JKCI yatoa wito kwa wanamichezo nchini kupima afya ya moyo mara kwa mara
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda akimsomea majibu mchezaji
anayeshiriki mashindano ya 16 ya Chipkiz Cup yanayofanyika katika viwanja vya
Tanganyika Game Trackers (TGT) vilivyopo jijini Arusha.
Wachezaji wa Singida Green Sports Academy kwenye picha ya
baada ya kupata elimu ya kujikinga na magonjwa ya moyo wakati wa mashindano ya
16 ya Chipkiz Cup yanayofanyika katika viwanja vya Tanganyika Game Trackers
(TGT) vilivyopo jijini Arusha.
*******************************************************************************************************************
Takwimu za shirika la National
Collegiate Athletic Association (NCAA) za mwaka 2024 zinaonesha kuwa kati ya
wanamichezo 50,000 mmoja yupo katika hatari ya kudondoka na kupoteza maisha
ghafla kutokana na matatizo ya moyo yanayotokana na sababu za kuzaliwa au
mabadiliko yanayojitokeza baada ya kushiriki michezo kwa muda mrefu.
Hayo yameelezwa na Daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)
Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda wakati wa zoezi la uchunguzi wa afya ya
moyo kwa wanamichezo wanaoshiriki mashindano ya 16 ya chipkiz cup katika
viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT) mkoani Arusha.
Dkt. Wakuganda amesema kuwa kutokana
na changamoto hizo Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeanzisha kitengo
maalum cha kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wanamichezo ndani
nan je ya nchi.
“Hiki ni kitu muhimu sana ambacho
kama Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete tumekianzisha ili kuwafikia wanamichezo
wa ngazi mbalimbali kuanzia timu za taifa, vilabu mbalimbali, michezo ya aina
zote, wanamichezo wanaofanya mazoezi katika gym pamoja na wanafunzi mashuleni”.
Alisema Wakuganda.
Ameeleza kuwa kwa wanamichezo wote
waliokuja kufanya uchunguzi na matibabu ya moyo wamepewa ushauri wa kitaalamu
ikiwemo dalili za hatari wanazopaswa kuzingatia na umuhimu wa kufanya uchunguzi
wa mara kwa mara wa afya ya moyo.
Dkt. Wakuganda ametoa wito kwa
wanamichezo wote nchini Tanzania kutumia fursa hiyo kwa kufika Tasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya moyo.
“Kwa sasa tunakaribisha wanamichezo
wote kuja kupima afya zao ili kubaini uwezo wao wa kimwili kuboresha utendaji
na kuzuia vifo vya ghafla vinavyoweza kuzuilika”. Alisema Dkt. Wakuganda.
Kwa upande wake Kocha wa Kibera Agoal
Academy kutoka Kenya Emmanuel Ouma ameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
kwa huduma walizotoa kwa wanamichezo, amesema kuwa huduma hizo ni muhimu sana
katika kuzuia vifo vya ghafla uwanjani.
“Nimeshuhudia kwa macho yangu
mwanamichezo mwenzangu akifariki uwanjani kwasababu hajawahi kufanya uchunguzi
na matibabu ya moyo, ndiyo maana ninashukuru sana JKCI kwa kazi kubwa
wanayoifanyakwani inasaidia walimu na makocha kufahamu hali ya afya za
wachezaji wetu”. Alisema Ouma.
Naye mchezaji wa Arusha Youth
Development Organization Academy Hossian Lowasa amesema zoezi la kupima afya ya
moyo limemsaidia kufahamu hali yake ya kiafya.
“Nimeshauriwa kuendelea kufanya
mazoezi kwa usahihi kuzingatia lishe bora na kula matunda ili kulinda afya ya
mwili wangu”. Alisema Hossiana.
Kwa upande wakemchezaji wa Kibera
Agoal Academy kutoka Kenya Labida Basmi amesema ameridhishwa na huduma za afya
zilizotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
“Nimefurahi sana kushiriki
mashindano haya na kupata huduma nzuri za afya, nawashukuru sana wataalamu wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa huduma wanazotupatia”. Alisema Basmi.
Mashindano haya ya 16 ya Chipkiz cup
yanaendelea kufanyika mpaka tarehe 21 Desemba 2025 katika viwanja vya Tanganyika
Game Trackers (TGT) mkoani Arusha, na kuuhudhuriwa na wanamichezo kutoka nchi
tofauti kama vile Tanzania, Kenya, Uganda na Zimbabwe
Comments
Post a Comment