JKCI yawafuata wagonjwa majumbani


 Mkurugenzi wa Sakaar Healthtech Limited Pankaj Kumar akimuonesha Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge mfano wa taarifa za mgonjwa aliyeko nyumbani ambaye amefungiwa kifaa kinachojulikana kwa jina la  DOZEE zinavyoonekana kupitia simu ya mkononi ya daktari aliyeunganishwa na kifaa hicho.

Mkurugezi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwaonesha waandishi wa habari kifaa maalumu kinachojulikana kwa jina la DOZEE ambacho kinawekwa chini ya godoro la mgonjwa akiwa nyumbani na kuweza kusoma shinikizo la damu, kiwango cha hewa mwilini, mapigo ya moyo na umeme wa moyo iwapo kutakuwa na shida taarifa itatumwa moja kwa moja kwa daktari kupitia simu yake ya mkononi ambayo imeunganishwa na kifaa hicho.


 Mkurugezi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwaonesha waandishi wa habari kifaa maalumu kijulikanacho kwa jina la DOZEE kinachotumika kufuatilia maendeleo ya mgonjwa anayetibiwa akiwa nyumbani huku daktari akipata taarifa zote kupitia simu yake ya mkononi ambayo imeunganishwa na kifaa hicho.

Mkurugezi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu Taasisi hiyo kutoa huduma ya kuwafuata wagonjwa majumbani mwao na kuwapatia tiba wanayostahili.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI) Smita Bhalia akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam aina za huduma za kuwafuata wagonjwa majumbani mwao na kuwapatia tiba wanayostahili zinakazotolewa na Taasisi hiyo. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge.

***************************************************************************************************************************************************************************************

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeanza kutoa huduma ya kuwafuata  wagonjwa manyumbani mwao na kuwapa tiba wanayostahili.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu huduma hiyo.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema huduma hiyo itasaidia kupunguza vifo vya ghafla vya wagonjwa pamoja na kuokoa muda wa kuwapeleka hospitali.  

Mkurugenzi huyo Mtendaji alisema huduma hiyo itakuwa ni maalumu kwa wagonjwa ambao walilazwa hospitali na wameruhusiwa kurudi nyumbani lakini pia wanahitaji kupata huduma ya uangalizi maalumu kwani wagonjwa hao shinikizo lao la damu linaweza kushuka au kuwa juu sana na kuwasababishia kifo cha ghafla.

“Hii ni huduma mpya ya teknelojia ya hali ya juu ambapo chini ya godoro la mgonjwa kitawekwa kifaa maalumu kinachojulikana kwa jina la DOZEE  ambacho kinamtetemo na kuweza  kusoma shinikizo la damu, kiwango cha hewa mwilini, mapigo ya moyo na umeme wa moyo iwapo kutakuwa na shida taarifa itatumwa moja kwa moja kwa daktari kupitia simu yake ya mkononi ambayo itakuwa imeunganishwa na kifaa hicho”.

“Baada ya daktari kupata taarifa tutatuma gari la wagonjwa ambalo litakuwa na daktari bingwa wa moyo pamoja na muuguzi ambao watakwenda kumuhudumia mgonjwa pia tutamuelekeza ndugu wa mgonjwa nini afanye wakati wataalamu wetu wanakwenda kutoa huduma kwa mgonjwa”, alisema Dkt. Kisenge.

Dkt.Kisenge alisema huduma hiyo pia itawasaidia wagonjwa ambao wamekaa hospitali muda mrefu na wanataka kukaa karibu na ndugu zao nyumbani na wagonjwa ambao ni watu wazima sana ambao watahitaji kutibiwa wakiwa nyumbani.

“Upatikanaji wa huduma hizi za matibabu ya kisasa ni jitihada za Mhe. Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma za afya nchini, hivi sasa katika Taasisi yetu tuna magari ya wagonjwa sita ambayo yanatusaidia kutoa huduma kwa wagonjwa”, alisema Dkt. Kisenge.

Akizungumza kuhusu huduma nyingine zitakazotolewa kwa wagonjwa walioko majumbani daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Smitha Bhalia alisema ni pamoja na wagonjwa waliopata kiharusi ambao watapata huduma ya mazoezi ya viungo na wenye shida ya lishe  watapewa ushauri na kuelekezwa vyakula gani watumie.

Dkt. Smitha alisema wagonjwa wengine ambao watapata huduma ya kufuatwa nyumbani ni wale ambao amefanyiwa upasuaji wa moyo na wanahitaji kusafishwa kidonda wauguzi watawafuata na kuwapa huduma hiyo pia kuna wagonjwa ambao wanahitaji kukaa na muuguzi wa kumuhudumia kwa saa 24 nao pia watapata huduma hiyo.

“Huduma hizi zitatolewa kwa wagonjwa ambao wamepimwa na kuonekana kuwa wanaweza kupata huduma wakiwa nyumbani na kwa ambao hali yao haiwaruhusu kutibiwa wakiwa nyumbani watapelekwa JKCI kwaajili ya matibabu”.

“Kuna huduma ya gari la wagonjwa ambapo mgonjwa akizidiwa atapiga simu namba 0688027982 na 0788308999 nasi tutamfuata na kwenda kumuhudumia, tutaangalia maendeleo ya afya yake na kuona kama tumlete hospitali au abaki nyumbani na kuendelea na dawa”, alisema Dkt. Smitha.


Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari