Dkt. Peter Kisenge awataka wafanyakazi ALMC kujituma
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wafanyakazi wa Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) wakati wa kikao cha kutoa mwelekeo wa kazi na mustakabali wa uendeshaji wa hospitali hiyo ambayo kuanzia tarehe 1/1/2026 itakuwa chini ya usimamizi wa JKCI. ALMC inamilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati (DKAK).
Mwenyekiti wa Bodi ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) Peter Maduki akizungumza na wafanyakazi wa Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) wakati wa kikao cha kutoa mwelekeo wa kazi na mustakabali wa uendeshaji wa hospitali hiyo ambayo kuanzia tarehe 1/1/2026 itakuwa chini ya usimamizi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI). ALMC inamilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati (DKAK).
*****************************************************************************************************************************************************************************************
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, amewataka wafanyakazi wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kuzingatia maadili ya kazi ili kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Dkt.
Kisenge ametoa wito huo leo wakati akizungumza na wafanyakazi wa hospitali
hiyo, ambayo kuanzia tarehe 1/1/2026 itakuwa chini ya usimamizi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Alisema JKCI
imejipanga kupokea mawazo bunifu na matumizi ya teknolojia kutoka kwa wafanyakazi
kama sehemu ya kuimarisha utamaduni wa kazi unaolenga kuongeza ufanisi na ubora
wa huduma za afya.
“Tutahakikisha
ubunifu unakuwa sehemu ya utamaduni wetu wa kazi. Hatutafanya kazi kwa mazoea,
bali tutaweka ubunifu katika kila tunachokifanya. Pia tutaandaa mpango wa
motisha (incentive plan) ndani ya bajeti kwa wafanyakazi watakaoleta ubunifu
katika utekelezaji wa majukumu yao na tutawazawadia,” alisema Dkt. Kisenge.
Aidha, aliwapongeza
wafanyakazi wa hospitali hiyo kwa kuvumilia changamoto mbalimbali na kuendelea
kutoa huduma kwa wagonjwa bila kukata
tamaa.
“Mmekuwa mkikabiliwa
na changamoto nyingi, lakini mmeendelea kusimama imara kwa kuwajali na
kuwahudumia wagonjwa. Mwenyezi Mungu
awabariki sana,” aliongeza Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC), Peter
Maduki, alisema hospitali hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto za uendeshaji,
hususan upande wa kifedha na upatikanaji wa wagonjwa.
“Uendeshaji
wa hospitali yetu umekuwa mgumu kutokana na upungufu wa fedha pamoja na idadi
ndogo ya wagonjwa wanaokuja kupata huduma ukilinganisha na miaka ya nyuma,”
alisema Maduki.
Alibainisha kuwa
ushirikiano kati ya ALMC na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ni hatua
muhimu ya kuikomboa hospitali hiyo kifedha na kuongeza idadi ya wananchi watakaokwenda
kupata huduma.
“Tumeamua kuingia
ubia na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ili kuhakikisha hospitali yetu
inaendelea kutoa huduma sasa na baadaye, huku tukilenga kuiweka katika hali
imara ya kifedha kwa ajili ya uendelevu,” alisema.
Nao wafanyakazi wa
Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) waliishukuru Serikali kupitia uongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) kwa kuchukua hatua ya kuisimamia hospitali hiyo, wakisema hatua hiyo
imeleta matumaini mapya katika utoaji wa huduma za afya.
Mmoja
wa wafanyakazi wa hospitali hiyo alisema ujio wa JKCI umeongeza morali na imani
ya wafanyakazi katika kuboresha huduma kwa wananchi.
“Tunaishukuru
sana Serikali inayoongoza na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia JKCI
kwa kutusikiliza na kutupa mwelekeo mpya. Uongozi huu umetupa moyo wa kufanya
kazi kwa bidii zaidi na kwa weledi,” alisema Msimamizi wa Wauguzi wa Hospitali
hiyo Afisa Muunguzi Magdalena Shangay.
Mfanyakazi mwingine
alisema kuwa wamepokea maelekezo na dira mpya ya kazi inayowahamasisha kujituma
na kushirikiana.
“Tunatoa
ahadi ya kushirikiana na uongozi mpya, kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na
uaminifu ili hospitali yetu iwe mfano wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi na
wagonjwa kwa ujumla ,” alisema Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi na Wakunga
Tanzania (TANNA) tawi la ALMC Afisa Muuguzi Anton Patrick.
Mkataba
wa ushirikiano wa miaka 20 uliosainiwa kati ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) na Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) inayomilikiwa na Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati (DKAK) unaashiria
mwanzo wa sura mpya katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Kanda ya
Kaskazini.
Comments
Post a Comment