Watu 1233 wafanyiwa upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo mkoani Arusha
Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) na wenzao wa Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) wakiwa katika
picha ya pamoja jana mara baada ya kumalizika kwa kambi maalum ya siku tano ya uchunguzi
na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wakazi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani. Jumla
ya watu 1233 wakiwemo watoto na watu wazima walifanyiwa uchunguzi katika kambi
hiyo iliyoanza tarehe 26 hadi 30/09/2022.
**************************************************************************************************************************************************************************************
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Jumla ya watu 1233 wamefanyiwa upimaji na matibabu ya moyo katika kambi maalum ya matibabu iliyofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC).
Kambi
hiyo ya matibabu ya moyo iliyofanyika kwa siku tano ilianza tarehe 26 hadi
30/09/2022 ambapo watu wazima pamoja na watoto walipata matibabu. Kambi hii ilikuwa ni maalum kwa ajili ya kuadhimisha siku ya moyo duniani iliyofanyika tarehe
29/09/2022.
Kwa
upande wa watu wazima waliofanyiwa upimaji wengi wao walikutwa na matatizo ya
shinikizo la juu la damu, kutanuka kwa moyo, kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo
na shida za valvu za moyo.
Watoto
70 walifanyiwa uchunguzi ambapo wengine walikutwa na matatizo ya moyo ya
kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika
mpangilio wake pamoja na valvu za moyo kuwa na shida.
Wagonjwa wengine kwa mara
ya kwanza wamegundulika kuwa na matatizo ya moyo ikiwa ni pamoja na kutanuka na
kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo ambapo asilimia 5 tumewapa rufaa ya kuja
kufanyiwa vipimo zaidi na kutibiwa katika Taasisi yetu.
Kwa
upande wa watoto wenye matatizo tumewaelekeza kuja JKCI ili waweze kufanyiwa
upasuaji katika kambi maalum za upasuaji wa moyo kwa watoto zitakazoanza tarehe
10/10/2022 na wengine watahudhuria kliniki zetu kwa ajili ya matibabu na kuwafuatilia kwa ukaribu zaidi.
Katika kambi hii wananchi walipimwa
vipimo mbalimbali vya moyo ikiwa ni pamoja na urefu, uzito, kiwango cha sukari
mwilini, kuangalia uwiano baina ya urefu na uzito, kipimo cha kuangalia jinsi
moyo unavyofanya kazi (Echocardiography), mfumo wa umeme wa moyo
(Electrocardiography) pamoja na vipimo vya damu (utendaji kazi wa figo, ini na
kiwango cha mafuta kwenye damu).
Tulikuwa na wataalamu wa
lishe ambao walitoa elimu ya lishe bora ambayo iliwapa wananchi kuwa na uelewa wa
kufuata mtindo bora wa maisha ambao utawasaidia kuepukana na magonjwa ya
moyo ambayo ni moja ya magonjwa yasiyoambukiza na mtu anaweza kuyaepuka kwa
kufuata ushauri wa kitaalamu.
Wananchi waliopata huduma za matibabu walitoka katika
mikoa ya Arusha, Shinyanga, Singida, Mara, Kagera, Morogoro, Tanga, Manyara,
Kilimanjaro na Iringa. Tumeona kuna uhitaji mkubwa wa huduma za kibingwa za
matibabu ya moyo hiyo basi Taasisi yetu itaendelea kuwasogezea wananchi huduma hizi
kwa kuwafuata mahali walipo.
Pia tutawajengea uwezo
wataalamu wa afya wa jinsi ya kutambua na kutibu magonjwa ya moyo kwani
Serikali imenunua mashine za kisasa za kuchunguza moyo na kuzisambaza katika
Hospitali mbalimbali hapa nchini.
Tunawaomba wananchi muepuke tabia hatarishi zinazoweza kuharibu mioyo yenu hii ikiwa ni pamoja na uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe uliokithiri. Zingatieni mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi na kula vyakula bora.
“Tunajali Afya ya Moyo Wako”.
Imetolewa na :
Anna Nkinda
Mkuu wa Kitengo
cha Uhusiano na Mawasiliano
Comments
Post a Comment