Wengi wafaidika na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo

Fundi sanifu wa moyo (Cardiovascular technologist) wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jasmine Keria akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography - ECHO) mkazi wa Iringa aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH) wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya upimaji inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa IRRH.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Grace Sanga akimpima sukari kwenye damu mwananchi wa Iringa aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH) wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya upimaji inayofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa IRRH.

Afisa Uuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH) Mary Lyimo akimpima kipimo cha kuangalia shinikizo la damu mwilini (BP) mwananchi wa Iringa aliyefika katika Hospitali hiyo wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya upimaji inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa IRRH.

Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Iringa wakisubiri kupatiwa huduma wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo iliyoanza leo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH).

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallangyo akizungumza na waandishi wa habari leo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo ya siku tano ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH).

Wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH) wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kwa kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo ya siku tano ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba iliyoanza leo katika Hospitali ya IRRH.

Picha na: Khamis Mussa

*************************************************************************************************************** 

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imesogeza huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa wananchi kupitia kambi maalumu za uchunguzi na matibabu ya moyo inazozifanya.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo na Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo leo mkoani Iringa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa kambi maalumu ya matibabu ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba.

“Kupitia huduma hii ya tiba mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan JKCI imeweza kufikia mikoa 13 na kuwahudumia wananchi 11,254”, alisema Dkt. Pedro

Dkt. Pedro alisema huu ni mwaka wa pili mfululizo JKCI inafanya kambi maalumu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH) lengo likiwa kuweka nguvu ya pamoja kuhudumia jamii ya watanzania wanaohitaji huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.

Dkt. Pedro alisema Tanzania ni kubwa na JKCI ndio taasisi pekee ya Serikali ya kibingwa ya matibabu ya moyo, hivyo wananchi wote hawawezi kuifikia taasisi hiyo mahali ilipo.

“Tunapokuja katika kambi kama hii tunafahamu siku tano hazitoshi lakini tunaweza kutoa huduma kwa kiwango kile tulichotegemea kufanya angalau wale waliokuwa hawana uwezo wa kusafiri wanapatiwa huduma”, alisema Dkt. Pedro

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH) Dkt. Scholastica Malangalila aliishukuru Wizara ya Afya kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kufikisha huduma za kibingwa kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa.

Dkt. Scholastica alisema kulingana na hali halisi ya wananchi wa Mkoa wa Iringa sio wote wenye shida za moyo wangeweza kufika JKCI kwaajili ya kupatiwa matibabu hivyo kupitia kambi hiyo wananchi wanapata nafasi ya kuchunguza afya zao na wale wenye matatizo ya moyo wanapata nafasi ya kutibiwa.

Dkt. Scholastica alisema mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa kuliko walivyotegemea hivyo kuiomba Taasisi ya Moyo Jakay Kikwete kuendelea kufikisha huduma hiyo ya kibingwa mkoani Iringa mara kwa mara.

“Tumejionea wenyewe tulivyofika hapa asubuhi tayari wananchi walikuwa wamejaa wakisubiri kupata huduma na leo ndio siku ya kwanza naamini siku nne zilizobaki kama wananchi wataendelea kuja kama leo hazitatosha hivyo huduma hii bado inahitajika kwa wananchi wetu”, alisema Dkt. Scholastica

Naye mwananchi aliyepatiwa huduma katika kambi hiyo Selestine Masele aliishukuru Serikali kwa kuwathamini wananchi wake na kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kuthamini afya za wananchi wake.

Selestine alisema uwepo wa wataalamu wa afya mabingwa wa moyo unatoa fursa kwa wananchi kuchunguza afya zao na pale wanapogundulika kuwa na shida za moyo kuanza kuchukua hatua za matibabu mapema.

“Tunawashukuru sana kwa ujio wenu, tunaomba kila mnapopata nafasi mtufikie ili tuweze kujenga tabia za kuchunguza afya zetu mara kwa mara”, alisema Selestine

Kambi hiyo maalumu ya matibabu ya moyo itafanyika katika Hospitali ya IRRH kwa muda wa siku tano ambapo huduma mbalimbali za uchunguzi na matibabu ya moyo zitatolewa ikiwemo huduma za kipimo cha Shinikizo la damu, kipimo cha kuangalia sukari kwenye damu, kipimo cha urefu na uzito, kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO), kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiography – ECG), pamoja na elimu ya lishe kutoka kwa mtaalamu wa lishe.

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari