatia usalama wa kiafya kabla ya kushiriki michezo ya ushindani.

“Tunashauri wanamichezo wafanyiwe uchunguzi na wenye matatizo wapatiwe matibabu ya moyo kabla ya kushiriki mazoezi makali au mashindano, ili kubaini mapema viashiria vyovyote vinavyoweza kusababisha madhara au vifo vya ghafla viwanjani,” aliongeza.

Kwa upande wake mchezaji kutoka Future Star Academy ya jijini Arusha  Arusha, Paschal Bugeraha alisema  huduma hiyo imewajengea uelewa  wa magonjwa ya moyo na kujiamini zaidi.

“Upimaji huu umetusaidia kujua hali za afya ya mioyo yetu na kupata elimu kuhusu dalili za magonjwa ya moyo. Endapo tutaziona dalili hizo, tutaweza kuchukua hatua mapema,” aalisema Bugeraha.

Naye mchezaji  kutoka Kilimanjaro  Alice Emmanuel  aliipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete  (JKCI)  kwa kutoa huduma bora na za kitaalamu za magonjwa ya moyo.


“Huduma za moyo zinazotolewa na JKCI ni za kiwango cha juu. Madaktari akiwemo Dkt. Eva na timu yake, wametupokea vizuri na kutuhudumia kwa weledi mkubwa,” alisema.

Zoezi la uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wanamichezo katika mashindano ya 16 ya Chipkiz Cup linafanyika kuanzia tarehe 15 hadi 21 Desemba 2025 katika viwanja vya michezo vya Tanganyika Game Trackers (TGT) mkoani Arusha.

Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi

Msumbiji kushirikiana na JKCI katika tiba ya moyo