JKCI kuzifikia hospitali 15; kuwatafuta watoto wenye matatizo ya moyo
Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa
watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao
wa shirika la Little Heart la nchini Saudi Arabia ambalo ni moja ya mradi
wa Afya ulioko ndani ya Taasisi ya Msaada ya Muntada yenye makao yake makuu jijini
London nchini Uingereza wakimfanyia
upasuaji wa kurekebisha mishipa ya damu mtoto ambaye mishipa yake ya damu ilikuwa
inarudisha damu safi kutoka kwenye mapafu kwenda kwenye moyo upande wa kulia
badala ya kupeleka damu hiyo upande wa kushoto wa moyo wakati wa kambi maalum
ya ya upasuaji wa moyokwa watoto inayofanyika JKCI.
Picha na Khamisi Mussa
**************************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imejipanga kuzifikia hospitali 15 zilizopo pembezoni mwa nchi kwa ajili ya kufanya uchunguzi na matibabu kwa watoto wenye matatizo ya moyo ambao wakati mwingine wanaweza kupoteza maisha kutokana na kukosa huduma sahihi na kwa wakati.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
kambi maalum ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanyika JKCI.
Dkt.Kisenge alisema watoto wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa
nayo; matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake kama
wataweza kugundulika mapema na kupata huduma sahihi na kwa wakati wanapona na
kuendelea na maisha kama watoto wengine.
“Tumejipanga kuendelea kutoa huduma za kibingwa kwa kuwafuata
wananchi mahali walipo kwa kufanya hivyo tunawagundua wagonjwa wengi wenye
matatizo ya moyo ambao baada ya
kuwafanyia upimaji tunawapa rufaa ya kuja kutibiwa JKCI na hivyo kupata huduma za matibabu kwa wakati”, alisema Dkt.
Kisenge.
Kuhusu kambi hiyo ya
ya upasuaji wa moyo kwa watoto alisema inayofanywa na wataalamu wa JKCI kwa
kushirikiana na wenzao kutoka shirika la Little Heart la nchini Saudi
Arabia ambao ni moja ya mradi wa Afya ulioko ndani ya Taasisi ya Msaada ya
Muntada yenye makao yake makuu jijini London nchini Uingereza.
“Wenzetu hawa kutoka shirika la Little Heart walipofika kwetu
mwaka 2015 wakati ambao uwezo wetu wa kutibu magonjwa ya moyo kwa watoto ulikuwa
bado uko chini lakini wao waliweza kutusaidia kututoa pale tulipokuwa hadi sasa
tunaweza kufanya upasuaji wa moyo wa aina mbalimbali kwa watoto wetu,”.
“Tutaendeleza mashirikiano haya ili taasisi yetu iendelee
kuwa taasisi bora Afrika Mashariki na Kusini mwa jangwa la Sahara lakini pia
tutahakikisha madaktari wetu wanapata ujuzi wa kutosha, tukiwa na lengo la
kutoa huduma bora kwa watoto wetu wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo,” alisema
Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Naiz Majani alisema shirika la Little Heart
ambalo linatoa misaada kwa ajili ya upasuaji wa moyo kwa watoto lilikuwa kundi
la kwanza la madaktari bingwa wa moyo kutoka nje ya nchi kwenda kufanya kambi
za matibabu ya moyo kwa watoto wakati taasisi hiyo inaanzishwa.
Dkt. Naiz ambaye pia ni Mkuu wa kitengo cha kudhibiti na kuhakiki
ubora wa huduma alisema Shirika hilo limekuwa likifanya upasuaji wa moyo kwa
watoto wengi kwa kipindi cha wiki moja jambo ambalo limekuwa ni la tofauti
ukilinganisha na upasuaji wa moyo unaofanywa na wataalam wengine.
“Shirika la Little
Heart lilipokuja kwa mara ya kwanza mwaka 2015 liliwashangaza watu kwani kwa
kipindi cha siku saba waliweza kuwafanyia upasuaji wa moyo watoto 64. Hii ni
mara yao ya sita toka walipoanza kuja hapa na wamekuwa wakiendelea kufanya
upasuaji wa moyo kwa watoto kwa idadi kubwa kwa kipindi kifupi kwa miaka yote
ambayo wamekuwa wakitutembelea,”.
“Mpaka sasa wataalamu wa Shirika la Little Heart wameweza
kufanya upasuaji wa moyo kwa kushirikiana na madaktari wa JKCI kwa watoto 352.
Ujio wa mabingwa hawa kwa mara ya kwanza walikuja wataalam 32 lakini ujio wao
wa sasa wamekuja wataalam 12 hii inaonyesha kuwa uwezo wa ndani wa JKCI
umeongezeka”,alisema Dkt. Naiz.
Naye Meneja kutoka Shirika la Little Heart Kabir Miah alisema
shirika hilo linatoa huduma za upasuaji
wa moyo kwa watoto wenye magonjwa ya moyo katika nchi mbalimbali zikiwemo nchi
zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara na Afrika.
“Hii ni mara yetu ya
sita kufika katika Taasisi hii kwa ajili ya kushirikiana na wataalam wa JKCI
kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto, kambi yetu ya kwanza ya mwaka 2015
tuliwafanyia upasuaji watoto 64, kambi ya pili mwaka 2016 tuliwafanyia upasuaji
watoto 73”,.
“Kambi ya tatu mwaka 2017 tuliwafanyia upasuaji watoto 50,
mwaka huo huo 2017 tulikuja mara ya pili Desemba na kuwafanyia upasuaji watoto
92, kambi ya tano ya mwaka 2018 tuliwafanyia upasuaji wa moyo watoto 73, na
sasa kambi yetu ya sita tunatarajia kuwafanyia upasuaji wa moyo watoto 70”,.
“Tokea ujio wetu wa kwanza hapa JKCI hadi sasa tumeona
mafanikio makubwa kwa wataalam waliopo hapa kwani mwaka 2015 upasuaji wa moyo
kupitia tundu dogo kwenye paja kwa watoto ulikuwa haufanyiki lakini sasa hivi wataalam
hawa wanafanya upasuaji huo,” alisema Kabir.
Kabir alisema wataalam kutoka shirika la Little Heart wataendelea kushirikiana na JKCI
katika kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto ikiwa ni sehemu ya msaada
kama ambavyo mradi wa Afya ulioko ndani ya Taasisi ya Msaada ya Muntada unavyolenga kuwasaidi watoto wanaosumbuliwa na
magonjwa ya moyo na kuwarejeshea matumaini ya kuishi.
Wataalamu walioko katika kambi hiyo walianza kufanya upasuaji
tarehe 09/10/2020 na watamaliza tarehe 14/10/2022
ambapo pamoja na kutoa huduma kwa wagonjwa pia kuna mafunzo mbalimbali
yanayofanyika ikiwa ni pamoja na kubadilishana ujuzi wa kazi.
Comments
Post a Comment