Kwa mara ya kwanza upasuaji kwa njia ya tundo dogo wa kurekebisha mishipa ya damu iliyotanuka na kupasuka kifuani na tumboni wafanyika nchini

Wataalamu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka nchini India wakimfanyia mgonjwa  upasuaji kwa njia ya tundu dogo wa kutumia kifaa maalumu ((Stent) wa kurekebisha mshipa wa damu uliotanuka  sehemu ya kifua. Wagonjwa watano watafanyiwa upasuaji huo ambao kwa mara ya kwanza umefanyika hapa nchini kwa kutumia mtambo wa Cathlab.

 *********************************************************************************************************************************************************************************************************************Kwa mara ya kwanza wataamu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanya upasuaji kwa njia ya tundu dogo wa kurekebisha mishipa ya damu iliyotanuka na kupasuka sehemu ya kifua na tumbo kwa wagonjwa watano wenye matatizo hayo.

 Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema wagonjwa wenye matatizo hayo wengi wao walikuwa wakipoteza maisha na wale ambao walikuwa wanapona walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa nje ya nchi.

 Dk Kisenge alisema upasuaji huo umefanywa na madaktari wazawa kwa kushirikiana na madaktari kutoka India na tayari mgonjwa mmoja  alishafanyiwa upasuaji huku wengine watatu  watafanyiwa upasuaji huo leo na mmoja kesho.

 "Kwa mara ya tatu tunavunja rekodi tumefanya matibabu makubwa ya kurekebisha mishipa ya damu ambayo imetanuka na kupasuka hii ni tatizo ambalo watu wengi wanalipata na kupoteza maisha ghafla  na wanaobaki tunawapeleka nje ya nchi lakini hivi  sasa tutaanza kuwahudumia hapa nchini”,.

 "Ni upasuaji mkubwa kufanyika Tanzania na Afrika Mashariki na Kati tumevunja rekodi tunampongeza Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapenda wananchi wake na kutoa  kiasi cha shilingi milioni 900 za matibabu ya kibingwa katika Taasisi yetu,", alisema Dkt. Kisenge. 

 Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema  mishipa ya damu ya tumboni na kifuani kutanuka na kupasuka kunasabahishwa na vitu vingi ikiwemo shinikizo la juu la damu  ambayo haitibiwi vizuri,uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe uliokithiri na uzito mkubwa.

 Dkt. Kisenge alisema katika Taasisi hiyo kuna wagonjwa wapatao 30 wanaosubiri kupata matibabu hayo ambapo gharama zake ni shilingi milioni 80 endapo mgonjwa atatibiwa hapa nchini na milioni 150 akitibiwa nje ya  nchi.

"Tutaendelea kutoa matibabu haya na tutaendelea kuwa na matibabu mapya mengine kwani wataalamu wetu wanajifunza kila siku. Upasuaji huu tulioufanya ukifanyika kwa njia ya kufungua kifua unachukua saa nane ila kwa njia ya tundu dogo ni saa mbili hii ni njia nzuri japo gharama ni kubwa ila Mhe. Rais wetu ametoa  fedha ili wananchi wasaidiwe”, alisema Dkt.Kisenge.

Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka nchini India Gireesh Warawdekar alisema upasuaji huo unaenda sambamba na mafunzo wanayoyatoa kwa wataalamu wa JKCI ili nao waweze kuwahudumia wananchi wenye shida za mishipa ya tumbo na kifua.

“Aina hii ya upasuaji ambao tunaufanya kwa njia ya tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab ni upasuaji mgumu lakini ni mzuri kwani hautumii muda mwingi kuufanya pia mgonjwa anayetibiwa anakaa muda mfupi hospitali na hapiti katika kipindi kigumu cha maumivu kama ilivyo kwa upasuaji wa kufungua kifua”, alisema Dkt. Warawdekar.

 Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema walikuwa hawana  utaalamu wala vifaa vya kuwezesha kufanyika kwa upasuaji huo lakini kwa uwekezaji uliofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wameweza kufanikisha hilo.

"Wataalmu hawa wa kutoka nchini India wapo na ujuzi mkubwa ambao wanatufundisha sisi,  tunatumia mashine zetu wao wamekuja na kifaa chenye gharama kubwa kinachotengenezwa ambacho kinatumika katika upasuaji, nasi tunaelekea huko kutengeneza wataalamu watakaofanya upasuaji wa aina hii”, alisema Dkt. Angela.

Naye Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo  na mishipa ya damu  wa JKCI Alex Joseph alishukuru ujio wa madaktari hao kutoka nchini India kwani wamefanikiwa kumfanyia upasuaji mzee wa miaka 66.

"Tulichukua saa mbili kufanyia upasuaji tulifanikiwa kwa kumuwekea kifaa maalumu (Stent) sasa hivi mgonjwa yuko vizuri ameamka na anaweza kutembea kesho anarudi kwake na upasuji wa awali wa kupasua tumbo na kifua ulikuwa na hatari kubwa ya kifo ila huu wa sasa ni salama zaidi”, alisema Dkt. Alex.

Mmoja wa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji huo kutoka Zanzibar Ali Suleiman alisema alipata matatizo ya moyo na  baada ya uchunguzi katika Hospitali ya Mnazi mmoja alibainika kuwa na matatizo ya mishipa ya damu na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI.

"Nimefika hapa Januari 1,2024 kulikuwa na changamoto nyingi hadi leo nimefanyiwa upasuaji,  ni upasuaji mzuri kwangu nawashukuru sana madaktari wote walionifanyia upasuaji kwa usalama najisiki nina nguvu na naweza kutembea kwa miguu “.

Ninawasihi wenzangu wenye matatizo kama haya wasihangaike kwenda kutibiwa nje ya nchi waje hapa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) watatibiwa mimi nimefanyiwa upasuaji jana usiku na kama unavyoniona niko vizuri tofauti na kabla sijafanyiwa”,  alisema Mzee Suleiman.

Wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji ni wale wenye shida za mishipa ya damu kutanuka, kupasuka kwa mishipa ya damu na kuziba kwa mishipa (Aortic Aneurysm, Dissection, Peripheral artery disease).


Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari