Watoto 64 wafanyiwa upasuaji wa moyo; Serikali yaokoa shilingi bilioni 1.6
Wataalamu wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Muntada Aid lenye makao yake makuu jijini London nchini Uingereza kupitia mradi wa Little Heart wakifanya upasuaji wa bila kufungua kwa kupasua sehemu ndogo kwenye paja kwa kutumia mtambo wa Cathlab kuziba tundu la moyo wa mtoto katika kambi maalum ya matibabu ya moyo ya siku sita iliyomalizika leo jijini Dar es Salaam. Katika kambi hiyo watoto 64 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo; matundu na mishipa ya damu walifanyiwa upasuaji wa kufungua na bila kufungua kifua.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu kambi maalum ya upasuaji wa moyo iliyomalizika leo katika Taasisi hiyo ambapo watoto 64 wamefanyiwa upasuaji. Upasuaji huo umefanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Shirika la Muntada Aid lililopo jijini London nchi Uingereza kupitia mradi wa Little Heart.
Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya akielezea matibabu waliyopatiwa watoto 64 waliofanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalum ya matibabu iliyofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Muntada Aid lililopo jijini London nchini Uingereza kupitia mradi wao wa Little Heart.
Meneja kutoka Shirika la Muntada Aid lililopo jijini London nchini Uingereza Kabir Miah akiwashukuru wataalam wa afya kutoka nchi mbalimbali waliojitolea kufanya kambi maalum ya siku sita ya upasuaji wa moyo kwa watoto iliyomalizika leo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) .
Wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Shirika la Muntada Aid lililopo jijini London nchini Uingereza wakiwa wameinamisha vichwa vyao chini ikiwa ni kumbukizi ya baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa kuhitimisha kambi maalum ya siku sita ya upasuaji wa moyo kwa watoto 64.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya Taasisi hiyo na madaktari kutoka shirika la Muntada Aid la jijini London nchini Uingereza wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa kuhitimisha kambi maalum ya upasuaji wa moyo uliofanyika kwa watoto 64.
Picha na Khamisi Mussa
*******************************************************************************************************************************************************************************************
Watoto 64 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo
wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalum ya matibabu ya siku sita iliyomalizika
leo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Watoto hao walikuwa na matatizo ya matundu pamoja na mishipa
ya damu ya moyo ambapo 20 walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na 44
walifanyiwa upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab.
Upasuaji huo ulifanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo kwa
watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka
Shirika la Muntada Aid lenye makao yake makuu jijini London nchini Uingereza
kupitia mradi wake wa Little Heart.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dkt. Peter Kisenge
alisema kupitia kambi hiyo ya siku sita serikali imeokoa kiasi cha shilingi bilioni 1.6 fedha ambazo
zingetumika kama watoto hao wengeenda kufanyiwa upasuaji huo nje ya nchi.
“Kupitia kambi hii madaktari wetu wameweza kujifunza mbinu
mpya za kitabibu kwasababu shirika hili ilimekuwa likileta madaktari kutoka
sehemu mbalimbali duniani hivyo kutuwezesha kupata ujuzi mpya waliona wenzetu,”.
“Tunamshukuru Rais wetu wa serikali ya awamu ya sita Mhe.
Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye miundombinu na
rasilimali watu katika Taasisi yetu hivyo kuifanya Taasisi hii kuwa na uwezo
mkubwa katika kutoa huduma za kibobezi kwa watanzania wanaohitia huduma za
matibabu ya moyo,” alisema Dkt. Kisenge.
Aidha Dkt. Kisenge aliwaomba wananchi kujiunga na bima ya afya mara baada
ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha sheria ya bima ya afya
kwa wote ili kukidhi gharama za matibabu pale watakapougua kwani magonjwa
yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo ni gharama kuyatibu.
Dkt. Kisenge alisema matibabu ya moyo yameigharamu fedha
nyingi Serikali kusaidia jamii kwani wananchi wengi hawana uwezo wa kukidhi
gharama za matibabu ya moyo kutokana na gharama zake kuwa kubwa lakini kama
wananchi hao watajiunga na bima ya afya kutapunguza mzigo mkubwa ulioachiwa Serikali
na kuiwezesha Taasisi hiyo kufanikisha matibabu ya watoto wengi zaidi.
“Upasuaji wa moyo kwa mtoto unagharimu shilingi milioni nane na
kuendelea kama mtoto huyo atafanyiwa upasuaji hapa nchini lakini akipelekwa nje
ya nchi itamgharimu kiasi cha shilingi milioni 25 kufanyiwa upasuaji, kama
tutakata bima za afya itatusaidia kukidhi gharama za matibabu pale tunapopatwa
na maradhi,” alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Meneja kutoka Shirika la Muntada Aid Kabir
Miah alisema kupitia mradi wa Little Heart unaotoa huduma mbalimbali zikiwemo
huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto wameweza kuwafanyia upasuaji wa moyo zaidi
ya watoto 3000 kutoka maeneo mbalimbali duniani.
“Kupitia mradi wetu wa Little Heart tumefanya kambi za
matibabu ya moyo zaidi ya 40 katika nchi 9 ambapo kwa hapa Tanzania hii ni mara
yetu ya sita kuweka kambi ya matibabu ya moyo kwa watoto na jumla
tumeshawafanyia upasuaji wa moyo watoto 416 tangu mwaka 2015 tulipoanza
kushirikiana na Taasisi hii,”.
“Tunafurahi kushirikiana na wataalamu wa JKCI lakini pia tunawashukuru
madaktari ambao wamekuwa wakijitolea kufanya kazi na shirika la Muntada Aid
kutoka maeneo mbalimbali duniani lengo likiwa moja la kurejesha afya kwa watoto
wetu ambao wanahitaji huduma ya matibabu ya moyo,” alisema Kabir.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete Godwin Sharau alisema kila mwaka huduma za upasuaji zimekuwa
zikiimarika kutokana na ujuzi ambao wamekuwa wakiupata kupitia kambi mbalimbali za matibabu
zinazofanyika katika Taasisi hiyo.
“Ujuzi tunaopata kutoka kwa madaktari wenzetu unaongeza pia
idadi ya watoto na watu wazima tunaowafanyia upasuaji wa moyo, mfano mwaka 2021
tulifanikiwa kufanya upasuji wa kufungua kifua kwa watoto 250 lakini kwa mwaka
huu 2022 hadi sasa tupo mwezi wa kumi tumeshawafanyia upasuaji wa kufungua kifua
watoto 230,”.
Kuhusu upatikanaji wa huduma za matibabu ya moyo Dkt. Godwin
alisema kwa viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO) inapaswa kuwa na taasisi
moja ya matibabu na upasuaji wa moyo ambayo itakuwa inatoa huduma kwa watu
milioni 3 tu.
“Ukiangalia Tanzania sasa ina watu zaidi ya milioni 50 hii
inamaanisha kwamba inahitaji kuwa na taasisi 20 za kutoa huduma za matibabu na
upasuaji wa moyo ili kuweza kukidhi mahitaji ya watu wanaozaliwa na matatizo ya
moyo na kuhitaji huduma za matibabu hayo.
“Kutipita Taasisi yetu tumeweza kuzalisha wataalamu ambao ni mbegu tunayotaka kuisambaza Tanzania nzima ili huduma za matibabu na upasuaji wa moyo ziweze kufika katika mikoa yetu na kupunguza idadi ya watoto wanaohitaji huduma za matibabu ya moyo”, alisema Dkt. Godwin.
Comments
Post a Comment