Wataalamu wa afya 65 wafundishwa jinsi ya kuwahudumia wagonjwa mahututi na wanaohitaji uangalizi maalum

 

Wataalamu wa Afya kutoka Shirika la Cardiostart International la nchini Marekani wakiwafundisha washiriki wa mafunzo ya siku tatu ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi namna ya kutumia mashine ya cardiac monitor kuangalia mwenendo wa mapigo ya moyo na oksijeni mwilini wakati wa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kuhudhuriwa na wauguzi na madaktari kutoka hospitali mbalimbali nchini.

Daktari bingwa wa moyo kutoka Shirika la Cardiostart International la nchini Marekani Donato Sisto akiwawafundisha washiriki wa mafunzo ya siku tatu ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa wagonjwa hao wakati wa mafunzo ya siku tatu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kuhudhuriwa na wauguzi na madaktari kutoka hospitali mbalimbali nchini.

Wataalamu wa Afya walioshiriki mafunzo ya siku tatu ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi wakijifunza namna ya kutumia mashine ya cardiac monitor kuangalia mwenendo wa mapigo ya moyo na oksijeni mwilini wakati wa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kuhudhuriwa na wauguzi na madaktari kutoka hospitali mbalimbali nchini.

Daktari bingwa wa moyo kutoka Shirika la Cardiostart International la nchini Marekani Michael Schupp akiwafundisha washiriki wa mafunzo ya siku tatu ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa wagonjwa hao wakati wa mafunzo ya siku tatu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kuhudhuriwa na wauguzi na madaktari kutoka hospitali mbalimbali nchini.


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na Daktari bingwa wa wagonjwa wanaohitaji huduma ya dharura na mahututi kutoka Shirika la Cardiostart International la nchini Marekani Richard Harper wakati wa mafunzo ya siku tatu ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi ya namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa wagonjwa hao Jana katika Ukumbi wa Taasisi hiyo Jjijini Dar es Salaam.

Picha na Khamis Mussa

*****************************************************************************************************************************************************************************************************

Wataalamu wa Afya 65 kutoka hospitali mbalimbali hapa nchini wanashiriki mafunzo ya kuwahudumia wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum na mahututi yanayotolelewa na madaktari bingwa wa Moyo kutoka Shirika la Cardiostart International la nchini Marekani.

Mafunzo hayo ya siku tatu yameandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo yamehusisha mafunzo ya kutumia vifaa mbalimbali vya matibabu vinavyotumika katika kutoa huduma kwa wagonjwa wanaohitaji huduma maalum na mahututi.

Akizungumza na vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Peter Kisenge alisema JKCI imeona umuhimu wa wataalam wa afya kupata mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa mahututi kwasababu wagonjwa hao wako katika hali ya kuumwa sana na ni rahisi kwao kupoteza maisha ghafla kama hawatapata huduma vizuri.

“Wagonjwa wetu wengi wanakuja wakiwa katika hali mbaya hivyo mafunzo haya kwetu sisi ni ya muhimu kwani wagonjwa mahututi wasipohudumiwa vizuri na kwa haraka wanaweza wakapoteza maisha yao,”.

“Tumewaalika wataalamu mabingwa wa moyo kutoka nchini Marekani ambao kwa siku tatu watawapa wataalamu wetu uwezo na ujuzi wa hali ya juu na baada ya mafunzo haya watalamu wetu watapeleka utaalam huo kwa wenzao ambao hawakupata nafasi ya kushiriki mafunzo haya,” alisema Dkt. Kisenge.

Aidha Dkt. Kisenge alisema Serikali ya awamu ya sita imewekeza kwa kiasi kikubwa katika vifaa tiba kwenye vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICU) hivyo kupitia mafunzo hayo wataalamu wa afya watapata pia nafasi ya kufundishwa namna ya kutumia mashine hizo na kuzitunza kwa maslahi ya nchi.

“Mafunzo haya yanaenda kuwa endelevu hapa kwetu kwani kila baada ya miezi mitatu wataalam wetu watapata mafunzo ya kuwahudumia wagonjwa mahututi na namna ya kutumia mashine za kuwahudumia wagonjwa hao ili kwa pamoja tutoe huduma bora na kulinda vifaa vyetu vya matibabu,” alisema Dkt. Kisenge.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dkt. Angela Muhozya alisema JKCI imeamua kuanzisha mafunzo hayo baada ya kuona uhitaji mkubwa uliopo nchini katika kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi.

“Tumedhamiria baada ya mafunzo haya wataalam wetu wataenda kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi katika kiwango cha ufanisi mkubwa zaidi na kupunguza vifo vinavyotokea kwa wagonjwa hao”, alisema Dkt. Angela.

Dkt. Angela ambaye pia ni mratibu wa mafunzo hayo alisema JKCI ni mdau mkubwa katika eneo la kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi kwani wagonjwa wengi wa moyo wanaofika katika Taasisi hiyo wanakuwa katika hali mbaya lakini pia wagonjwa wa moyo wanaofanyiwa upasuaji wa moyo huwa katika hali ya umahututi hivyo uhitaji kupatiwa huduma hizo.

“Tupo na wataalam wabobezi wa magonjwa ya dharura na mahututi ambao wanatupa mafunzo kwa kiwango cha hali ya juu, tunaamini ndani ya siku hizi tatu wataalamu wetu walioshiriki mafunzo haya watakuwa na elimu ya ziada watakayoenda kuitumia katika maeneo yao ya kazi,” alisema Dkt. Angela. 

Akizungumzia mafunzo hayo Daktari bingwa wa wagonjwa wanaohitaji huduma ya dharura na mahututi kutoka Shirika la Cardiostart International la nchini Marekani Richard Harper alisema madaktari kutoka shirika hilo wamekwenda JKCI kwa ajili ya kuwasaidia wataalam wa afya hapa nchini ili waweze kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya tiba.

“Nimefurahi kuona wataalam wa afya walioshiriki mafunzo haya wanajitoa na kutamani kujua zaidi namna ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi, tunaenda kuwapa mafunzo ya hali ya juu ambayo yataleta mabadiliko katika kutekeleza majukumu yao,”alisema Dkt. Richard.

Naye Daktari kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) Issa Kisoma alisema amevutiwa kushiriki mafunzo hayo kwasababu katika eneo lake la kazi amekuwa akikutana na wagonjwa wanaohitaji kupatiwa huduma ya dharura hivyo kuona umuhimu wa kuongeza ujuzi katika eneo hilo.

 “Wagonjwa ninaokutana nao katika eneo langu la kazi wanahitaji kupatiwa huduma ya dharura kwa usahihi ili kuokolewa maisha yao, hivyo natamani sana nisikosee kuwapatia huduma na kupoteza maisha yao ndio maana nikaona nami nishiriki mafunzo haya ili niokoe maisha ya wagongwa ninaowahudumia,”.

“Mafunzo haya yatanisaidia pia kuongeza ubunifu, ufanisi na namna ya kuokoa maisha lakini pia kuwafundisha wataalam wenzangu ambao hawajapata nafasi ya kushiriki mafunzo haya,” alisema Dkt. Issa.

Comments

Popular posts from this blog

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024

Maabara ya JKCI yapata ithibati ya kimataifa (ISO 15189:2012)