JKCI yatafuta bilioni 1 ya upasuaji kwa watoto 500 wasio na uwezo


Kaimu mtendaji mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Heart Team Africa Foundation (HTAF) Linda Gideon akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu shirika hilo kuandaa chakula cha jioni (Dinner Gala) kwa ajili ya kuchangisha fedha za  matibabu ya moyo kwa watoto wasio na uwezo.



Mkutano wa waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya  chakula cha jioni (Dinner Gala) kwaajili ya kuchangisha fedha za  matibabu ya moyo kwa watoto wasio na uwezo ukiendelea katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).


Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya kuandaa chakula cha jioni (Dinner Gala) kwaajili ya kuchangisha fedha za matibabu ya moyo kwa watoto wasio na uwezo Dkt.  Naizihijwa Majani akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.


Mjumbe wa  Kamati ya Maandalizi ya kuandaa chakula cha jioni (Dinner Gala) kwaajili ya kuchangisha fedha za  matibabu ya moyo kwa watoto wasio na uwezo Idd Lema akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

*********************************************************************************************************************************************************************************************************************************************************

Taasisi ya  Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) inatarajia kufanya upasuaji wa  moyo kwa watoto 500 katika kipindi cha mwaka mmoja  yatakayogharimu shilingi  bilioni moja.

Fedha hizo zinatarajiwa kukusanywa Julai 6,  mwaka huu, kupitia chakula cha jioni (Dinner Gala) itakayofanyika jijini Dar es Salaam  katika Hoteli ya Johari Rotana chini ya shirika lisilo la kiserikali la Heart Team Africa Foundation (HTAF) linaloshughulika na upatikanaji wa matibabu ya moyo kwa watoto wasio na uwezo.

Akieleza kuhusu mpango huo wa kuwatibia watoto hao leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema lengo la kutoa matibabu hayo ni kuokoa maisha ya watoto waliozaliwa na mgonjwa hayo kupitia HTAF na Tasisi hiyo.

“Takwimu zinaonesha kuwa watoto wengi wanazaliwa na matatizo ya moyo kati ya watoto milioni mbili wanaozaliwa kwa mwaka 14,000 wamakuwa na matatizo ya moyo  na  watoto 4,000 wanahitaji upasuaji”, alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alieleza kwamba JKCI kwa mwaka uliopita  ilifanya upasuaji wa moyo kwa watoto  357 ambapo kwa mwaka huu wanataraji kufanya upasuaji kwa watoto 500.

Alisema kupitia shilingi bilioni  moja inayotarajiwa kukusanywa na HTAF, itawezesha kuwatibia watoto hao, hususan wale wa vijijini ambao hawana uwezo wa kugharamia huduma hizo.

Mkurugenzi huyo mtendaji Dkt. Kisenge alisema gharama za  matibabu ya moyo kwa watoto ni ghali  hadi kufikia shilingi  milioni 10 kwa mgonjwa mmoja na shilingi milioni 15 kwa upasuaji wa mtoto mmoja, huku wakiishukuru serikali na wadau mbalimbali kwa kudhamini watibabu hayo.

Dkt. Kisenge aliishukuru serikali kwani imekuwa ikifadhili matibabu ya watoto kwa sehemu kubwa, karibu asilimia 70 hadi 90, kwani walio wengi hawawezi kumudu gharama hizo.

Kaimu mtendaji mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Heart Team Africa Foundation (HTAF),Linda Gideon alisema  lengo kuu  la kuanzishwa kwa shirika hilo ni kuboresha huduma za moyo kwa jamii ndani na nje ya Tanzania.

"Pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali kuchangia matibabu kwa asilimia 70 bado kuna changamomoto ya kumalizia kiasi kilichobaki na ili kufanikisha hilo tumeandaa chakula cha jioni hoteli ya Johari Rotana tutashirikiana na jamii”.

 "Tunaomba wadau wote ambao wanawiwa kusaidia watoto wajitokeze kwa wingi kurudisha  tabasamu la watoto wenye tatizo la moyo na tutatoa account maalumu kwa watu wanaotaka kuchangia wataweka katika account hiyo”, alisema Linda.

Akielezea kuhusu Dinner Gala hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa JKCI Naizihijwa Majani alisema wamejipanga vyema kuhakikisha wanafanikisha  harambee hiyo kupitia fedha hizo za kuwatibia watoto.

Alisema kuwa katika usiku huo wa Dinner Gala, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, hivyo aliwaomba watu wajitokeze kwa wingi ambapo watatangaza utaratibu maalumu utakaotumika.

Kwa upande wake, Meriselina Athanasi ambaye ni mama mzazi wa mtoto mwenye ugonjwa wa moyo aliishukuru serikali kupitia JKCI kwa namna ambavyo imewasaidia kupata matibabu bila gharama.

Alisema kuwa, baada ya kugundua tatizo hilo kwa mtoto wake, ndugu zake walidai hawana uwezo wa kumsafirisha wala kumtibu mtoto huyo hivyo wasamalia wema walimpatia nauli ya kufika Dar es Salaam akitokea Morogoro.

“Ninamshukuru Mungu mtoto wangu baada ya kufanyiwa vipimo anaendelea vizuri sasa hivi tuko wodini anasubiria kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo, nimepewa gharama ya upasuaji ni milioni nane ”.

“Gharama ya upasuaji ni kubwa mimi peke yangu siwezi kulipia, tunaiomba Serikali na wananchi msituchoke mtusaidie kulipia gharama za matibabu ya moyo ya watoto wasiokuwa na uwezo”,  alisema Theochrista Kambi mama wa mtoto mwenye shida ya moyo.


Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari