Watoto 40 wafanyiwa upasuaji wa moyo: Serikali yaokoa shilingi bilioni moja
Wataalam wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la
Mending Kids la nchini Marekani wakifanya upasuaji mdogo wa moyo kwa kutumia
mtambo wa Cathlab kuziba tundu la moyo wa mtoto katika kambi maalum ya matibabu
ya moyo ya siku tano iliyomalizika jana katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar Es Salaam.
Wataalam wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Mending Kids la nchini Marekani wakiangalia kifaa alichowekewa mtoto kwenye moyo kama kimeka sawa kwa kutumia mashine ya Trans esophageal ECHO wakati wa kambi maalum ya matibabu ya moyo ya siku tano iliyomalizika jana katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar Es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwashukuru wataalam kutoka Shirika la Mending Kids la nchini Marekani kwa kutoa msaada wa vifaa vya matibabu ya moyo kwa watoto wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu kambi ya matiababu ya moyo iliyofanywa na wataalam hao na kumalizika jana katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar Es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mending Kids la nchini Marekani Isabelle Fox akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu kambi maalum ya matibabu ya moyo iliyomalizika jana ambapo watoto 40 walifanyiwa upasuaji wa kufungua na bila kufungua kifua wa moyo.
Baadhi ya wataalam wa afya kutoka Shirika la Mending Kids la nchini Marekani wakifuatilia mkutano na waandishi wa habari kuhusu kambi maalum ya matibabu ya moyo iliyofanywa na wataalam wa JKCI kwa kushirikiana na wataalam hao iliyomalizika jana jijini Dar Es Salaam.
Picha na Khamis Mussa
*******************************************************************************************************************************************************************************************
Watoto 40 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu wamefanyiwa upasuaji kwenye kambi maalum ya matibabu iliyomalizika jana katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Kambi hiyo ya siku tano ilifanywa na wataalamu wa magonjwa ya
moyo kwa watoto wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Mending
Kids la nchini Marekani.
Kwa watoto hawa kufanyiwa upasuaji huu hapa nchini Serikali
imeweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni moja fedha ambazo zingelipwa kama
upasuaji huo ungefanyika nje ya nchi.
Akizunguma za waandishi wa habari jana jijini Dar Es Salaam Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema
kati ya watoto 40 waliofanyiwa upasuaji 20 walifanyiwa upasuaji wa kufungua
kifua na 20 walifanyiwa upasuaji kwa njia ya tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab.
Dkt. Kisenge alisema tangu waanze kushirikiana na shirika
hilo la Mending Kids jumla ya kambi sita za matibabu ya moyo kwa watoto zimeshafanywa
huku wataalamu wa JKCI wakifundishwa njia mbalimbali za kufanya upasuaji wa
kufungua kifua na ule wa tundu dogo kwa utaalam zaidi.
“Kupitia Shirika la Mending Kids wataalam wa JKCI wa upasuaji
wa moyo kwa watoto wamekuwa mabingwa wabobezi katika kutoa huduma za upasuaji
wa moyo kwa watoto wenye magonjwa ya moyo hivyo kutufanya kuwa mabingwa kusini
mwa jangwa la Sahara katika kutoa huduma bora za matibabu ya moyo kwa watoto,”
alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge pia alisema shirika la Mending Kids limetoa
msaada wa vifaa vya matibabu katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete vyenye
gharama ya dola za kimarekani milioni 1.2 ikiwa ni sehemu ya kusaidia watoto
wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa upasuaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema kwa mara ya kwanza tangu
waanze kufanya upasuaji wa moyo hapa nchini ameweza kufanya upasuaji maalum
(hybrid procedure) unaohusisha upasuaji wa aina mbili (kwa wakati mmoja) ule
wa kufungua kifua na upasuaji wa tundu dogo kwa kufungua kidogo kifua na
kumpatia mtoto matibabu ya upasujai wa tundu dogo.
Dkt. Angela alisema wataalam wa upasuaji walifungua kifua
kidogo na kuwafanyia upasuaji wa tundu dogo watoto wawili ambapo mtoto mmoja alifanyiwa
upasuaji huo katika chumba cha upasuaji
mkubwa wa moyo (theater) na mwingine kufanyiwa upasuaji huo katika chumba cha
upasuaji wa tundu dogo (Cathlab).
“Mtoto aliyefanyiwa upasuaji katika chumba cha upasuji mkubwa
wa moyo tulimfungua kifua kidogo kwasababu mishipa yake jinsi ilivyokuwa
haikuwezekana kupitisha kifaa kwa tundu dogo hivyo kifua chake kufunguliwa
kidogo na wataalam wanaofanya upasuaji kwa tundu dogo wakapitisha waya kwenye
mishipa ya moyo na kuweka kifaa cha kuziba tundu la moyo,”.
“Katika upasuaji huo mtoto amezibwa tundu la moyo lakini sio
kwa kushonwa kama ambavyo tungefanya upasuaji mkubwa wa moyo ambapo tungeshona
tundu hilo ili liweze kufunga,” alisema Dkt. Angela.
Dkt. Angela alisema katika kambi hiyo pia walifanikiwa kufanya
upasuaji wa aina hiyo kwa mgonjwa ambaye ana muunganiko wa mirija mikubwa ya
mshipa wa moyo unayotoa damu kwenye moyo kupeleka kwenye mwili na ule
unaopeleka damu kwenye mapafu kuingiliana.
“Kawaida hii mishipa huwa haiingiliani kwasababu damu lazima
iingie kwenye moyo izunguke kutoka upande wa kulia iende upande wa kushoto ndiyo
hiyo mishipa inavyofanya kazi lakini kwa mtoto huyu amezaliwa akiwa na
muingiliano kati ya mishipa hiyo miwili hivyo kuisababishia damu kutoka kwenye
moyo kwenda kwenye mapafu”,.
“Changamoto kubwa aliyokuwa anaipata mtoto huyo damu iliyokuwa inatoka kwenye moyo
kwenda kwenye mapafu ilikuwa na msukumo mkubwa hivyo kumsababishia kupata homa
ya mapafu mara kwa mara na kuwa na tatizo la kushindwa kupumua,”alisema
Dkt.Angela.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mending Kids Isabelle
Fox alisema anafurahi kuona utaalamu wa wataalam wa JKCI umekuwa ukiongozeka
kila siku ambapo kwa sasa wanaweza
kufanya upasuaji wa aina mbalimbali wa moyo tofauti na walivyoanza kushirikiana
mwaka 2015.
“Katika kambi hii pamoja na kufanya upasuaji wa moyo tumekuwa
tukitoa mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo wataalamu wa Taasisi hii ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kuokoa maisha ya
watoto wenye matatizo ya moyo ili waweze kuendelea na maisha kama watoto
wengine na kuwarejeshea tabasamu”, alisema Isabelle.
Comments
Post a Comment