Dumisheni ushirikiano kuwahudumia wagonjwa – Dkt. Kisenge


 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi hiyo leo katika Ukumbi wa JKCI katika kikao cha kuangalia utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo kwa kufuata mpango mkakati wa mwaka 2022/23 – 2026/27.

Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo na Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023 kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo wakati wa kikao cha kuangalia utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo kwa kufuata mpango mkakati wa mwaka 2022/23 – 2026/27.

Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakisikiliza taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023 wakati wa kikao cha kupitia utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo kwa kufuata mpango mkakati wa mwaka 2022/23 – 2026/27.

Afisa Tehama wa Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Fiona Kavishe akielezea namna ambavyo Kitengo cha Tehama kimejipanga kuboresha huduma wakati wa kikao cha kupitia utekelezaji wa majukumu ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023 kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo kwa kufuata mpango mkakati wa mwaka 2022/23 - 2026/27.

Daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Loth akitoa hoja wakati wa kikao cha kupitia utekelezaji wa majukumu ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023 kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo kwa kufuata mpango mkakati wa mwaka 2022/23 - 2026/27.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Sulende Kubhoja akichangia mada wakati wa kikao cha kupitia utekelezaji wa majukumu ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023 kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo kwa kufuata mpango mkakati wa mwaka 2022/23 - 2026/27.

*******************************************************************************************************************************************************************************

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kuendelea kudumisha ushirikiano wa kuwahudumia watanzania wenye matatizo ya moyo kwa kufanya hivyo wagonjwa watapata huduma iliyo bora zaidi.

Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na wafanyakazi hao katika kikao cha kutoa taarifa ya kazi zilizofanyika kwa kipindi cha miezi mitatu ya Julai hadi Septemba mwaka huu.

Taarifa hiyo ya kazi inaenda sambamba na utelekezaji wa mpango mkakati wa  mwaka 2022/23 – 2025/26 ambao Taasisi hiyo imejiwekea.

Dkt. Kisenge alisema wananchi wenye matatizo ya moyo wanawategemea wafanyakazi wa Taasisi hiyo ili wawape huduma bora ya matibabu hivyo basi jukumu lao ni kuhakikisha wagonjwa wanaowatibu wanapata matibabu mazuri bila ya kuwa na manung’uniko yoyote yale.

“Mnanifahamu mimi ni mchapa kazi na ninapenda kuwahudumia vizuri wagonjwa, nitasimamia  kazi ziende kama inavyotakiwa ili Taasisi yetu iweze kufika mbali zaidi  jambo la muhimu kweni ni kuwaunga mkono viongozi wenu kwa kufanya kazi kwa ushirikiano ili malengo tuliyojiwekea yaweze kufikiwa,”.

“Fanyeni kazi ya kuwahudumia wagonjwa kwa kufuata miongozo na taratibu za tiba zilizopo hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wagonjwa wanapata tiba sahihi na kwa wakati kwa kufanya hivyo wagonjwa hawatakaa muda mrefu Hospitali wakisubiri kupata huduma za matibabu,” alisema Dkt.Kisenge.

Kuhusu wananchi wengi zaidi kufikiwa na huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo Dkt.Kisenge alisema JKCI imesogeza  huduma zake kwa wananchi kwa kuwafuata mahali walipo pia inatoa elimu kwa wataalamu wa afya walioko katika hospitali za mikoa ya jinsi ya kufanya vipimo na kuwatambua wagonjwa wa moyo kitu ambacho kitasaidia  wagonjwa kutambulika na kuanza matibabu mapema.

Aidha Mkurugenzi Mtendaji huyo ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo aliiagiza Kurugenzi ya Utawala na Rasiliamali watu kuhakikisha kila mfanyakazi anapata nakala ya mpango mkakati wa JKCI wa mwaka 2022/23-2025/2026 ili aweze kuyasoma malengo yaliyowekwa  katika idara yake na kuweza kuyafanyia kazi.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia utetekelezaji wa mpango mkakati huo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo alisema mpango huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa hii imeonekana katika taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo zilizofanyika kwa kipindi cha miezi mitatu ya robo mwaka wa fedha 2022/23.

“Tumeona utekelezaji wa mpango mkakati umefanikiwa katika maeneo mbalimbali hii ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma za matibabu kwa wagonjwa kwani idadi ya wagonjwa tunaowaona na kuwafanyia upasuaji imeongezeka, Taasisi imetoa mafunzo ya jinsi ya kuwatambua wagonjwa wa moyo pamoja na kufanya vipimo kwa wataalamu wa kada za afya kutoka hospitali mbalimbali,”.

“Kamati yetu itasimamia kila Idara ili kuhakikisha vipaumbele walivyojiwekea vinafanikiwa pia tutahakikisha kila mfanyakazi anaufahamu zaidi mpango mkakati huu kwa kutoa elimu ya mara kwa mara,” alisema Dkt. Pallangyo.

Kwa upande wa wafanyakazi waliohudhuria mkutano huo waliupongeza uongozi wa JKCI kwa kusimamia mpango mkakati huo ambao umewawezesha kufanya kazi zao za kuhudumia wananchi  na kutimiza malengo waliyojiwekea.

“Leo hii tumesomewa taarifa ya kazi tulizozifanya kwa kipindi cha miezi mitatu na kuweza kuona kama tumefanikiwa kutimiza malengo tuliyojiwekea au la, hiki ni kitu kizuri kwani kila mtu sasa atakuwa anafanya kazi ili kuhakikisha malengo aliyojiwekea yanatimia jambo ambalo litaifanya Taasisi yetu ifike mbali zaidi,” alisema Dkt. Godwin Sharau.


Comments

Popular posts from this blog

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024

Maabara ya JKCI yapata ithibati ya kimataifa (ISO 15189:2012)