Watoto 60 kufanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya matibabu

Wataalamu wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka mradi wa Little Heart wa Shirika la Muntada Aid lenye makao yake makuu mjini London nchini Uingereza wakimfanyia mtoto upasuaji mdogo wa kuzibua mshipa wa damu wa moyo ulioziba katika kambi maalumu ya matibabu ya siku nane inayofanyika JKCI.

Wataalamu wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka mradi wa Little Heart wa Shirika la Muntada Aid lenye makao yake makuu mjini London nchini Uingereza wakimfanyia mtoto upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua na kuziba tundu la moyo  katika kambi maalumu ya matibabu ya siku nane inayofanyika JKCI.

*********************************************************************************************************************************************************************************************************

 Watoto 60 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu kutokukaa katika mpangilio wake wanatarajia kufanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya matibabu inayofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Kambi hiyo ya upasuaji mkubwa na mdogo wa moyo ya siku nane inafanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na  wenzao kutoka mradi wa Little Heart wa Shirika la Muntada Aid lenye makao yake makuu mjini London nchini Uingereza.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam kuhusu kambi hiyo Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Sulende Kubhoja alisema katika kambi hiyo watoto wanafanyiwa uchunguzi, ambao wanakutwa na matatizo yanayohitaji kufanyiwa upasuaji wanafanyiwa upasuaji mdogo wa moyo kwa njia ya tundu dogo kupitia mtambo wa Cathlab pamoja na upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua  kifua.

 “Tunawaomba wazazi wenye watoto wanaosumbuliwa na matatizo ya moyo yakiwemo matundu, mishipa ya damu na valvu za moyo (PDA, ASD, VSD for device closure na PS) wawalete katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi na kupata matibabu”.

“Pia tunawaomba madaktari kutoka Hospitali zote nchini kuwapa rufaa watoto wenye matatizo hayo ili waje JKCI kwaajili ya kupata huduma za matibabu”, alisema Dkt. Kubhoja ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji  Dkt. Angela Muhozya, Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo wa JKCI Alex Joseph alisema wanatarajia kufanya upasuaji  mkubwa wa kufungua kifua kwa watoto 20 .

“Mgonjwa anayefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo anahitaji damu nyingi, tunashukuru tuna damu ya kutosha kwaajli ya watoto wanaofanyiwa upasuaji, tunawaomba wananchi muendelee kuchangia damu kwaajili ya watoto wetu wanaofanyiwa upasuaji wa moyo”, alisema Dkt. Alex.

Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela alisema katika kambi hiyo watoto 40 watafanyiwa upasuaji mdogo wa moyo kwa njia ya tundu dogo kupitia mtambo wa Cathlab.

“Katika upasuaji huu mdogo wa moyo tunatumia mtambo wa Cathlab ambao ni maabara maalumu inayotumia mionzi kwaajili ya kufanya  uchunguzi na matibabu ya moyo, matibabu tunayoyatoa ni ya kuziba matundu ya moyo pamoja na kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba”, alisema Dkt. Stella.

Naye Meneja wa miradi wa Shirika la Muntada Aid Kabir Miah alisema Shirika hilo lina miradi mingi ikiwemo ya afya, elimu na maji na linafanya kazi katika nchi mbalimbali duniani ambapo katika bara la Afrika linafanya kazi katika nchi 30 ikiwemo Tanzania.

“Hii ni mara ya tisa tunakuja Tanzania kuwasaidia watoto wenye matatizo ya moyo na tumeshafanya upasuaji kwa watoto 475,tunafurahi kuona tumeweza kuokoa maisha ya watoto ambao baada ya kupona wameweza kuendelea na maisha yao kama watoto wengine ambao hawakuzaliwa na matatizo ya moyo”, alisema Kabir. 


Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari