Zaidi ya watu 11,250 wafikiwa na huduma ya tiba mkoba ya matibabu ya kibingwa ya moyo
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Eva Wakuganda akizungumza na waandishi wa habari leo mkoani Kigoma kuhusu kambi maalumu ya siku tatu ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa – Maweni.
Mratibu wa Huduma za Afya Mkoa wa Kigoma Dkt.Frank Sudai akizungumza na waandishi wa habari leo mkoani humo kuhusu kambi maalumu ya siku tatu ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa – Maweni.
Wananchi wa mkoa wa Kigoma wakisubiria kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa – Maweni katika kambi maalumu ya siku tatu ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayofanyika katika hospitali hiyo.
Mratibu wa Huduma za Kitabibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa – Maweni Dkt.Boniphace Kilangi akizungumza na waandishi wa habari leo mkoani Kigoma kuhusu kambi maalumu ya siku tatu ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa hospitali hiyo.
Wataalamu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa – Maweni wakiwahudumia wananchi waliofika katika hospitali hiyo kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wataalamu hao katika kambi maalumu ya matibabu ya siku tatu.
*******************************************************************************************************************************************************************************************
Zaidi ya Wananchi 11,250 wamefikiwa na huduma ya tiba mkoba ya matibabu ya kibingwa ya moyo kwa kufuatwa mahali walipo ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Hayo yamesemwa leo na daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Eva
Wakuganda wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi maalumu ya
upimaji na matibabu ya moyo inayotolewa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana
na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa – Maweni.
Dkt. Eva alisema kutolewa kwa huduma hiyo katika
mikoa 13 ya Tanzania Bara na Visiwani kumewasaidia wananchi wengi kupata huduma
za matibabu ya kibingwa ya moyo kwa wakati tofauti na ambavyo wangezifuata
huduma hizo jijini Dar es Salaam.
“Kwa wiki hii kuna watalaamu wa JKCI ambao
tuko hapa Kigoma, wenzetu wako Iringa na wengine wako Chato huko kote tunatoa
huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo pamoja na elimu ya jinsi ya
kuepukana na magonjwa haya”.
“Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya
moyo yanaweza kuepukika kwa kufuata ushauri wa kitaalamu ikiwa ni pamoja na
kufanya mazoezi, kutokutumia bidhaa aina ya tumbaku, kula chakula bora na
kutokunywa pombe kupitiliza”, alisema Dkt. Eva.
Dkt. Eva alisema huduma hiyo ni endelevu kutokana
na Taasisi hiyo kufika katika mikoa 13 na baadhi ya wilaya na kuwa na malengo
ya kufika katika mikoa yote ambayo bado haijafika.
“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa
na Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za afya kwa
kununua vifaa tiba vya kisasa pamoja na kuendelea kuwasomesha wataalamu katika
kada ya afya, kutokana na uwekezaji huo matibabu ya kibingwa yanafanyika hapa
nchini tofauti na zamani ambapo wagonjwa walikuwa wanatibiwa nje ya nchi”,
alishukuru Dkt. Eva.
Kwa upande wake Mratibu wa Huduma za Afya Mkoa
wa Kigoma Dkt.Frank Sudai aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kuwatuma wataalamu wake katika mkoa huo ambao
wanashirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa - Maweni kutoa huduma za
uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wananchi.
“Ninawaomba wananchi wa mkoa wa Kigoma na
maeneo ya jirani kutumia fursa hii kufika hospitalini hapa kupata huduma ya
uchunguzi na matibabu ya moyo kwani huduma hii imesogezwa karibu na
kuwapunguzia gharama kama wangesafiri na kuifuata jijini Dar es Salaam”,
alisema Dkt.Sudai.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa – Maweni Dkt. Stanley Binagi, Mratibu wa Huduma za Kitabibu wa
Hospitali hiyo Dkt.Boniphace Kilangi alisema
kufanyika kwa kambi hiyo pia kunawajengea uwezo wataalamu wa hospitali hiyo wa kuwatambua
na kuwatibu wagonjwa wa moyo.
“Kambi hii ni nzuri kwani kila mtaalamu wa
JKCI anafanya kazi na mtaalamu wetu wa hapa hii ikiwa ni pamoja na kufanya
vipimo vya moyo na kuwatibu wagonjwa ninaamini ujuzi wanaoupata wataalamu wetu
utatusaidia katika kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa wagonjwa pindi wenzetu
wa JKCI watakapoondoka”, alisema Dkt. Kilangi.
Katika kambi hiyo ya siku tatu wananchi
wanapata huduma mbalimbali za uchunguzi na matibabu ya moyo ikiwa ni pamoja na kupewa
elimu ya lishe bora na matumizi sahihi ya dawa za moyo, kupimwa uwiano baina ya
urefu na uzito, shinikizo la damu, kiwango cha sukari kwenye damu, kupimwa
vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi pamoja na mfumo wa umeme wa
moyo.
Comments
Post a Comment