JKCI yaanzisha kliniki ya jioni
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wagonjwa wanaotibiwa katika
Taasisi hiyo kuhusu Kliniki mpya ya matibabu ya moyo inayoanza saa kumi jioni
hadi saa mbili usiku aliyoizundua jana jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wagonjwa wanaotibiwa katika
Taasisi hiyo kuhusu Kliniki mpya ya matibabu ya moyo inayoanza saa kumi jioni
hadi saa mbili usiku aliyoizundua jana jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpima shinikizo la damu na kiwango cha oksijeni kwenye damu mgonjwa aliyehudhuria kliniki mpya ya matibabu ya moyo inayoanza saa kumi jioni hadi saa mbili usiku wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Henry Mayala akiwaeleza wagonjwa waliohudhuria kliniki ya jioni inayoanza saa kumi jioni hadi saa mbili usiku kuwa huduma za vipimo vya magonjwa ya moyo vitakuwa vinapatikana katika kliniki hiyo.
Picha na Khamis Mussa
*********************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeanzisha
kliniki ya matibabu ya moyo inayoanza saa kumi jioni hadi saa mbili usiku ili
kutoa nafasi kwa wagonjwa walioshindwa kufika kliniki za asubini kupata huduma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo jana jijini
Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
alisema kuanzishwa kwa kliniki hiyo kumelenga kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa wanaotibiwa katika
Taasisi hiyo.
Dkt. Kisenge alisema kuna wagonjwa ambao wanashughuli nyingi
wakati wa asubuhi na pia baadhi ya wazee wanashindwa kuamka alfajiri kwa ajili
ya kuwahi kliniki lakini kuwepo kwa
kliniki ya jioni kutawasaidia wagonjwa wote kupata muda wa kuhudhuria kliniki
zao.
“Tumeanzisha Kliniki mpya ya matibabu ya moyo ambayo itakuwa
inaanza saa kumi hadi saa mbili usiku lengo likiwa ni kuwasaidia wagonjwa ambao
wanataka kupata huduma za matibabu ya moyo wakati wa jioni,”.
“Taasisi yetu imekuwa ikipata wagonjwa takribani 400 kila
siku na wengine wengi wanahitaji kupata huduma za matibabu lakini hawapati
kwasababu wanakosa muda na nafasi ya kutibiwa katika siku husika, hivyo basi tumeona
tuendelee kuimarisha huduma na
kuwasaidia hasa wazee ambao wanashindwa kuamka asubuhi na kuwahi kliniki,”
alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema kuwepo kwa kliniki ya jioni kutatoa
fursa kwa wagonjwa wa moyo ambao wanafanya kazi za kuajiriwa kwani watapata
nafasi ya kwenda kazini na baada ya majukumu yao ya kazi watafika katika taasisi hiyo kwa ajili ya kupatiwa huduma katika kliniki ya jioni.
“Tunaendelea kuboresha huduma zetu na sasa tutakuwa
tunawafuata wananchi mahali walipo ambapo tumejipanga kuzunguka zaidi ya mikoa
15 ili tuweze kuwapatia huduma za matibabu ya moyo na kutoa elimu kwa madaktari
walioko mikoani ili na wao waweze kuwabaini na kuwapatia huduma wagonjwa wetu
moyo”, alisema Dkt. Kisenge.
Akizungumzia kuhusu kliniki hiyo Daktari bingwa wa magonjwa
ya moyo aliyebobea katika kutoa huduma za vipimo vya moyo Henry Mayala alisema kliniki
hiyo ya jioni itatoa fursa pia kwa wagonjwa hao kufanyiwa vipimo vya magonjwa
ya moyo.
“Siku za nyuma vipimo vya magonjwa ya moyo vilikuwa
vinatolewa kwa idadi na wagonjwa wengine kupewa tarehe za kurudi kwa ajili ya
vipimo husika lakini kupitia kliniki hii ya matibabu ya moyo inayoanza jioni
tutaendelea kutoa huduma za vipimo kwa wagonjwa wengi zaidi,”.
“Kupitia kliniki ya jioni iliyoanzishwa tutaenda kupunguza
msongamano wa wagonjwa wetu kwani vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya
kazi (Echocardiography-ECHO) na vipimo vya kuangalia mfumo wa umeme wa moyo
unavyofanya kazi (Electrocardiography-ECG) vitakuwepo kuanzia asubuhi hadi saa
mbili usiku,” alisema Dkt. Mayala.
Kwa upande wa wagonjwa waliohudhuria kliniki hiyo walishukuru
kwa kuanzishwa kwa huduma ya kliniki ya jioni ambayo inatoa nafasi kwa wagonjwa
wengi zaidi kupata nafasi ya kutibiwa.
“Ninaushukuru uongozi wa JKCI kwa kuanzisha kliniki ya jioni
kwani kwa kupitia kliniki hii kutarahisisha upatikanaji wa matibabu hasa kwa
watu wazima ambao kuamka asubuhi ni changamoto,”.
“Hapo awali ilitulazimu kufika JKCI alfajiri lakini kutokana
na idadi ya wagonjwa kuwa wengi tulijikuta tunakaa hadi jioni lakini kupitia
kliniki hii ya jioni tutakuwa tunakuja mchana kupata huduma bila msongamano na
kurejea nyumbani kwa wakati,” alisema Omary Chudi.
Halima Mbaga anayetibiwa katika Taasisi hiyo alisema kliniki
ya jioni ya matibabu ya moyo inawapa fursa wagonjwa wa moyo kufika JKCI wakati
wowote kwa ajili ya kupatiwa huduma za matibabu na vipimo vya magonjwa ya moyo.
Comments
Post a Comment